|
Chenge atikisa
2008-05-08 14:47:47
Na Mwandishi wetu, Bariadi
Wale waliodhani kwamba aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bwana Andrew Chenge, angepata wakati mgumu kuwakabili wapiga kura wake, wameula wa chuya.
Alipoingia Bariadi Magharibi jana, alipagawisha ile mbaya.
Hadi leo, katika mji mzima bado watu wanazunguzia ujio wa mheshimiwa huyo ambaye hivi sasa amepachikwa jina la Mzee wa Vijisenti.
Kilichopagawisha kwanza ni msafara wa mwanasiasa huyo ambao watu walioshuhudia wanadai, ulianzia Mwanza mjini huku ukiwa na magari kibao ambayo kwa hesabu ya haraka haraka yangeweza kufikia hata ishirini na mbili.
Wanadai kuwa msafara huo ulipowasili huko Bariadi Magharibi, ulipokelewa na viongozi wa CCM pamoja na wafanyabiashara wakubwa wa Wilaya ya Bariadi katika mji mdogo wa Lamadi.
Kutoka mjini Lamadi, mashuhuda wanasema, msafara huo, uliongezewa magari na yakafikia kama sabini hivi.
Wakasema baada hapo, walianza safari, wakipitia katika vijiji vya Dutwa na Sapiwi, ambako Bw. Chenge alilazimika kusimama kusalimiana na wapiga kura wake waliokuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa.
Jioni ya jana Bw. Chenge alihutubia wananchi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mpira wa Manispaa ya Bariadi maarufu kama Uwanja wa Sabasaba.
Katika mkutano huo, Bw. Chenge aliwaambia wananchi kuwa tuhuma zote zilizoelekezwa kwake na kusababisha ajiuzulu ni uzushi mtupu na kuwa yeye ni mtu safi.
Bw. Chenge akawataka wapiga kura wake wasiyumbishwe na tuhuma zinazoelekezwa kwake, na badala yake washikamane na kufanya mambo yatakayowaletea maendeleo yao.
Bw. Chenge alipagawisha zaidi pale alipoibuka na msamiati mpya. Alijiita nyumba imara itakayowasaidia sana wananchi kuwaletea maendeleo na akawataka wazidi kuijenga.
``Jengeni nyumba imara ili iendelee kuwasaidia, mimi ndiyo nyumba imara... La msingi kwetu ni kushikamana msivunjike moyo,`` akasema Bw. Chenge.
Kilichowafurahisha zaidi wapiga kura wake ni pale mbunge huyo alipokuwa akichanganya Kiswahili na Kisukuma.
Chenge alijiuzulu uwaziri wa miundombinu hivi karibuni baada ya kuwepo na taarifa kuwa ana akaunti katika kisiwa cha New Jersey nchini Uingereza iliyo na zaidi ya Sh. bilioni moja.
Taarifa zilieleza kuwa mapesa hayo ya akaunti ya nje ya Chenge yanachunguzwa na Taasisi ya Kuchunguza Rushwa kubwa kubwa nchini Uingereza, SFO ili kujua kama ni malipo aliyopewa baada ya kushiriki `dili` la ununuzi wa rada ya mabilioni ya pesa toka katika kampuni ya BAE System ya nchini humo, wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu katika Serikali ya awamu ya tatu.
Hata hivyo, Chenge aliporejea nchini toka kwenye ziara ya Rais Kikwete nchini India na kuhojiwa na waandishi kuhusiana na madai kuwa ana akaunti nje ya nchi yenye zaidi ya Sh. Bilioni moja, akakaririwa akiziita pesa hizo kuwa ni vijisenti tu, jambo lililozusha gumzo kubwa.
Baadaye, Chenge alimuandikia barua ya kuomba kujiuzulu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Jakaya Kikwete, ombi ambalo lilikubaliwa na hivyo kumfanya abakie na nafasi za uongozi anazoshikilia ndani ya CCM na pia ile ya ubunge wa jimbo la Bariadi Magharibi.
|