22 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wamasai wasikubali kudhalilisha utu wao kwa watalii
 
2005-07-22 08:07:34
Na Namsembaeli Mduma

Ni hivi karibuni, nilitembelea vijiji mbalimbali katika tarafa za Sale na Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Nilijionea mambo mbalimbali ya kuvutia, zikiwamo mbuga na hifadhi za wanyama pori.

Pia, nilijionea jinsi baadhi ya Wamasai waishio katika maeneo hayo, wasivyoweza kuutumia mwanya huo na kujipatia kipato kutoka kwa watalii.

Wanapotakiwa kuonyesha sehemu ya mila zao ama kupigwa picha huwa na misimamo tofauti ya kutoafiki ombi hilo.

Hayo yametokea,pengine kutokana na kutojua umuhimu wa mila zao hizo, pamoja na uasili wao, wanajirahisi kwa watalii hao au ni kwa kukosa kujua kama wanaweza kujikwamua kiuchumi kupitia vitu hivyo ambavyo ni vivutio tosha kwa watalii.

Sikusimuliwa bali nilijionea mwenyewe jinsi watalii wanavyong’ang’ania kutoishia kuangalia wanyama tu na kurudi makwao, bali kutaka kupiga picha au kuwapiga picha Wamasai na kuzipeleka kwao.

Pia, nilishuhudia jinsi watalii kadhaa kutoka Uingereza na Sweden, wakiwataka wamasai walio katika maeneo ya Waso na mengine yaliyo nje ya hifadhi ya Ngorongoro wawaonyeshe michezo yao ya asili mfano kuruka juu kwa malipo kidogo sana.

Haikuniingia akilini na nilizidi kujiuliza kuwa, Wamasai wanakubaliana na matakwa ya watalii hao kwa malipo ya dola moja(USD 1) kwa watu watatu au wawili na kwa kubahatisha mmoja, kwa kutojua thamani ya michezo na nguvu wanazozitumia kucheza au ni kwa kukosa namna au jinsi nyingine ya kujipatia kipato.

Kama sababu ya mwisho ni sahihi, basi itakuwa kwamba Wamasasi hao wanajirahisi hivyo, kwa kukosa la kufanya.

Pengine hawajui pia kama kuna umuhimu wa picha hizo kwa watalii hao, licha ya ukweli kuwa wapo wanaokwenda kuziuza na wengine kupamba katika majengo na sehemu zao za biashara.

Binafsi nilidhani kuwa, thamani ya sura za Wamasai hao zinazopigwa picha wakati wakicheza ngoma, kuruka au wakiwa katika staili mbalimbali , ni kama ile ya wanaotumika katika matangazo mbalimbali.

Kama hivyo ndiyo, ningedhani ingekuwa vema endapo kungewekwa utaratibu wa kiasi kitakachotozwa kwa watalii hao, ili kupata picha hizo kwa Mmasai yeyote yule au vikundi watakavyovihitaji kupata picha zao hizo, mahali popote pale, hata kama ni majumbani.

Hiyo ni katika kuhakikisha kuwa, Wamasai hao wanapata chochote, hata kama ni nje ya maboma yao ya asili .

Maboma haya yanajulikana kwa kuendesha shughuli hizo maalum kwa watalii, kwa malipo.

Unaweza ukajiuliza ni kwa nini watalii wanawafuata wamasai nje ya maboma na kuhitaji huduma hizo, niliofanikiwa kuzungumza nao walidiriki kuweka wazi kuwa ni kwa sababu huko wanakowafuata (nje ya maboma) wanawalipa fedha kiasi.
Nawanukuu katika tafsiri isiyo rasmi’’

Unajua ni rahisi kupiga picha na Wamasai nje ya boma zao za jadi..ndio maana tunawafuata wanapokuwa nje au nyakati nyingine tunawaalika mahotelini au maeneo tunayoishi kwa muda na kupiga nao picha’’.

Kwa hali ya maisha ya maeneo kama Waso mjini Loliondo, dola moja haikidhi hitaji la maana hata moja, kwa kuwa ni kiasi kidogo na kila kitu katika maeneo hayo ni aghali.

Sababu zinaeleweka kuwa ni ukame na ukosefu wa eneo la kutosha kwa kilimo.

Kwa kulitambua hilo, Wamasai walipaswa kuwa na viwango maalum vya kuwatoza watalii hao, pindi wanapohitaji picha zao au kuona ngoma zao ili wawe na njia mbadala ya kujiingizia kipato.

Ukiwakuta Wamasai katika maeneo yao hayo, utaamini kuwa kweli, kuna watu wanaodumisha na kuzielewa mila zao.

Hao wapo tofauti kabisa na wale tunaowaona mijini kimaadili na hata kiutamaduni (mavazi yanazingatiwa pia).

Hata watalii wa kizungu wenyewe wanakiri kuwa Wamasai hao na mila zao, wamekuwa gumzo katika mitaa yao huko Ulaya na kwamba wanafurahi kuwapata ili wawachezee, au kuwa piga picha kwa fedha kidogo.

Hebu tujiulize, dola moja inatosha nini hata kwa Mmasai mmoja? Na je inavyogawiwa kwa Wamasai wawili au Watatu? Si wanakuwa wamejidhalilisha kwa kujirahisi Ilihali wana matatizo chungu nzima?

Naiomba Wizara ya Maliasili na Utalii ijaribu kuangalia uwezekano wa kuwaanzishia Wamasai wanaoendesha shughuli hizo nje ya maboma ya asili bila mpango mzuri wa bei, mkakati utakaowawezesha kuwa na mfumo mzuri wa bei zitakazotozwa kwa watalii watakaohitaji huduma zao.

Hilo ni moja, pili, Wizara hiyo iangalie uwezekano wa kuwapa Wamasai hao elimu ya kuthamini utu wao na kukataa kujirahisi au kujidhalilisha, kwa kuwavizia watalii wa kizungu mbugani na kuruhusu kupigwa picha hovyo.

Wakati tunakatiza mbuga ya eneo la pori tengefu la Loliondo tulikotoka na wakati tukielekea kwenye hifadhi ya Ngorongoro, nilijionea vituko vya aina yake na kuwauliza wenyeji niliokuwa nao garini maswali mengi.

Nilikuwa nikiwaona Wamasai wakitokeza barabarani kutokea mbugani kwa kunyata na kutimua mbio kurudi kwenye msitu baada ya kugundua kuwa magari waliyokuwa wakiyavizia siyo yenyewe.

Nilielezwa kuwa, walikuwa wakifanya vile wakifikiri ni watalii ambao pengine wangeweza kufanya nao biashara ya picha au kuwaonyesha vituko fulani na kupata hizo dola moja moja.

Nilipenda kujua ni kwa nini walikuwa wakitimua mbio kurudi mbugani na kujibiwa kuwa, ni kwa sababu ya hofu ya kukamatwa na watu wa hifadhi ya Ngorongoro kwa kufanya vitendo hivyo ambavyo kwa njia moja au nyingine vinawadhalilisha.

Ilielezwa kuwa wengi wa wanaojificha porini humo, ni wale wanaokubali kupiga picha hata za utupu na pengine kwa kudhalilishwa zaidi.

Inatia aibu kwa maana nilijionea kwa macho yangu akina mama wa Kimasai wakikimbia kujificha baada ya gari letu kuwakaribia na wawili walidondoka wakati wakitimua mbio hizo.

Sasa, kama kweli Wamasai mko makini na mnapenda kukuza uchumi wenu, basi kubalianeni juu ya kiwango kizuri cha kuwatoza watu hawa na sio kukubali wawaamulie wao.

Kwa kufanya hivyo, watakuwa wakiwalipa chini ya kiasi kinachoendana na hadhi ya mila zenu, ngoma mnazowachezea pamoja na sura zenu wanazokwenda kuziuza, kuzionyesha kwao au hata kuzitengenezea vitabu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.