25 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

DK EMMANUEL KANDUSI: Bunge la sasa lahitaji watu walioelimika
 
2005-07-25 07:09:24
Na JACKSON KALINDIMYA

Wakati joto la uchaguzi mkuu linazidi kupanda, wananchi wametakiwa kuwa makini kuchagua wawakilishi walioelimika wanaoweza kuchambua masuala mbalimbali ya zama hizi na kutumia fursa zilizopo kushirikishana kukuza uchumi na kupiga vita umaskini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kukuza Haki za Binadamu, Dodoma (CHRP) na mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya Southern Africa Human Rights NGO Network,DK EMMANUEL JOB KANDUSI.

SWALI: Mwaka huu, wasomi au watu wenye taaluma za ngazi na viwango mbalimbalii wameamua kujitosa kugombea ubunge na nafasi nyingine za uwakilishi. Nini hasa sababu ya uamuzi huo?

JIBU: Tanzania tuliyonayo sasa imebadilika sana. Masuala mbalimbali yanatakiwa kutazamwa kwa mtazamo mpana wa kina, na wa mbali.

Kuna mambo mengi ya kitaalamu yanahitaji mtu mwenye taaluma au watu walioelimika kuyachambua ndani ya bunge, nje ya bunge, nchini na kimataifa.

Mtu ambaye hajaelimika ni kazi nzito sana kwake kwenda sambamba na mazingira ya sasa ya kuchambua na kutafsiri utekelezaji kwa wananchi wake, hata kunufaika kikamilifu na uwakilishi wake.

Kwa hakika, majimbo yatakayochagua watu wasioelimika yatapata hasara sana.

Siasa za zamani za maneno mengi ya porojo hata kutoa ahadi zisizotekelezeka hazina nafasi tena.

Watu hao hawataweza kuchambua mambo mbalimbali, kuwawakilisha kikamilifu na kutafsiri mambo yaliyoandaliwa kisomi, ikizingatiwa kuwa dunia sasa ni kama kijiji kimoja kikubwa.

Watu wanabadilishana taarifa,ujuzi na kuwasiliana kwa haya na yale, ikiwa pamoja na kuchukua tahadhari katika mchakato huo pale inapostahili.

Wabunge au wawakilishi walioelimika, katika zama hizi wanaweza kuitumikia na kutoa mchango mkubwa kwa nchi na watu wake.

Rais Benjamin Mkapa, amefanikiwa kuliongoza taifa kwa ufanisi, kwa sababu anazungumza na kuchambua mambo kisomi.

Aina hiyo ya uongozi na mafanikio yaliyopatikana katika awamu hii, yamewavutia wasomi wengi kwa kuamini kuwa, sasa wana nafasi ya kutoa mchango wao muhimu kwa manufaa ya watu na maendeleo ya nchi.

Wanaamini kuwa bunge la aina hiyo wanaweza kufanya nalo kazi na likaleta mapinduzi kwa maendeleo ya watu wao.

Mikakati mbalimbali kama vile MKUKUTA, uchambuzi wa bajeti inayoandaliwa kitaalamu na miswada mingine inayojadiliwa bungeni, inahitaji watu walioelimika kuweza kuielewa, kuitafsiri na kuitekeleza kwa kuishirikisha jamii.

SWALI: Hoja kubwa ya zama hizi ni Mkakati wa kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) 2005 – 2010.

Unazungumziaje kuhusu utekelezaji wake?
JIBU: Dunia nzima hivi sasa, hoja kubwa inayokabiliwa ni suala la kutokomeza umaskini.

Nchini mwetu, tulikuwa na Mkakati wa Kupunguza Umaskini 2000 – 2003 na mwaka jana tathmini ya mafanikio ilifanywa.

Hivi sasa tumeingia katika awamu ya Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA 2005 – 2010).

Mkakati huu unaendana na Mkakati wa Kimataifa unaojulikana kama Malengo ya Milenia.

MKUKUTA utakuwa ndio msingi wa shughuli zote zikazofanyika nchini mwetu katika sekta zote.

Changamoto nyingi zinaukabili MKUKUTA. Kuna changamoto ya masuala ya umaskini na kipato.

Umaskini huu wa pili unajumuisha huduma za afya, uhai na lishe, UKIMWI, maji na afya ya mazingira, unyonge wa makundi ya watu wasiojiweza.

Dodoma Mjini tunahitaji kujiletea maendeleo yetu sisi wenyewe, ni lazima tuwe makini na kucheza ngoma hii ya MKUKUTA na mikakati mingine ya kimataifa kama Malengo ya Milenia.

Mbunge wa Dodoma Mjini ni lazima awe mtu mwenye uelewa mkubwa juu ya fursa hizi .

SWALI: Ukiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kukuza Haki za Binadamu, Dodoma (CHRP).Je kituo kimefanya au kinafanya nini katika kuihamasisha jamii kuhusu uchaguzi mkuu ujao?
JIBU: Tunaielimisha jamii kwa njia ya filamu.

Mojawapo ya filamu hizo ni iitwayo Masahibu ya Boboa. Hii inatoa elimu ya uraia na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Haki ya mtu kujiandikisha, kupiga kura, vita dhidi ya rushwa, upendeleo, jinsi ya kupata wagombea wazuri ambao baadhi yao, hasa akina mama, hawajitokezi kugombea hadi washawishiwe au kushauriwa kuwa wanaweza.

Filamu hii tayari imeonyeshwa kwenye vijiji zaidi ya 100 katika mikoa ya Pwani na Morogoro.

Wananchi wakifahamu haki zao na kuzitumia kikamilifu wanaweza kupata viongozi wanaowapata kwa njia ya kidemokrasia.

SWALI: Kituo cha Kukuza Haki za Binadamu Dodoma (CHRP) kipo Dodoma.

Je kituo chenu kimefanya nini cha kujivunia kwa ajili ya kukuza haki za binadamu, maendeleo na mabadiliko ya tabia kwa watu wa Dodoma?

JIBU: Kituo chetu kimekuwa kikiandaa filamu na kuzitumia kuifikisha ujumbe jamii kwa njia ya ushirikishaji wa kuleta mabadiliko ya tabia.

Kuna filamu iitwayo Sona. Inachambua mila potofu ya ukeketaji. Filamu hii, imeonyeshwa katika vijiji vipatavyo 500 na vitongoji vyote vya mkoa wa Dodoma.

Lengo ni kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya mila hiyo na nini cha kufanya katika dunia ya sasa inayohitaji maendeleo huku haki za binadamu zikizingatiwa.

Mradi huo ulianza kutekelezwa toka mwaka 2002 hadi Juni 29, mwaka huu.

SWALI: Je kuna mafanikio yoyote yamefikiwa au kupatikana katika mradi huo?

JIBU: Wananchi wameupokea vyema mradi huo. Baada ya kuelimika na kutambua ubaya wa mila hiyo, watu wameanza kuzomea ukeketaji hadharani.

Mangariba wameanza kubwaga manyanga na kutafuta njia nyingine za kuishi.

Baadhi ya watu wamepelekwa mahakamani huko Kongwa, watoto wa kike wamekuwa wakisema hapana kwa ukeketaji.

Na vijana wa kiume wamekuwa na misimamo kuwa, hawaoi wasichana waliokeketwa.
Kwa ujumla, wengi wanasema kuwa wanahitaji sheria mpya inayopiga vita ukeketaji.

SWALI: Wananchi wa Dodoma,ikiwemo Dodoma Mjini, wanahitaji mikakati thabiti ili kutumia fursa zilizopo kupiga hatua za uhakika kujiletea maendeleo kwa kasi mpya.

Je mbunge atakayechaguliwa anatakiwa kutoa kipaumbele kwa fursa zipi?

JIBU:Mwaka 1973, iliamuliwa makao makuu ya Serikali yahamie Dodoma na Mamlaka ya Ustawishaji Makuu(CDA) iliundwa.

Kama mamlaka hiyo ingekuwa inashinikiza kutoa mapendekezo endelevu ya ujenzi wa makao makuu, Dodoma leo hii ingekuwa wapi?.

Ujenzi wa makao makuu ni fursa inayohitajika kupewa msukumo mpya sasa, kwa kutumia fikra mpya kwa Dodoma mpya.

Ufanisi wa zoezi hili utatafsirika neema kwa Dodoma Mjini.

Dodoma mjini ni makutano ya barabara zote muhimu-The Great North South Road inapita Dodoma.

Barabara zote au nyingi zimo au zinaelekea kuwa za kiwango cha lami.

Dodoma panatakiwa kufanyiwa kazi ya ziada katika barabara, mazao,mifugo na mengineyo ambayo yakipewa kipaumbele kwa fikra mpya kwa Dodoma mjini mpya, kuna uwezekano wa kupata mafuta ya kulisha nchi nzima na kuboresha maisha ya watu.

Dodoma ina mifugo mingi inayohitaji kupewa msukumo mpya ,yanaweza kutokea mapinduzi makubwa katika ufugaji na biashara.

SWALI:Je nini matokeo ya kutumia fursa hizo kwa wananchi wa Dodoma?

JIBU:Kutatokea mabadiliko na kasi mpya ya maendeleo na kutekeleza MKUKUTA kwa vitendo.

Dodoma tuna mandhari nzuri za kuukuza utalii huo kwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii ambavyo vitavutia watu wengi.

Majengo yatajengwa, watu wataongezeka, mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa.

Sekta binafsi itapanuka, ajira itapatikana,
umaskini wa kipato utapungua na huduma za kijamii zitaboreshwa na watu kumudu kulipa kodi ili kuchangia maendeleo yao.

SWALI: Mafanikio ya uhakika siku zote huletwa na watu. Ukiwa Daktari wa Falsafa na Teolojia, mwenye uzoefu wa ndani na nje ya nchi, Je unawaambia nini watu wa Dodoma, hasa Dodoma Mjini?

JIBU: Wananchi wa Dodoma na Dodoma Mjini wanatakiwa kuwa makini na kujua fika maendeleo huletwa na watu. Dodoma tuna bahati ya kuwa na fursa kibao.

Tunaishi katika wakati mzuri ambapo tuna siasa safi na uongozi madhubuti wa Chama Cha Mapinduzi.

Nafasi ya kuchagua viongozi na hususani mbunge wetu iwe ni kwa lengo la kupata mtu mwenye fikra na upeo mkubwa wa hapa nyumbani, lakini pia kwenye anga za kimataifa.

Mtu ambaye ana ’fikra mpya kwa Dodoma Mjini Mpya’ na ambaye atapiga vita rushwa na kuwa tayari kuwajibika na kuwajibishwa.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.