|
Tendwa aja juu
2008-05-15 19:56:06
Na Sharon Sauwa, Mikocheni
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa, amevijia juu vyama vya CUF na CCM na kuvitaka viache malumbano yao ya sasa yanayoweza kuwapeleka Watanzania kule ambako kamwe hawakujui na badala yake watumie busara zaidi katika kumaliza tofauti zao.
Akizungumza katika mahojiano maluum na Alasiri jana, Bw. Tendwa amesema kutokana na mahali yalipofikia mazungumzo hayo ya vyama vya CUF na CCM, ni wazi kwamba vyama hivyo vinapaswa kutulia na kusaka mtu wa tatu atakayeweza kutuliza jazba zao na hatimaye kuwapatanisha, badala ya sasa ambapo wamekuwa wakiendeleza malumbano yasiyoashiria mwisho mwema.
``Imefikia mahala ambapo vyama viwili hivi vya siasa vinapaswa kutulia na kuacha malumbano... nadhani sasa inatosha, walipofikia panatosha,`` akasema.
Akasema mazungumzo ya mara ya kwanza ya vyama hivyo vya kisiasa ya mwaka 2001, yaliijengea nchi heshima kubwa duniani.
``Lakini sasa vyama hivi vinatutoa katika lengo na kutupeleka tusipokujua, busara inahitaji kutumika ili kurudi katika njia yenye mwelekeo sahihi,`` akasema.
Akasema tatizo kubwa ni kwamba wamefanya mazungumzo wao wenyewe (CCM na CUF), bila kumshirikisha mtu mwingine wa kati.
Akasema kungekuwa na mtu wa kati angeliweza kuzuia ghadhabu, hisia na jazba na hivyo kungekuwa hakuna haja ya kulumbana.
Akasema kilichotokea ni kwamba upande mmoja ulikosa uvumilivu.
Pia akasema kutokea kwa mlipuko wa hisia za kutoaminiana ni hatari sana.
Alipohojiwa kuhusiana na hatua anazochukua, Bw. Tendwa akavitaka vyama hivyo kunyamaza na kutafakari kwa sababu muafaka unaleta maisha bora na ni jambo jema sana.
Pia akasema kwakuwa mambo hayo yanahusu vyama viwili vya siasa, yeye kama msajili wa vyama vya siasa ana wajibu wa kuviangalia kwa mujibu wa sheria na kuwasaidia kurejea katika mazungumzo.
Akasema ingawa CUF hivi sasa hawamtaki Katibu Mkuu Bw. Yusuf Makamba kuwemo katika timu hiyo ya muafaka, bado wanaweza kukaa na kutazama mambo mengine yatakayowawezesha kurejea katika meza ya mazungumzo badala ya kususia.
Hadi sasa, vyama hivyo vimeendelea kulumbana vikali huku kila kimoja kikilaumu kingine kwa kukiuka mambo waliyokubaliana.
Chama cha CCM kinaitupia lawama CUF kuwa kimeudanganya umma wa Watanzania kuhusiana na masuala ya muafaka.
CUF nao wanalalamikia agenda ya kulirejesha suala hilo kwa wananchi ili walipigie kura kuwa halipo katika agenda za mazungumzo ya muafaka, huku wakidai kuwa wenzao wa CCM wanafanya `usanii` wa kisiasa katika jambo kubwa na lenye maslahi kwa taifa.
|