|
`Tatizo la Wazanzibari ni kutoaminiana`
2008-05-17 15:45:19
Na Haji Mbaruku, Jijini
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Makete, Dk. Hassy Kitine amesema kuwa matatizo ya kisiasa visiwani Zanzibar yanasababishwa na hali ya kutoaminiana baina ya vyama viwili vikuu vya CCM na CUF.
Dk. Kitine ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya awamu ya tatu, amesema kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, nao umetonesha vidonda visiwani humo.
Dk. Kitine alikuwa akitoa maoni yake katika mahojiano ya kipindi kilichokuwa kikirushwa na kituo kimoja cha luninga Jijini.
Alikuwa akielezea kuendelea kuwepo kwa mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo ya muafaka baina ya CCM na CUF.
Kuvunjika kwa mazungumzo hayo kumesababisha malumbano makali toka kwa wajumbe wa kamati zote mbili za muafaka za vyama hivyo na kufikia hatua ya kumwagiana mchele hadharani huku kila chama kikidai kuwa mwenzake ndiye anayekwamisha mazungumzo hayo.
CCM inadai kuwa kimsingi, azimio la Butiama lilikuwa na mapendekezo ya kamati ya muafaka, lakini ikataka wananchi wenyewe washirikishwe kuhusiana na Serikali ya mseto visiwani humo.
Uamuzi huo unapingwa vikali na CUF kwa maelezo kuwa kura za maoni hazikuwepo kwenye ajenda ya mazungumzo hayo na badala yake, hoja hiyo inalenga kuchelewesha kuwepo kwa serikali ya mseto.
Tangu hapo, malumbano baina ya vyama hivyo yameendelea kila kukicha.
Hata hivyo, Dk. Kitine amesema kuwa mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar utaweza kupata ufumbuzi pale wazanzibar watakapokaa chini na kuanza kuaminiana.
Anasema kuwa, hisia zinazoendelea kuwepo visiwani humo kuwa wapemba sio waswahili ndizo zinazosababisha matatizo ya kisiasa visiwani humo.
Kuna hisia kuwa wapemba wanadai kuwa wao sio waswahili.
Hata wangazija nao wanadai hivyo hivyo, sasa matatizo kama haya ndiyo yanayosababisha hali ya kutoaminiana, akasema.
|