|
Wachezaji Stars wapozwa
2008-05-08 14:40:45
By Somoe Ng\'itu, Posta Mpya
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) jana ilitoa kiasi cha Dola za Marekani 100 kwa kila mchezaji wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars ikiwa ni kwa ajili ya motisha ya ushindi walioupata katika mechi ya kwanza ya mashindano ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda, The Cranes.
Katika mechi hiyo Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza ambapo umehusisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani pekee.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SBL, Paul Bomani, alisema kuwa kampuni hiyo imeamua kuwapa wachezaji fedha hizo ili kuwaongezea morali na kujiamini zaidi katika mchezo wa marudiano ambao umepangwa kufanyika Mei 17, kwenye uwanja wa Namboole jijini Kampala.
Bomani alisema kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na Shirikisho la soka nchini (TFF) ili kufanikisha kuwa timu hiyo inafanya vizuri na inatafanikiwa kucheza fainali za mashindano hayo.
Mgeni rasmi katika tafrija hiyo fupi iliyoandaliwa na SBL jana usiku, Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, George Mkuchika aliwapongeza wachezaji kwa ushindi walioupata na kusema kuwa hali hiyo imewapa raha Watanzania.
|