|
Mtoto Dar atumbukia kwenye karo na kufa
2008-05-15 19:53:40
Na Sharon Sauwa, Jijini
Mtoto Frank Damas, 6, mkazi wa Mtaa wa Kisaga katika eneo la Kinondoni B Jijini amefariki dunia baada ya kutumbukia katika karo la maji yaliyoandaliwa kwa ajili ya kujengea nyumba.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jamal Rwambow, amesema tukio hilo lilitokea jana mishale ya saa 11:00 jioni wakati mtoto huyo akicheza na wenzake.
Amesema mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huohuo, wakazi wawili wa Jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukamatwa wakiwa na kete 76 za bangi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Kandihabi amesema watu hao walikamatwa jana mishale ya saa 10:00 jioni pale katika eneo la Charambe Machinjioni.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Nasoro Maweja, 20, na Yusuf Salum, 28.
Katika tukio jingine, watu watano wamekamatwa na Polisi wakiwa na lita nne za gongo.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile amesema watu hao walikamatwa jana mishale ya saa 3:00 usiku, katika maeneo ya Feri.
Akawataja watu hao kuwa ni Juma Ali, 32, Hanadi Singumbi ,20, Huruka Mwinchande, 25, Lazaro Gervas, 32 na Kidau Ali mwenye miaka 36.
|