|
Siongozi Simba kidikteta - Dalali
2008-05-16 15:57:04
By Badru Kimwaga, Jijini
Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba, Hassani Dalali, amedai haioOngozi klabu hiyo kidikteta kutokana na kushindwa kwake kuitisha mkutano mkuu wa wanachama, isipokuwa katiba mpya imembana kufanya hivyo.
Aidha, Dalali amewataka wanachama wa klabu hiyo, kuwa watulivu na kuacha kusikiliza maneno ya uchochezi yanayosambazwa na kundi la wanachama wachache kuhusiana na mkutano huo kwa lengo la kuvuruga amani na utulivu ndani ya klabu.
Akizungumza na Alasiri jana kwa njia ya simu, Dalali amesema siku zote amekuwa kinara wa kutaka demokrasia kufuatwa ndani ya Simba na katu hawezi kwenda kinyume na kuendesha klabu kidikteta.
Amesema kushindwa kuitishwa kwa mkutano kumetokana na zoezi la ugawaji wa kadi mpya kwa wanachama zaidi ya 6000, na hivyo kufanya kikwazo cha kufanyika kwa mkutano huo, ambao huenda ukafanyika baada ya miezi mitatu ijayo.
``Siongozi kama dikteta kwa kugoma kuitisha mkutano mkuu, lakini tujiulize tukiitisha mkutano wanachama wapya watapataje fursa ya kushiriki, hii inaweza kuleta matatizo zaidi Simba,`` amesema Dalali.
Kiongozi huyo amesema wanachama wapya na wa zamani waliopitishwa kwa mujibu wa katiba mpya wanapaswa kupewa kadi zao na kutambuliwa rasmi, ndio maana wanakazania hilo.
``Wanaolazimisha kudai mkutano ni wale waliokabidhiwa kadi zao, lakini kama wasingepewa wangesubiri kama wengine waliotuliwa wakisubiri kupewa kadi zao na kuruhsiwa kuhudhuria mkutano huo,``
Dalali ameongeza kwa kusema wanachama wasiowe wepesi wa kusikiliza majungu na badala yake kuwa watulivu wakisubiri maagizo ya viongozi wao na kusema mkutano wao utafanyika mwezi Agosti.
``Mkutano utafanyika Agosti na hivyo wanachama watulie kwani lau tungekuwa tunaogopa mikutano nisingeitisha mikutano mitano ndani ya mwaka mmoja, pia au kwa vile mie mswahili, mbona Kassim Dewji aligawa kadi mpya kwa muda wa mwaka mzima?``
Dalali alihoji na kusema kuwa zoezi lao la kusajili na kugawa kadi mpya ndio kwanza lina muda wa miezi sita na hivyo hakuna haja wanachama wakaanza `kuwaka`, akisema mkutano mkuu ni haki yao na wao uongozi hawana jeuri ya kuukwepa.
Kauli ya Dalali imekuja siku chache baada ya kundi la wanachama kuulalamikia uongozi juu ya kuupiga danadana mkutano huo wakidai kuwa mwenyekiti huyo anaendesha Simba kibabe na kidikteta.
|