|
Usaili Copa Coca cola TMK tamati
2008-05-08 14:39:52
By Chile Kasoga, Jijini
Usaili kwa ajili ya wachezaji watakaoshiriki michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya Copa Coca cola `mkoani` Temeke, unakamilika leo ili kupisha kwa michuano hiyo mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na Alasiri kwa niaba ya katibu mkuu, mjumbe wa Chama cha Soka wilayani Temeke, TEFA, Fikiri Magoso, amesema timu zote ambazo hazijakamilisha taratibu za usaili zinatakiwa kufanya hivyo kabla ya saa 12 jioni.
Magoso amesema klabu zilizojitokeza kuchukua na kurudisha fomu katika mashindano hayo ya vijana ya mwaka huu ni klabu 28 pekee.
``Suala la umri kwa vijana wetu tumelipa kipaumbele mkubwa sana kwa kuwa tunataka kupata timu za vijana wenye damu changa watakaoleta ushindani mkubwa,`` amesema Magoso.
Ameongeza, kwa mwaka huu klabu nyingi zilizojitokeza zimefuata sifa zote zinazokubalika na waandaaji wa mashindano hayo hivyo kufanya zoezi la kusajili klabu mpya kwenda vizuri.
Amezitaja baadhi ya klabu zilizojitokeza kuchukua fomu ni Panama Kids, Soweto, Tandika Kids, Tayfa, Ngwele Academia, Twalipo, Tiger na Elite Soccer Academy.
Nyingine ni Umoja, Redfish, Bernabeu, Chang`ombe Youth, TMK Family, BM International, Vimto, DYOC na Serengeti.
|