|
Manispaa Temeke yaunda tume kubaini waliouza eneo la shule
2008-05-15 19:51:38
Na Frank Mbunda, Temeke
Manispaa ya Temeke imeunda Tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa sakata la kuuzwa kwa eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule katika kata ya Sandali.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Manispaa hiyo zimesema kuwa kamati hiyo ya watu watano, itafanya kazi ya kuchunguza uhahali wa kuuzwa kwa eneo hilo.
Aidha, habari zimesema kwamba maamuzi ya kuundwa kwa tume hiyo, ni kutaka kupata ukweli kuwa baadhi ya maafisa wake walihusika kusaidia kuuzwa kwa eneo hilo.
Imeelezwa na baadhi ya maafisa kuwa maamuzi hayo yanatokana na kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. John Guninita.
Bw. Guninita alidaiwa kusema katika kikao cha Aprili 11 mwaka huu kwamba Diwani wa Kata hiyo, Bw. Abel Tarimo, hakuhusika kuuza eneo hilo na badala yake akasema waliohusika na uuzaji wa eneo hilo ni baadhi ya maofisa wa Manispaa ya Temeke.
Mbali na kudaiwa kusimamia uuzaji wa eneo hilo, pia tume hiyo itamchunguza diwani Tarimo, anayetuhumiwa kuwa alitoa kauli juu ya eneo hilo kupigwa bei.
Hata hivyo, Bw. Guninita alipoulizwa kuhusu hatua ya kuundwa kwa tume hiyo, alisema hayo ni maamuzi ya manispaa katika kujichunguza yenyewe.
Ni kweli nilisema hivyo, tena mbele ya Meya Mstahiki Meya Bw. Jerome Bwanausi, hasa baada ya kuona kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinamsakama diwani Tarimo,`` akasema Bw. Guninita.
Alipoulizwa, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Bw. Stephen Kongwa, amekiri kuundwa kwa tume hiyo na kueleza kuwa inatarajiwa kumaliza kazi yake hivi karibuni.
Akasema kazi ya tume hiyo inaendelea vizuri na kwamba taarifa ya sakata hilo zitatolewa kwa umma baada ya kukabidhiwa kwao.
Ni kweli tumeunda tume kwa ajili ya kuchunguza suala hilo. Naomba kwa sasa uniache, lakini tutaweza kutoa taarifa kamili baadaye, akasema Bw. Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Luteni Abdallah Kihato, amekiri kuwapo kwa taarifa za kuuzwa kwa eneo hilo na kusema kuwa ameshaagiza eneo hilo lirejeshwa mikononi mwa Serikali.
Ni kweli kuna taarifa za kuuzwa kwa eneo hilo na wahusika waliotajwa kuwa ni pamoja na diwani na mtendaji wa kata... lakini nilikwenda katika eneo hilo haraka sana baada ya kuombwa na wananchi,amesema Luteni Mstaafu Kihato.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa baada ya kufanya uchunguzi, alibaini mapungufu na hivyo aliagiza kufutwa kwa ofa ya kumilikishwa mwekezaji katika eneo hilo.
|