|
Mtaala wa somo la dini duniani waandaliwa
2005-07-26 08:34:39
Na Mashaka Mgeta, Dodoma
Serikali inandaa utaratibu wa kuandaa mtaala wa somo la dini za duniani litakalofundishwa mashuleni bila kujali tofauti za imani ya wanafunzi.
Hayo yalisemwa jana Bungeni na Waziri wa Elimu na Utamaduni, Bw. Joseph Mungai alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibiti, Profesa Juma Mikidadi (CCM).
Profesa Mikidadi alitaka kujua kama utekelezaji wa mtaala huo hauwezi kutoa fursa kwa walimu kufundisha masomo yanayohusu dini ambayo wanafunzi hawaamini mafundisho na imani zake.
Bw. Mungai alisema, mchakato wa kuandaa mtaala huo unaendelea kwa kuwahusisha wadau wote ili kuliwezesha somo hilo kujumuisha misingi ya dini mbalimbali.
Hata hivyo, Bw. Mungai hakusema kama kuanza kufundishwa kwa somo hilo kutaondoa ama hakutaondoa nafasi ya somo la dini linalofundishwa sasa katika shule zote nchini.
Bw. Mungai alisema, kuwepo kwa somo la dini za duniani kutawawezesha vijana wa Kitanzania kupata uelewa mpana na ujuzi wa jinsi watu wa imani tofauti wanavyoweza kuishi kwa pamoja, kuelewana na bila kuathiri mifumo ya maisha ya kawaida hasa katika kipindi hiki cha utandawazi.
Aidha, Bw. Mungai alisema somo la dini litaendelea kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili katika shule za msingi na Kiingereza kwa shule za sekondari nchini.
Bw. Mungai alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CCM) aliyetaka kujua sababu za wanafunzi hao kusomeshwa somo hilo kwa Kiingereza badala ya Kiarabu au Kiswahili.
Bw. Mungai alisema, hatua ya kutumia Kiswahili na Kiingereza katika kufundisha somo la dini, inatokana na utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo iliyopitishwa na Bunge.
Alisema sera hiyo iliidhinisha matumizi ya lugha hizo.
Aidha, Bw. Mungai alisema hakuna somo la dini katika mtaala wa elimu nchini, wala viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuamua lugha ya kufundishia somo lolote katika shule.
Mwenye mamlaka ya uamuzi huo kwa mujibu wa sheria ya elimu ni Ofisa Kiongozi ambaye pia anatakiwa kuzingatia maagizo yoyote maalum au ya kiujumla ya Waziri wa Elimu, alisema.
Wakati huo huo, Bw. Mungai alisema tatizo la kujua lugha za Kiingereza bado ni kubwa kwa wanafunzi wa ngazi tofauti hapa nchini.
Hata hivyo, Bw. Mungai alisema, suluhu ya kuondokana na tatizo hilo siyo kuacha kutumia lugha hiyo, bali ni kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha wanafunzi hao kuwa katika hali hiyo.
|