07 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Leo ni leo
 
2008-05-07 19:45:19
Na Mwandishi, Bariadi

Leo ni leo! Kile kitendawili kuhusu ukweli juu ya sakata la vijisenti vya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Bwana Andrew Chenge, huenda leo kikapata jibu wakati mwanasiasa huyo atakapotua kwenye jimbo lake, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipokumbwa na zahama hilo.

Taarifa za kuaminika zinasema, Bw. Chenge ameondoka leo saa 4:00 asubuhi mjini Mwanza, kuelekea jimboni mwake Bariadi Magharibi. Imeelezwa kuwa Chenge alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza jana jioni.

Kwa mujibu wa ratiba iliyoandaliwa, Bw. Chenge amepanga kuhutubia wananchi kuanzia saa kumi jioni, mkutano utakaofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Manispaa ya Bariadi.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wanasema, wanasubiri kwa hamu kubwa hotuba hiyo kwani wana matumaini mbunge wao huyo, atawaeleza ukweli kuhusu sakata linalomkabili.

Bw. Chenge alilazimika kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri baada ya Taasisi ya kuzuia rushwa kubwa ya nchini Uingereza, SFO, kufichua akaunti yake yenye kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja katika visiwa vya New Jersey.

Pesa hizo zilihusishwa na ununuzi wa rada ambao mazingira yake yanadaiwa kugubikwa na rushwa. Wakati rada inanunuliwa, Bw. Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Habari zaidi kutoka mjini Bariadi zinasema tangu juzi, mji huo ulikuwa umeshaanza kufurika watu waliokuwa kwenye hekaheka za mapokezi ya mbunge huyo.

Habari zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zinadai kuwa Bw. Chenge anasema ziara yake hiyo hailengi kwenda kujisafisha bali kuhamasisha miradi ya maendeleo jimboni mwake.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.