08 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

CHADEMA yasema ufisadi nchini unazizima hadi Ulaya
 
2008-05-08 14:43:38
Na Sharon Sauwa, Mikocheni

Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), kimebanwa na maswali kibao katika ziara yao ya nchi za Scandinavia yanayohusiana na vita dhidi ya ufisadi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa na Mkurugenzi wa Vijana wa Taifa, Bw. John Mnyika, amesema kuwa katika nchi za Sweden na Norway walizotembelea wamekumbana na maswali kutoka kwa washirika wao kuhusiana na masuala mbalimbali ya ufisadi yanayolitikisa taifa la Tanzania.

Akasema katika ziara za nchi hizo ambazo ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa Tanzania katika maendeleo, wamekuwa wakikumbana na suala hilo na kisha kupongezwa kwa jitihada zao katika kuibua masuala mbalimbali yanayohusiana na ufisadi.

``Lakini kote huko, sisi msimamo wetu kila mara umekuwa ni ule wa kutaka wasitunyime misaada kwa sababu ya kashfa ya watu wachache... na siku zote tutaendelea kusema hivyo,`` akasema.

Akatoa mfano wa nchi ya Norway ambayo katika siku alizokaa nchini humo wamekumbana na taarifa zinazohusiana na ufisadi nchini Tanzania kila siku.

Akasema hali hiyo imekuwa ikiwapa hofu watu wa nchi hizo kwa sababu fedha zinazoletwa kusaidia nchini zinatokana na kodi za wananchi wao.

Bw. Mnyika akasema kwa upande wao wamewashauri kuendelea kuvipa nguvu vyama vya upinzani ili viweze kuongeza idadi ya wabunge na hivyo kuongeza nguvu ya kupambana na ufisadi.

Akasema timu ya kwanza ya Chadema imetua nchini Aprili 28 mwaka huu baada ya kukaa katika nchi hizo za Scandinavia kwa wiki moja.

Akasema mpango huo wa ziara za nchi marafiki umeanza mwaka jana ambapo katika kipindi cha mwaka uliopita, walikwenda wanachama wawili.

Akasema ziara hizo zinalenga katika kujifunza na kukutana na wadau mbalimbali wa masuala ya demokrasia na maendeleo.
Kwa mujibu wa Bw. Mnyika, ujumbe wa wanachama wanne kutoka Chadema uliongozwa na yeye.

Akawataja wajumbe katika ziara hiyo kuwa ni wabunge wawili, Bw. Mhonga Said Ruhanywa, Bi. Maulidah Anna Komu na Afisa Mwandamizi wa Uchaguzi toka makao makuu Bi. Suzan Kiwanga.
Akasema wakiwa nchini Sweden, walikutana na wajumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Pia akasema katika kikao hicho Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika, Balozi Andes Hagelberg pamoja na Mshauri wa Tanzania, Bw. Johan Rydberg walishiriki katika mazungumzo hayo ya pamoja.

Akayataja mambo mengine yaliyozungumzwa kuwa ni mfumo wa vyama, ufanisi wa Bunge na amani nchini Burundi.

Aidha, akasema ziara hiyo ilihusisha kutembelea Ofisi za Jiji la Stockholm na kuzungumza na maofisa wa Jiji hilo kuhusu masuala ya maendeleo, usafiri katika jiji na huduma za afya zinazotolewa na Serikali.

Akasema mbali na shughuli hizo, pia ujumbe wa Chadema ulikutana na wabunge wa chama cha Moderate kinachotawala nchi hiyo, Bi. Sofia Arkelsten na Ewa Thalén Finné, na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu harakati za mazingira, makazi na ushiriki wa wanawake katika siasa.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.