21 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

BEST:Kuboresha mazingira bora ya biashara
 
2005-07-21 07:40:04
Na Grace Chilongola wa PST

Mfumo wa utoaji na upatikanaji leseni, umekuwa na vikwazo vingi, hata kuwakatisha tamaa baadhi ya watu na kuamua kufanya biashara bila ya leseni au kutumia njia za mkato.

Programu ya uimarishaji na uboreshaji wa mazingira bora ya biashara (BEST) inakusudia kuleta mageuzi katika kuhakikisha kuwa, kanuni na sheria zilizopo zinaboreshwa ili kusaidia sekta binafsi, katika maeneo yanayohusu utoaji wa leseni za biashara, taratibu za ardhi na mageuzi katika sheria za ajira.

Mpango huo, ulianzishwa na serikali kwa lengo la kupunguza umaskani, ambapo utekelezaji wake ulianza Januari, mwaka huu, baada ya kuanzishwa kwa kitengo kijulikanacho Better Regulation Unit (BRU) katika ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Afisa Mtendaji Mkuu wa programu ya BEST, Dk. Stergomena Tax’Bamwenda, anasema kuwa serikali imedhamiria kuunga mkono ukuaji wa sekta binafsi kwa kuhakikisha kuwa, mazingira endelevu ya kibiashara yanaboreshwa.

Kimsingi, serikali ya Tanzania inatambua kuwa maendeleo endelevu ya uchumi wa kijamii na utokomeshwaji wa umaskini, vinaweza kufikiwa mapema kutokana na ukuaji wa haraka wa uchumi. Kwa sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 6.7.

Programu hiyo ya miaka mitano inayoendeshwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ambao ni serikali za Denmark, Sweden, Uingereza na Uholanzi imeamua kutekeleza ili kupunguza gharama za kiutawala na usimamizi, katika kufanya biashara nchini na kuboresha utoaji wa huduma za kiserikali na kisheria kwenye sekta binafsi kwa kutumia muingiliano wa malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza wakati wa maonyesho ya 29 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) Bw Tax’Bamwenda anasema kuwa, madhumuni ya programu ya BEST ni kuimarisha ujasiriamali na ushindani, kwa kuboresha mifumo ya sheria na kanuni, ili kupunguza gharama za uendeshaji biashara na kuboresha huduma zitolewazo na serikali kwa sekta binafsi.

Kwa kufanya hivyo anasema kuwa, sekta binafsi itakua na kufanya kazi, katika mazingira bora na hivyo kuchangia kupunguza umaskini.

Uandaaji wa sheria ya kusajili biashara unaofanywa na programu hiyo, utachangia kubadili mfumo mzima wa leseni kutoka chanzo cha mapato ya serikali na kuwa chombo cha kusajili biashara.

Hali hiyo inasemwa kuwa, itarahisisha usajili wa biashara na kuwavutia watu wengi zaidi wasajili na kurasimisha biashara zao.

Akizungumzia utoaji wa leseni za biashara Bw Tax’Bamwenda anasema kuwa, serikali ipo mbioni kuanzisha mifumo miwili huru yenye malengo sawa,ya usajili wa shughuli za biashara na kupunguza au kuondoa kabisa gharama zisizo za lazima.

Halikadhalika mfumo wa kanuni za utoaji wa leseni unaohakikisha ufanisi na usimamizi kwa gharama nafuu.

Mihimili itakayowezesha mageuzi katika uimarishaji na uboreshaji wa mazingira bora ya biashara, ni pamoja na upatikanaji wa kanuni bora, ambazo zinalenga kuondoa kanuni zisizo za lazima, na kuhakikisha utekelezaji mzuri unaolenga hasa kwenye biashara ndogondogo na za kati.

Pia kuharakisha na kuboresha utatuzi wa migogoro ya kibiashara, ili kuharakisha ufanisi katika ushughulikiaji wa migogoro ya kibiashara hususani biashara ndogondogo na za kati.

Mpango , kuimarisha kituo cha uwekezaji Tanzania kwa kusaidia kuwaonyesha kasoro na matatizo yaliyopo katika uwekezaji nchini.

Anasema mihimili mingine ni kuzipa uwezo na sauti sekta binafsi, ambazo nazo zitawajibika kuunda na kusimamia mfuko maalum.

Mfuko huo, unalenga kuboresha uwezo wa wadau wa sekta binafsi, katika kugundua na kubainisha matatizo ya kanuni zilizopo ili kutoa suluhisho la kuweza kujenga mazingira bora ya biashara na kubadili utamaduni wa serikali, ili ulenge kwenye kuboresha utoaji huduma za serikali kwa sekta binafsi.

Kimsingi,Kwa kuwa lengo ni mazingira bora ya biashara na kupunguza umaskini, kazi ya kurekebisha sheria za ardhi zilizopo inaendelea ili kuleta mabadiliko kwenye vifungu mbalimbali vinavyohusu rehani.

Lengo la mabadiliko hayo, anasema kuwa ni hatimaye kuwezesha ukopaji mitaji ya biashara kuwa rahisi zaidi.

Akielezea jinsi wafanyabiashara ndogondogo na wa kati watakavyonufaika na programu ya BEST, Bw Tax’Bamwenda anasema, kwa sababu sheria wanazozishughulikia zinahusu wafanyabiashara hao, zitasaidia kuondoa urasimu unaofanyika kwenye utapatikanaji wa leseni za biashara.

Wafanyabiashara ambao mapato yao ni chini ya sh mil. 20 kwa mwaka, watatakiwa kusajili mara moja tu biashara yao, hivyo kutopata usumbufu kama ule wa kubadili leseni kila mwaka, zinapomaliza muda na kwamba hata usumbufu wa kukamatwa kwa mali zao wanaposhindwa kulipia leseni hautakuwepo.

Uanzishwaji wa BEST anasema kuwa, utawawezesha wafanyabiashara na wananchi, kusajili biashara zao huko walipo mikoani, badala ya kuja makao makuu ya BRELA Dar es Salaam.

” Hakutakuwa na ulazima wa kuja mjini hivyo kupunguza gharama za usafiri, muda, ufuatiliaji na malazi.” Alisema.

Kuhusu mafunzo kuhusu BEST, yataanza kutolewa nchi nzima, mara baada ya sheria leseni kurekebishwa na kupitishwa na bunge, kwa lengo la kuwaelimisha wananchi na wafanyabiashara juu ya usajili wa leseni.

Kwa upande wa mageuzi ya sheria za kazi, anasema baadhi zimepitwa na wakati, kwani hazijitoshelezi na zimeshindwa kutoa huduma za ajira katika sekta binafsi, na kwamba hazioani na mahitaji ya soko la kazi na vigezo vya kimataifa.

Baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo na wa kati watakaonufaika na programu hiyo, ni pamoja na wafanyabiashara wa samaki, uchongaji wa vinyago na wengine wengi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.