|
Chenge: Mambo magumu!
2008-05-16 16:15:55
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Mambo yameanza kuwa magumu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, baada ya uchunguzi wa mapesa yake zaidi ya Sh. Bilioni Moja na ambayo mwenyewe ameyaita vijisenti kuelekea kukamilika.
Taarifa zilishaeleza kuwa Chenge anachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa kubwa ya nchini Uingereza, SFO ili kujua kama mapesa zaidi ya Sh. Bilioni Moja aliyokutwa nayo katika akaunti yake iliyoko kwenye kisiwa cha Jersey nchini Uingereza yana uhusiano na manunuzi tata ya rada yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kampuni ya BAE System, wakati huo, yeye (Chenge) akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, imeelezwa kuwa uchunguzi huo unaofanywa na SFO unatarajiwa kukamilika wiki hii na hivyo Waziri huyo aliyeachia ngazi kutokana na sakata hilo, huenda kipindi hiki kikawa kigumu kwake.
``Bila shaka atakuwa na wakati mgumu... hii ni kwa sababu maelezo yake katika uchunguzi huu yakionyesha kuwepo na shaka ya fedha hizo, anaweza kuonekana kuwa naye ni mtuhumiwa na hivyo akaingia matatani,`` kikasema chanzo kimoja.
``Na hata akionekana kuwa hahusiki na tuhuma za kupokea mapesa yatokanayo na ununuzi wa rada, bado atakuwa na wakati mgumu katika kuwafafanulia wanaohoji namna alivyopata mapesa hayo anayoyaita vijisenti,`` kikaongeza chanzo hicho.
Taarifa nyingine zinaeleza kuwa Chenge amekwenda nchini Uingereza na kukabiliana na watu hao wa SFO, ambao ndio walioanika habari kuwa Chenge ana akaunti yenye zaidi ya Sh. Bilioni Moja katika benki moja iliyoko katika kisiwa cha Jersey, Uingereza.
Chanzo chetu kimeiambia Alasiri leo asubuhi kuwa wakati muda wa uchunguzi wa tuhuma hizo ukielekea ukingoni, Bw. Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, alishakwea pipa kuelekea Uingereza.
Chanzo hicho kikasema kuwa Bw.Chenge anatarajiwa kuwa nchini Uingereza kwa siku tatu, ambapo atakuwa na mahojiano ya mwisho mwisho na makachero wa SFO kabla ya kazi hiyo ya kumchunguza kukamilika.
Hata hivyo, Bw. Chenge mwenyewe jana alikaririwa na vyombo vya habari akikiri kuwa atasafiri kwenda Uingereza, lakini akadai kuwa safari yake hiyo ni ya kawaida na kamwe haihusiani na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Awali, Bw. Chenge alipohojiwa na gazeti moja la Uingereza, alikiri kumiliki akaunti na fedha hizo, lakini akapinga vikali kuwa fedha hizo hazitokani na rushwa bali amezipata kwa njia ya halali.
|