|
Denti Jijini asombwa na maji na kufariki
2008-05-08 14:46:09
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Watu wawili wamefariki dunia Jijini katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mwanafunzi wa darasa la tatu aliyekufa maji wakati akiogelea mtoni.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kandihabi, amesema tukio la kwanza limetokea jana mishale ya saa 3:00 asubuhi katika eneo la Temeke Kilungule kunako Mto Kilungule.
Amesema mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kingugi aitwaye Issa Njigama, 12, akiwa anaogelea katika mto huo wa Kilungule, alikwenda katika maji yenye kina kirefu na kuzidiwa nguvu kabla hajazama, kunywa maji mengi na hatimaye kufariki dunia.
Amesema maiti ya mwanafunzi huyo imeopolewa toka majini na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke.
Katika tukio jingine, Kamanda Kandihabi amesema mwili wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 30 umekutwa kandokando ya barabara ya Mandela, eneo la Serengeti, ukiwa na majeraha mbalimbali mwilini.
Amesema mwili wa mwanaume huyo umegunduliwa leo, mishale ya saa 1:30 asubuhi, ukiwa umetupwa huku ukiwa na majeraha ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali katika sehemu ya jicho la kushoto, mdomoni na kwenye kidevu.
Aidha, amesema maiti ya mtu huyo ilikuwa imefungwa kwa kamba mikononi na miguuni, ambazo ni viti vya gari vilivyochanwachanwa na kufanywa kamba na kisha kutupwa katika mtaro.
Amesema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na msako zaidi unaendelea.
Wakati huo huo, moto unaosadikika kusababishwa na hitilafu ya umeme umeteketeza sehemu ya chini ya ghorofa moja huko Kariakoo inayotumiwa kuhifadhi matairi na betri za magari.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile, amesema tukio hilo limetokea leo mishale ya saa 7:00 usiku katika ghorofa linalomilikiwa na mfanyabiashara aliyetambulika kwa jina la Nile Altars, 45.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitalafu ya umeme na thamani ya mali iliyoteketea bado haijafahamika.
Amesema hadi polisi inapata taarifa hizi, moto huo ulikuwa haujazimwa na wananchi, kikosi cha jiji cha zimamoto na Shirika la Umeme nchini, TANESCO, walikuwa wakiendelea na shughuli ya kuuzima moto huo.
|