|
Malori `vimeo` Dar yapigwa stop
2008-05-17 15:46:41
Na Moshi Lusonzo, Jijini
Polisi Jijini wameyanasa malori 35 mabovu na yaliyo katika hali mbaya huku wakiyafutia leseni mawili baada ya kubainika kuwa yenyewe hayafai tena kutembea barabarani.
Akizungumza na Alasiri wakati akiwa katika eneo la Chang\'ombe, Mkuu wa operesheni hiyo kutoka makao makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarni, Inspekta Abel Swai, amesema magari yaliyokamatwa yameonekana kutokuwa na breki na matairi yake hayana kiwango cha kutembea barabarani.
Inspekta Swai akasema hivi sasa, zoezi hilo linaendeshwa katika kanda ya Temeke na tena ni maalum kwa magari aina ya malori ambayo yanafanya kazi ya kubeba mizigo kutoka bandarini.
Akasema, katika msako huo, jumla ya magari 33 yamesimamishwa kuendelea na shughuli zake baada ya kugundulika kuwa na hitilafu zinazoweza kurekebishwa, huku malori mawili yameondolewa kabisa kutembea barabarani kutokana na ukweli kuwa yako katika hali mbaya kiasi cha kutoweza kurekebishika.
``Tumewaeleza wamiliki na madereva wa malori hayo kwenda kuyarekebisha ili yaruhusiwe kutembea tena... na hili litafanyika kama magari hayo yatakaguliwa tena na kuthibitika kuwa yapo salama,`` akasema Inspekta Swai.
Kwa mujibu wa Inspekta Swai, magari ya aina hiyo yamekuwa chanzo kikubwa cha ajali zinazotokea hapa nchini, kutokana na mengi kati yao kuendeshwa yakiwa hayana matairi yanayofaa na hata breki.
Hata hivyo, aakaeleza wamiliki wa magari hayo licha ya kutakiwa kifanya ukarabati, pia wamepewa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 20,000 kwa kila kosa.
Amewataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kuyabaini magari ya aina hiyo na kuripoti kwa ili hatua kali ichukuliwe dhidi yao.
|