|
Diwani ataka mafunzo ya ukimwi na ujasiriamali vijijini
2008-05-12 18:40:30
Na Abdul Mitumba, Kariakoo
Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Ilala Jijini, Bi. Asha Sururu, ametoa changamoto kwa Serikali na asasi binafsi kuelekeza mafunzo ya ukimwi na ujasiriamali vijijini ili kujenga uwiano wa uelewa kwa wananchi wa maeneo yote.
Aidha, diwani hiyo, amesema endapo mafunzo hayo yataendelea kutolewa zaidi mijini, ukubwa wa tatizo la maambukizi ya ukimwi utaongezeka kwa sababu vijijini ndiko kwenye wakazi wengi.
Diwani Sururu amesema hayo alipozungumza na Alasiri kueleza umuhimu wa asasi binafsi kujengezwa uwezo ili zimudu kupeleka mafunzo ya UKIMWI na ujariamali vijijini.
``Sisemi kwamba wakazi wa mijini wametosheka na mafunzo hayo la hasha, isipokuwa kwa kiasi kikubwa wameelimishwa vya kutosha na sasa, nadhani kuna haja ya kuelekeza nguvu kubwa vijijini,`` akasema.
Amesema tangu UKIMWI ugundulike kuwepo nchini mwaka 1983, serikali na taasisi za kiraia zimekuwa zikitoa elimu ya kujijkinga na ugonjwa huo pamoja na ujasiriamali mijini zaidi na kusahau mafunzo hayo vijijini.
``Watu wanasahau kwamba asilimia kubwa ya watu wenye UKIMWI hukimbilia makwao wakiwa bado na nguvu ambapo huko huambukiza wengine wasio na elimu yoyote ya jinsi ya kujikinga,`` akasema.
Amesema kwa kawaida watu wanaoishi mijini na kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI, hukimbilia vijijini wanapogundua hawana msaada wa kutosha mijini, hali inayochangia maambukizi huko waendako.
|