|
Uchaguzi wa wazazi CCM Kinondoni waahirishwa
2008-05-12 18:36:16
Na Abdul Mitumba, Kinondoni
Uchaguzi mkuu wa viongozi wa Jumiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, ngazi ya matawi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki wilayani Kinondoni Jijini umekwama, imefahamika.
Kukwama huko kumekuja baada ya Baraza Kuu la Jumuiya hiyo taifa kuagiza chaguzi zote za jumuiya hiyo zikiwemo za UVCCM na UWT zisimamishwe hadi hapo yatakapotolewa maelekezo mengine.
Hatua hiyo limekuja siku chache tangu kufanyika kwa semina elekezi kwa wasimamizi kutoka kata zote 27 za wilaya ya Kinondoni ambao walitarajiwa kusimamia uchaguzi huo.
Kulingana na barua ya kuahirisha uchaguzi huo iliyosambazwa juzi na kusainiwa na katibu wa jumuiya hiyo wilayani humo, Bw. Stanley Mkandawile, inasema hatua hiyo imetokana na agizo la uongozi wa juu wa jumuiya yao.
``Nimepokea barua kutoka mkoani na makao makuu Mei 8 ikitoa mwaka huu ikitioa maelekezo ya kunitaka nisitishe zoezi la uchaguzi mkuu wa wazazi mpaka hapo vikao vya juu vya chama na jumuiya vitakapoketi ns kupitisha kanuni na kalenda ya uchaguzi,`` imesema taarifa hiyo ya Bw. Mkandawile.
``Kwa barua hii nawaagiza kusitisha zoezi la uchaguzi kwa ngazi zote hadi tutakapopata maelekezo mengine.
Pia kwa kipindi hiki elekezeni nguvu katika kuingiza wanachama wapya na kuhimiza ulipaji wa ada,``imesema.
Nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Katibu wa CCM Kinondoni, Wenyeviti na Makatibu wa wazazi kata zote za Kinondoni na wajumbe wa kamati za utekelezaji za wazazi Kinondoni kwa taarifa.
|