|
Simba, Yanga zacheka
2008-08-18 16:56:28
By Somoe Ng\'itu
Kampuni ya bia Tanzania (TBL) jana iliingia mkataba wa kuzidhamini klabu za Simba na Yanga wenye thamani ya bilioni tatu ambapo kila mwaka kuanzia msimu wa Ligi Kuu ya Bara unaotarajiwa kuanza kufanyika Jumamosi kila klabu itapata zaidi ya Sh. milioni 654.
Akitangaza udhamini huo katika sherehe maalumu, Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo, David Minja alisema kuwa TBL imeamua kudhamini timu hizo ili kutoa mchango wa maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.
Minja alisema kuwa kila timu inatarajiwa kupatiwa Sh. milioni 16 kwa ajili ya kulipia mishahara ya kila mwezi ya wachezaji, basi la kusafiria, vifaa vya mazoezi, jezi, fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya ofisi zao na fedha za uendeshaji wa ofisi.
Minja alisema kuwa pia TBL itatoa Sh. milioni 25 kwa timu itakayofanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika msimu ujao wa ligi na ile itakayomaliza ikiwa ya pili itajinyakulia kitita cha Sh. milioni 15.
Aliongeza pia kampuni yake itaendelea kuzitangaza timu hizo ili kuweza kufahamika na kujulikana katika medani ya kimataifa na wameamua kuzichagua klabu hizo kwa sababu wanaamini ndio zinazochangia kuleta hamasa katika mchezo wa soka hapa nchini.
``Najua timu ziko nyingi ila Simba na Yanga ndio msingi na zinawakilisha uhai wamichezo hapa Tanzania ndio maana tumeamua kuzifadhili baada ya kuombwa na TFF (Shirikisho la soka nchini),`` alisema Minja.
Mara baada ya kumaliza kusaini mkataba huo, TBL ilikabidhi viongozi wa klabu hizo hundi zenye thamani ya Sh. milioni 25 ili kuweza kuwasaidia katika maandalizi ya ligi.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa wanaipongeza TBL kwa kukubali kuzidhamini klabu hizo mbili ambapo wanatarajia kuona fedha hizo zinachangia kukuza viwango vya wachezaji walioko katika timu hizo.
Tenga alisema kuwa uongozi wao mzuri ndio uliozaa matunda hayo ambapo mwaka 2005 baada ya kuingia madarakani kampuni hiyo ilisita kutoa fedha zake kutokana na kutoamini kwamba zitatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
``Ili kuenzi udhamini huu ni pamoja na klabu kufuata na kuheshimu kanuni za ligi ambapo fedha hizo ni sawa na kupewa mtaji,`` alisema Tenga.
Aliongeza kuwa bado wanahitaji kuona wadhamini wengine wanapatikana katika soka kwa sababu mchezo huo kuundesha unagharama kubwa.
Naye mgeni rasmi katika sherehe hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu aliyekuwa akimuwakilisha Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alisema kuwa udhamini huo ni changamoto kwa timu hizo kuwa na maendeleo na ndio ujenzi wa timu ya taifa bora.
Viongozi wa Simba waliosaini mkatana huo ni Mwenyekiti, Hassan Dalali na Yanga ni Mwenyekiti, Imani Madega.
|