|
Taa za kuongoza magari zitumike wakati wote
2005-07-26 08:33:01
Na Mhariri
Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi kubwa. Majengo yanayoongezeka kama unyoya na wakazi wake wanazidi kuongezeka. Magari nayo yanaongezeka kwa kasi kubwa.
Kwa hakika watu wengi sasa wanamiliki magari.
Lakini ongezeko hilo la magari haliendi sambamba na ongezeko la barabara. Kutokana na hali hiyo usafiri saa zile ambazo watu ama wanaenda kazini ama wanarudi nyumbani kutoka kazini unakuwa wa shida kubwa.
Pia usafiri huwa mgumu hata wakati wa mchana ambapo watu ama wanaenda ama wanatoka kwa mapumziko ya mchana.
Kwa jumla hali ni vurugu tupu. Kuna haja kubwa kwa barabara kuongezwa na zingine kupanuliwa ili kuwezesha magari mengi yasafiri kwa urahisi.
Wakati tunatoa kilio hiki cha kuongezwa na kupanuliwa barabara, tunachukua nafasi hii kuzungumzia juhudi za ndugu zetu askari wa usalama barabarama – Trafiki – za kujaribu kusaidia kupunguza msongamano kwenye barabara zetu.
Hawa jamaa, wake kwa waume kila kukicha asubuhi . mchana na jioni wako kazini kuongoza magari na wakati mwingine tunaambiwa hupata madhara ya kugongwa.
Kwa kuona umuhimu na uzito wa kazi yao, awali ya yote tunapenda kuwapongeza.
Hata hivyo tunaona kuna haja ya trafiki kupunguziwa jukumu hili la kuongoza magari kila kukicha barabarani.
Tunashauri kwamba katika maeneo ambapo zipo taa za kuongoza magari barabarani zitumike na kama zina dosari zirekebishwe.
Tunasema hivi kwamba hivi sasa tumo katika karne ya sayansi na teknolojia ni vizuri matumizi ya teknolojia ya kisasa yakapewa mkazo zaidi.
Kwa kuzingatia ukweli kwamba idadi ya magari imeongezeka, ni muhimu taa zikatumika zaidi na yale maeneo ambayo yanastahili kuwa na taa, basi yawekewe.
Bila shaka taa zikitumika zaidi, zitatoa nafasi kwa trafiki kusimamia na kuangalia mambo mengine ya usalama barabarani na kufanya hali kuwa nzuri kwa jumla.
|