26 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

TLA yashauri maktaba ziwezeshwe kutimiza wajibu wao
 
2005-07-26 08:31:54
Na Raymond Kaminyonge

Uhaba hata kukosekana kwa maktaba katika baadhi ya vijiji na wilaya, kunachangia kushusha ari ya watu kupenda kujisomea, Katika makala hii, Mwandishi Raymond Kaminyonge anazungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Wakutubi Nchini (TLA) Dk.Alli Mcharazo akuhusu namna Wakutubi wanavyotakiwa kubuni njia za kuwezesha uboreshaji na uanzishaji maktaba zao na kuihamasisha jamii kujenga utamaduni wa kupenda kujisomea.

Baadhi ya Watanzania wamekuwa na mazoea ya kuhifadhi fedha za kuzipachika katika kurasa za vitabu, kama njia ya kuzifanya ziwe salama.

Imani hiyo imejengeka kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu hata kama vinapatikana.Hali hii hufanya kitabu kuweza kukaa kwa muda mrefu hata miaka bila kuguswa, na kusababisha fedha kuwa salama.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakutubi nchini, Dk Ali Mcharazo anasema kwa baadhi ya watu hiyo siyo sababu. Hawajengi mazoea ya kusoma kwa kuwa hawana vitabu vya kusoma.

Ukweli uko bayana kuwa, zipo wilaya na baadhi ya mikoa ambayo haina maktaba. Watu wanapenda kusoma lakini hawana vitabu.

Kwa mujibu wa Dk Mcharazo,wilaya pekee zenye maktaba hapa nchini ni tisa tu ambazo ni Njombe, Pangani, Tunduru, Bagamoyo, Biharamulo,Kilosa, Kwimba, Lushoto, Makete na Mbozi.
Mikoa ambayo haina maktaba za mikoa ni Singida, Pwani na Manyara.

Katika mazingira hayo, Dk.Mcharazo anasema Serikali itoe kipaumbele kwa fani ya maktaba, maana elimu bora hutegemea upatikanaji wa vifaa vya kujisomea ikiwa ni pamoja na matumizi ya maktaba
Aidha anasema, kuna umuhimu wa kutengenezwa kwa sera ya maktaba hapa nchini, Bodi ya maktaba ipewe nguvu zaidi ili iweze kusimamia ipasavyo shughuli za maktaba nchini.

Anasema hakuna maktaba inayoweza kukidhi mahitaji yote ya watumiaji wake, hivyo ni vyema maktaba zikajenga ushirikiano na kutengeneza taratibu zitakazowawezesha kutumia taarifa na habari zipatikanazo kwenye maktaba mbali mbali za hapa nchini.

Kwa matazamo wake, Wakutubi na wafanyakazi wa maktaba ni lazima waonyeshe tofauti ya kuwepo kwao na kutokuwepo kwao kwenye taasisi, idara na mshirika mama wanayofanyia kazi.

Anasema ni lazima wafanyakzi wengine waone kuwa, utendaji wao wa kazi unasaidiwa pia na kuweko kwa mkutubi na maktaba.

Mwenyekiti huyo anasema iwapo hilo hawataliona, basi ajira ya mkutubi na fani kwa ujumla itakuwa mashakani hapa Tanzania.

’’Ni vyema basi wakutubi wakawa wabunifu na wawe tayari kubadilika kutokana na wakati, ili kuleta mambo mapya yatakayonufaisha taasisi wanazofanyia kazi na watumiaji wao.’’Anasema na kuongeza ’’Matumizi ya nyenzo mpya kama zile zinazohusiana na teknolojia ya habari kama kompyuta ni muhimu kuwepo,’’

Kuhusu wakati tulionao sasa ambapo ruzuku toka serikalini ni ndogo, Dk Mcharazo anasema kuwa ni muhimu sana wakutubi wajifunze jinsi ya kujitafutia fedha na uwezo mwingine ili kusaidia bajeti zao ambazo ni ndogo.
Anasema kuwa mkutubi katika karne hii, ni jambo la fahari na wito, kwa kuwa matokeo ya kazi zao humwezesha binadamu kuchukua maamuzi muhimu na kuleta mabadiliko ya kifikra na mengineyo.

Katika zama hizi za utandawazi,Dk Mcharazo anasema majukumu ya mkutubi ni mazito zaidi kwa kuwa taarifa ni moja ya mhimili wa utandawazi, hivyo mkutubi sasa ana majukumu yanayofanana
Umasikini ni moja ya sababu kushusha ari ya kujisomea kutokana na watu kutoa kipaumbele kwenye shughuli za kujitafutia riziki badala ya kujisomea.

Aidha anasema sababu nyingine ni uhaba wa maktaba kule vijijini ambako watanzania wengi wanaishi, pamoja na baadhi ya wilaya.

Aidha uhaba wa vitabu katika maktaba zetu hasa vile vya Kiswahili na vinginevyo, ambao pia unasababishwa na maendeleo duni ya fani ya uchapishaji hapa Tanzania ni sababu nyingine zinazoshusha ari ya kujisomea.

Akizungumzia mafanikio anasema, chama chao kimeweza kusimama kwa muda mrefu kama chombo pekee kinachowaunganisha wakutubi wa Tanzania bila kujali wapi wanafanya kazi na viwango vya elimu yao.

Anasema hakuna tena matabaka ubaguzi miongoni mwa wanachama. Ushauri kuhusu mambo ya maktaba pia umekuwa ukitolewa na chama kwa wafanyakazi walio katika fani ya maktaba na maktaba pia.

Kama hiyo haitoshi,Chama pia kimeweza kutoa elimu kwa wafanyakazi wa maktaba wa ngazi mbalimbali kwa kutumia warsha, semina, makongamano, na mikutano mingine.

TLA pia kimefanikiwa sana katika kuhamasisha wakutubi na maktaba zao kwenda na wakati, na kutumia teknologia ya habari katika utendaji wao wa kazi.

Kwa kiasi kikubwa, chama pia kimefanikiwa kujenga mahusiano mema na endelevu na taasisi na mashirika kadhaa ndani na nje ya nchi, na hivyo, wakati mwingine, kufanya kazi kwa pamoja na taasisi na mashirika hayo.

Hii inaashria kuwa TLA imefanikiwa katika kuifanya jamii kutambua umuhimu wa maktaba na mkutubi.
Akizungumzia matatizo, Mkutubi huyo anasema kuwa, kinaongozwa na kuendeshwa na viongozi ambao wanatumia muda wao wa’ziada, yaani baada ya kazi zao za ajira.

Anasema utaratibu huo, kwa wakati huu ambapo chama kinabadilika na kuendelea kwa kasi hausaidii sana maana majukumu yanakuwa ni mengi kuliko muda uliopo.

Chama kinalijua tatizo hilo, na kamati kuu ya TLA inalifanyia kazi, ili baadaye waje kupata watendaji ambao ni waajiriwa wa TLA.

Aidha tatizo jingine ni uwezo mdogo wa chama, ikilinganishwa na matakwa ya wanachama wake pamoja na fani kwa ujumla, na hilo limesababisha chama kuchagua yale machache tu yenye ulazima wa haraka kufanywa.
Moja ya malengo makuu na mikakati ya Chama ni kujijengea uwezo kwa ajili ya manufaa ya chama, wanachama na fani ya ukutubi.

Kuhusu mipango ya baadaye alisema, Chama hicho ili kiende na wakati na kuleta manufaa kwa wakutubi na maktaba zao inabidi TLA nayo ibadilike.

’’Mipango yetu ya kimkakati inahusisha malengo makuu kama mabadiliko ya kisheria/kikatiba na kimuundo na utafutaji wa rasilimali ili kujijengea uwezo na kufanya yale yote yanayotakiwa kwa ajili ya kuijenga na kuiendeleza fani ya ukutubi’’ alisema.

Aidha anasema mipango utoaji wa elimu na kujenga mitandao na mahusiano miongoni mwa wakutubi na maktaba za Tanzania na vyama vya wakutubi wa nje ya nchi.

Akizungumzia historia, anasema chama hicho kilianzishwa mwaka 1972 baada ya kuvunjika kwa Chama cha Wakutubi cha Afrika Mashariki.

Chama hicho kilipata usajili kwa Msajili wa Vyama mwaka 1973. Lengo kuu la la chama hicho, wakati kinaanzishwa lilikuwa ni kuwafanya wakutubi wa Tanzania kuwa kitu kimoja.

Chama hicho, pia kilihusika sana katika uhamasishaji wa kuanzishwa kwa maktaba nchini Tanzania na kutoa elimu endelevu kwa wanachma wake na wafanyakazi wa maktaba.

TLA pia ilishiriki kikamilifu kuhamasisha maktaba za umma na nyingine kutekeleza programu za serikali kwenye miaka ya 1970 na 1980.

Programu kama za elimu ya watu wazima na nyinginezo zilihitaji sana msaada wa maktaba kwenye kusambaza taarifa na habari.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.