|
Simba wamjia juu bosi wao
2008-05-08 14:41:43
By Jacqueline Massano, Jijini
Baadhi ya wanachama wa Simba, wamempinga katibu mwenezi wa klabu hiyo, Said Rubeya wakidai hana mamlaka ya kuupeleka mkutano mkuu mbele.
Kauli ya wanachama hao, imekuja siku moja baada ya Rubeya kudai mkutano wa klabu hiyo utafanyika mwezi ujao badala ya huu.
Akizungumza na Alasiri jana, mwanachama wa klabu hiyo, Juma Mnonja amesema wao kama wanachama wanania njema na klabu yao na ndiyo maana wanahitaji mkutano huo ufanyike mapema na wala si kugosezwa mbele kiholela.
``Akumbuke kuwa nasi tuna haki, na tunahitaji kufahamu kile kinachoendelea ndani ya klabu yetu, hivyo suala la yeye kudai mkutano utafanyika Juni, hatutendei haki kabisa,`` amesema.
Mnonja amesema mara kwa mara uongozi wao hautaki kuweka mambo ya klabu hadharani ili yafahamike na wanachama.
Naye Stambuli Mponda amesema wanachohitaji kufahamu ni usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao kwani wanaimani kuwa uongozi peke yao hauwezi kufanikisha hilo.
``Wanachama tunaona mbali, ndiyo maana tunataka mkutano haraka, kwani hadi sasa tunasikia wachezaji wengi wanaondoka, hivyo kulidhibiti hilo tunatakiwa kukutana ili tujue jinsi gani ya kusaidiana,`` amesema.
Mponda amesema wao kama wanachama wanapenda kuona klabu yao inakuwa na mafanikio hata kama imenyang`anywa ubingwa wa Ligi Kuu.
|