17 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Baada ya soo la kichwa: Miujiza mipya yazuka!
 
2008-05-17 15:51:49
Na Mwandishi Wetu, Jijini

Siku chache tu baada ya kijana Ramadhani Musa wa Jijini kufikishwa kortini na mzazi wake akikabiliwa na lile soo la kukutwa na kichwa cha binadamu, miujiza mingine ya aina yake imeibuka baada ya mtu mwingine kubambwa na utumbo na misuli ya nyama kadhaa zinazodhaniwa kuwa ni za binadamu.

Mtu huyo mwenye miaka 50, ametajwa kuwa ni mganga mmoja maarufu wa kienyeji kule katika Kata ya Ikomelo wilayani Ileje mkoani Mbeya, anayefahamika kwa jina la Amakisye Kayuni.

Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Bw. Suleiman Kova, amethibitisha juu ya kukamatwa kwa mganga huyo na kueleza kuwa hadi sasa, wanamshikilia na uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo unaendelea kufanywa.

Hata hivyo, Kamanda Kova akasema bado hawajawa na uhakika kama nyama hizo ni kweli za binadamu ama la.

``Hivi sasa tuko kwenye mchakato wa kupeleka nyama hizo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuthibitisha kama kweli ni za binadamu ama vinginevyo,`` akasema Kamanda Kova.

Akielezea zaidi, Kamanda Kova akasema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo ni matokeo ya ufanyaji kazi wao wa sasa unaoshirikisha jamii katika kuwalinda wao na mali zao.

Awali, Kamanda Kova alieleza kuwa utumbo na nyama hizo zinazodhaniwa kuwa ni za binadamu, zilikutwa chumbani kwa mganga huyo wakati polisi wakiendesha msako dhidi ya waganga wa jadi wanaofanya kazi zao mkoani humo bila vibali.

Akasema wakiwa katika operesheni hiyo, ndipo wananchi walipowafahamisha juu ya kuwepo kwa mganga huyo.

Akasema askari walipofuatilia, wakamkamata mganga huyo baada ya yeye mwenyewe kukiri kuwa anafanya kazi bila ya kuwa na kibali na zaidi, ndipo wakamkuta na utumbo na misuli ya nyama hizo zinazodhaniwa kuwa ni za binadamu.

Aidha, akaeleza kuwa mtuhumiwa huyo anahusishwa pia na kupotea kwa albino aitwaye Henry Mwakajila, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ukukwe wilayani Rungwe ambaye ametoweka tangu mwezi Februari mwaka huu.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.