|
Trafiki Dar atekwa
2008-05-17 15:47:33
Na Futuna Seleman,Temeke
Katika hali ya kushangaza, askari wa usalama barabarani wa Jijini Dar es Salaam almaarufu kama trafiki, ametekwa nyara.
Askari huyo wa kike inadaiwa alitekwa Mei 9 mwaka huu majira ya saa 9:30 alasiri katika maeneo ya Tandika Jijini.
Imedaiwa kuwa watekaji walimdaka askari huyo mwenye namba WP 5866 Jamila, kumpakia kwenye gari bila ridhaa yake na kisha kwenda naye mahali asikokujua.
Hata hivyo wanaotuhumiwa kuzua balaa hilo wamedakwa na inasemekana yumo dereva wa daladala aitwaye Stephano Mongerere, 30, mkazi wa huko huko Tandika.
Dereva huyo tayari amefikishwa kwenye vyombo vya dola ambapo sakata hilo linasikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Temeke na hakimu Masaid Mnzava.
Hata hivyo mshtakiwa aliposomewa shitaka lake na mwendesha mashitaka, Alice Mtonga amekana na kurudishwa rumande hadi Mei 21, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Katika kesi nyingine mahakamnani hapo vijana tisa wakazi wa maeneo tofuati kata ya Mbagala, wamefikishwa mahakamani hapo kujibu tuhuma za kumuingilia kimwili msichana kwa kupokezana.
Inspekta Mtonga amewataja washtakiwa hao kuwa ni Doglas Thomas, 19, Shaban Ramadhan, 20, Salum Milumba, 33, Idrisa Hamis, 19, Mtaka Hamis, 17, Samwel Mdota, 17, Ali Yahaya, 20, Rajabu Bakari, 21, pamoja na Idd Mapatu, 19.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo majira ya saa 6.00 usiku huko Mbagala Kiburugwa.
Ilidaiwa kuwa watu hao baada ya kumbaka msichana huyo walimpiga na kumsababishia maumivu makali mwilini na kisha kumuibia vitu na fedha zote alizokuwa nazo.
Washtakiwa wamekana shtaka lao na kurudishwa rumande hadi Mei 27, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
|