|
Madiwani kutembelea vituo vyote vya yatima Kinondoni
2008-05-13 17:50:23
Na Grace Chilongola, PST - Jijini
Madiwani katika manispaa ya Kinondoni wameanza ziara ya kutembelea vituo vya watoto yatima ili kutambua matatizo yanayowakabili.
Ziara hiyo ya siku tatu ni moja ya utekelezaji wa majukumu yao ya kuhakikisha kuwa watoto hao wanahudumiwa ipasavyo, mbali na kujiridhisha kuwa wanafaidika na misaada inayotolewa kwao na manispaa.
Akizungumza na PST, Afisa Habari wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Martha Kawishe, amesema lengo lao ni kuboresha misaada wanayopatiwa yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuhakikisha kuwa yenyewe hailengi zaidi chakula kama ilivyo sasa na badala yake iwe pia ikizingatia upatikanaji wa maendeleo ya kielimu.
Amesema ziara hiyo itawawezesha madiwani kufahamu idadi halisi ya vituo ya kulelea yatima vilivyopo katika manispaa yao na kuhakikisha kuwa watoto waliopo kwenye vituo hivyo, wanahudumiwa na hawafanyishwi shughuli zilizo kinyume na utaratibu.
Bi. Kawishe amesema baadhi ya wamiliki wa vituo vya kulelea yatima wamebainika kutokuwa na maeneo ya kutosha kwa watoto kucheza kwani vituo vingi huwa ni nyumba za kuishi familia na hazikujengwa kwa malezi ya watoto wengi.
Ameongeza kuwa wamiliki wengine wa vituo hivyo wamekuwa wakijipatia misaada kutoka kwa wahisani kwa ajili ya kuwasaidia watoto lakini matumizi yake yamekuwa kinyume na makusudio kwani wamekuwa wakijinufaishi wenyewe kupitia watoto yatima.
Ameongeza kuwa watoto yatima wanahitaji misaada pamoja na upendo kutoka kwenye jamii inayowazunguka na watu wote ili wasijisikie wanyonge mbele ya wenzao.
Hadi sasa Manispaa ya Kinondoni ina jumla ya vituo vya kulelea watoto yatima vipatavyo 30 wakati 18 vimekuwa vikipatiwa misaada.
|