|
...Mapinduzi yanukia
2008-05-16 15:53:23
By Onesmo Kapinga, Msimbazi
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba upo kwenye hatihati ya kupinduliwa kwa madai kuwa umeshidwa kuongoza klabu hiyo.
Wakizungumza a Alasiri jana jioni baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamesema uongozi huo hautadumu madarakani zaidi ya miezi miwili kuanzia sasa.
Wamesema pamoja na Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba Hassan Dalali kudai mkutano mkuu wa wanachama unatafanyika Agosti mwaka huu, lakini hauwezi kufika hadi mwezi huo.
``Sisi tunakuambia viongozi hao hawafiki Juni watakuwa wameng`olewa,`` amesema mmoja wa wanachama hao ambao hakutaka majina yao yaandikwe gazetini.
Hata hivyo wamesema viongozi hao wameshindwa kuongoza klabu hiyo na badala yake wamekuwa wakigombana wao kwa wao.
Wakati huo huo, Dalali amesema mkutano wa mapato na matumizi utaitishwa Agosti mwaka huu.
``Tunataka kufanya mkutano wetu kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara,`` amesema Dalali.
Dalali amesema mkutano ambao ni muhimu pia wanachama watapata fursa ya kujadili suala la kusimamishwa kwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda.
Kaduguda amesimamishwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, kwa muda usiojulikana kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
|