24 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tamasha la Nchi za majahazi
 
2005-07-24 07:41:14
Na Flora Wingia

Watengenezaji filamu wa Nigeria wamekuwa wakali katika soko lao la sinema kwa kutumia vyema uhakiki wa filamu hizo na pia matumizi ya matamasha kama la Tanzania linaloandaliwa na ZIFF mjini Zanzibar.Beda Msimbe mwandishi aliyekuwa Zanzibar akijifunza zaidi uhakiki wa filamu anaeleza zaidi:

Unapofyatua sinema ya Tumaini kwa ajili ya kuiangalia kitu cha kwanza unachokiona ni mawimbi yanayotamalaki kama kibwagizo kinachosindikiza maelezo ya awali ya sinema, utambulisho.

Mawimbi haya ni ya ziwa Viktoria na unapokuwa huna mtu wa kukueleza kuwa hiki ni kitu gani,madhari ya ufunguzi kwa jinsi inavyovutia unajiweka sawa ili uweze kufaidi si mandhari tu yanayoonekana kuwa bora, bali pia hadithi yenyewe.

Mwalimu anayefundisha chuo kikuu cha Australia cha Murdoch,Martin Mhando aliitumia sinema ya Tumaini iliyotengenezwa Tanzania na Mtanzania kuonyesha maana halisi ya uhakiki wa filamu kwa namna inavyoweza kuwasaidia watazamaji na watengenezaji wenyewe.

Waandishi wa habari wa Tanzania na Afrika Mashariki ambao bado wanapigana kupata kujua miiko ya uhakiki wa filamu na sanaa nyingine za maonyesho walikuwa na mtihani mkubwa wa kuangalia sinema hiyo ambayo pia ilikuwemo katika mashindano, kwenye tamasha la nane la nchi za jahazi.

Waandishi wachache wa Tanzania waliokuwepo katika mafunzo hayo yaliyoendeshwa na taasisi ya maendeleo ya mawasiliano ya kusini mwa Afrika (SACOD) na waandazi wa Tamasha la Nchi za Jahazi, ZIFF, walifahamu baadaye kwamba mwalimu Mhando alikuwa na sababu kubwa ya kuleta picha ya Tumaini kama, filamu kweli, iliyokidhi mahitaji ya kuwa filamu. Picha hii ilitwaa tuzo mbili ya UNICEF na East African Prodiuction taika tamasha la nchi za Jahazi.

Ilikuwa ni filamu inayogusia matatizo ya watoto yatima na haja kubwa ya jamii kuangalia watoto hao katika upeo mkubwa zaidi na wala si huu wa sasa uliojaa unyanyapaa.

Kazi ya uhakiki wa filamu katika upeo wa kimataifa, kwa kuzingatia vionjo vya kawaida, ni kazi ambayo si rahisi, lakini pia ni kazi ambayo kama ikiendelea kufanywa kama inavyofanyika sasa, inaweza kuwa na msukumo zaidi wa kibiashara badala ya kuwa sehemu ya mtengeneza sinema kujiona na pia wananchi kutambua nini hasa kinasubiriwa katika sinema hiyo au sanaa hiyo.

Mratibu wa kongamano hilo Farida Nyamachumbe amesema kwamba nia ya kongamano hilo ni kuhakikisha kwamba waandishi wa habari wanasaidia kukuza sekta ya filamu nchini Tanzania na Afrika Mashariki.

’’Kwa sasa hatuna wahakiki wa filamu na kama tunataka kukuza sekta hii ni lazima kuwa nao’’ alisema Farida katika ukumbi wa Baraza la Habari uliopo barabara ya Kenyatta.

Amesema kwamba waandishi ni msaada mkubwa katika kuwaelekeza watu nini kinafanyika na nini kinastahili kufanyika kutokana na uwezo wao wa ubunifu kwa hiyo kuwapatia kanuni za msingi za uhakiki zitakazowasaidia katika kazi zao ni muhimu.

Kongamano hilo ambalo lilipitia filamu kadha, lilionyesha udhaifu mkubwa wa watengeneza filamu hasa wa Afrika Mashariki ambao wamekuwa wakifikiria kuwa, uhakiki ni lazima uwasaidie kufanya biashara wala si kusaidia kukuza sekta yenyewe.

Wahakiki wa filamu wa Nigeria wamefanikisha sana kukuza sekta ya nyumbani kwao kwa kuwaweka sawa wazalishaji ,waendesha sinema na wasanii wakuu wao(waongozaji) katika kutambua njia ambayo wananchi wanaitaka na jinsi soko lilivyo.

Wahakiki wa Afrika na dunia wa FIPRESCI walikuwepo pia kutoa mada zao juu ya haja ya mawasiliano ili kuzidi kuimarisha uhakiki wa filamu kwa manufaa ya pande zote husika.

Farida akizungumza katika moja ya mdahalo wa kwenye kongamano hilo la kujifunza uhakiki na haki za binadamu,alisema kuwa uhakiki wa sasa umekuwa ukiangalia nafasi ya kuuza zaidi filamu yenyewe badala ya kufanya wajibu wa kuelewa kama kweli sinema hizo zimefanyiwa kazi za kutosha kwa ajili ya manufaa ya jamii na watengenezaji wenyewe.

’’Ukuaji wa sinema unategemea watu zaidi, na kama mwandishi anayehakiki atajua kwamba anafanya nini basi ni dhahiri kwamba ataisaidia jamii na watengenezaji wenyewe namna bora ya kufanikisha mawasiliano’’ alisema mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Murdoch cha Australia, Martin Mhando.

Ukuaji wa sekta ya filamu unatakiwa kwenda sambamba na wahakiki na kwamba watengeneza filamu hawana sababu ya kuwaogopa wahakiki hao. Wahakiki kutoka Federation of Film Critics and Journalists (FIPRESCI)walisisitiza.

Aidha wahakiki hao walionyesha haja ya kuungana kwa wahakiki wa Afrika ili kuweza kufanyakazi yao wanayostahili kusaidia jamii.
Ni biashara au kifo cha sekta.

Uandishi wa kibiashara au kisiasa pekee ulijadiliwa katika kongamano hilo na kwa mara nyingine tena mhadhiri wa chuo kikuu cha Murdoch Australia Dk Martin Mhando alisema unaua maana halisi ya uandishi.

Amesema kwamba kwa kuwa na uandishi unaozingatia maana ya kisiasa au kibiashara, uandishi unapoteza maana yake halisi na kutumika kama bidhaa tu ya kutengeneza faida ya kifedha.
Kuandika kwa namna ya dhamira halisi ya kupasha habari kutaonekana na hivyo kutoa msukumo wa wasomaji na wataalamu kubaini mambo yanayostahili kufanyiwa kazi.

Matatizo halisi ya katika vyumba vya habari, matatizo ambayo yanachangia kuwa na mweleko usiokuwa mzuri wa habari yametakiwa kufanyiwa kazi na hasa kwa wahariri kutambua kwamba kukosekana kwa mwenge (uhakiki) habari huenda zikawa ni zajuu juu tu na wala haziwezi kuleta msingi unotarajiwa katika ukuzaji wa sanaa na utamaduni wa kitaifa.

Amesema stori inayoandikwa kwa mtiririko wa promosheni inapoteza kwa kiwango kikubwa ubinadamu na kuacha maswali yasiyoweza kujibika kirahisi au kufanyiwa kazi inayostahili.

’’Waandishi wanakuwa na haraka mno na kujipanga ukavukavu, lakini wakitulia wataandika ukweli kwa kuchagua kile cha heshima na kuelimisha namna ya kujenga’’ alisema mmoja wa walimu kutoka Kenya, Ogova.

Ya kujifunza
Katika kongamano la uhakiki pia suala la kuangalia miingiliano ya muziki, upigaji picha na uwezo wa muongozaji kama msanii mkuu pia liliangaliwa.

Onyo kubwa lilikuwepo la watu wanaohamisha michezo ya jukwaani na kugeuza sinema, kwa kutozingatia ukweli kuwa sanaa ya jukwaani si sanaa ya sinema, sinema ina adabu yake.

Aidha wahakiki wanafunzi katika baadhi ya sinema walizotakiwa kuangalia na kufanyia mazoezi zilibainisha ujuzi mdogo wa watengeneza hadithi za sinema zenyewe.

Sinema za muda mfupi za mafunzo na uhakika wa ukweli wa takwimu zilizokusanywa, hazikuonekana kuwa na tatizo kwa upande wake, lakini bado zina safari ndefu kwa kuwa ukweli wa utengenezaji wake ni wazo la mwandishi jinsi anavyotaka jamii kuelewa anachotaka kuwaeleza.

Msanii mkuu wa Tumaini (muongozaji) Beatrix alisema wazi kuwa bila wahakiki wa filamu sekta ya utengenezaji wa filamu ambayo kwa sasa ndio inaamka usingizini itakuwa na mgogoro mzito zaidi katika ukuaji wake.

Alitaka waandishi wa habari kwa misingi waliyoipata kuhakikisha kwamba wanakosa sinema zilizotengenezwa na zinazotengenezwa mpaka ifike mahali, kazi za kisanii ziweze kumsaidia mtengenezaji mwenyewe.

Bi Beatrix alizungumza hayo muda mfupi tu baada ya kupokea tuzo zake katika ukumbi wa Ngome Kongwe mjini Zanzibar, Tuzo za nchi za jahazi kwa sinema yake ya Tumaini.

Darasa la wahakiki wanafunzi pia lilipata nafasi ya kuzungumza na watengeneza filamu wanaharakati ambao nao waliwapa mawazo yao kwanini wanafaa katika mazingira ya ukuzaji wa sinema.

Watengeneza sinema wa Kenya na Uganda walitoa darasa lilisilorasmi kwa wanahabari waliokusanyika kujifunza kuhakiki kuonyesha ni namna gani mtengeneza sinema anavyotegemea watu wengine kupunguza kama si kuondoa makosa katika utengenezaji Sinema.
Sinema za nchini.

Kimsingi katika darasa ilionekana wazi kwamba sinema zinazotengenezwa nchini nyingi, labda kwa ukosefu wa fedha au utaalamu zimekuwa ni mchezo wa kuigiza unaopigwa picha na kukosa hadhi inayotakiwa kama sinema.

Kama wahakiki wakitumia kanuni zao zote za ufanyajai wa uhakiki, kuna kipindi kirefu cha ukimya katika utengenezaji wa filamu, vinginevyo , filamu zinazostahili kuitwa filamu ni chache zaidi nyingi zikiwa ni michezo ya kuigiza.

Aidha daawa njema ni kwa taasisi husika kuanza kutoa elimu ya utengenezaji wa filamu na si suala la kuendelea kuachia watu wajifunze kutokana na dunia, kwani hilo litafanya watengeneza sinema wa Tanzania kubaki katika shimo bila kuwa na ngazi za kukwea kutoka nje.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.