|
Zao jipya la Lulu kuwaongezea kipato wananchi wa Mafia
2005-09-22 08:51:23
Na Lusekelo Philemon
Uzalishaji wa zao jipya la Lulu katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani,unatarajiwa kutoa fursa za ajira na kuinua kipato cha wakazi wa eneo hilo.
Zao hilo linatokana na mnyama chaza apatikanaye baharini. Katika makala haya Mwandishi, Lusekelo Philemon anaelezea kwa kina zao hilo.
Kisiwa cha Mafia ni moja ya maeneo yaliyofunikwa na maliasili kibao zisizotumika kwa miaka mingi. Juhudi mpya zilizoanza kufanywa na Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengevu (MPRU) kilicho chini ya Wizara ya Mali Asili na Utalii zimewezesha kuanzishwa kwa miradi mbalimbali inayoendana na kilimo cha zao la Lulu ambalo ni muhimu sana katika kuboresha hali za wananchi kiuchumi.
Uzalishaji mkubwa wa zao hilo unategemewa kuanza hivi karibuni kisiwani humo. Hatua hiyo inaelezwa kwamba itaweza kupanua wigo wa ajira kwa wakazi wa kada mbalimbali hususani wanawake.
Kitengo cha MPR kimedhamiria kukuza uzalishaji wa zao hilo katika fukwe za bahari hapa nchini. Zao la lulu linalotokana na mnyama apatikanaye baharini maarufu kama Chaza.
Lulu ni zao ambalo linahitajika sana kutokana na umuhimu wake, ambapo linatumika kutengeneza vito mbalimbali vya thamani kama vile bangili, pete, mikufu, vifungo, hereni na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.
Kitengo cha hifadhi ya bahari, kimefikia hatua ya kuwahamasisha wananchi waishio kwenye hifadhi ya Mafia, kuanzisha miradi ya kufuga Chaza baada ya kufanya utafiti wa kina na kugundua kuwa miradi hiyo inaweza kuwaondolea wananchi umaskini.
Uzalishaji wa Lulu, ni miongoni mwa miradi muhimu itakayoweza kuwasaidia wakazi wa Pwani kutojishughulisha zaidi na uvuvi wa samaki pekee ambao kwa sasa unahitaji teknolojia kubwa zaidi.
Uzalishaji wa zao hilo utawapatia wakazi wa maeneo ya Pwani fursa ya kuongeza vipato vyao kwa sababu ya uhakika wa soko lake nchi za nje.
Zaidi ya kilo 150 za lulu zilivunwa tangu mwaka jana, ambapo mradi wa majaribio kuhusu uzalishaji wa zao hilo, ulianzishwa kwa mara ya kwanza visiwani.
Majaribio hayo ya awali ya kuzalisha lulu yaliweza kuzalisha lulu 143 zinazokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni saba.
Meneja wa kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengevu (MPRU), Bw. Chikambi Rumisha, anasema kuwa, mashamba ya kufuga chaza kwa ajili ya Lulu yanatarajiwa kuwa tayari na kufanya kazi mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa meneja huyo, uamuzi wa kuanzisha mashamba hayo, umekuja kutokana na mafanikio ya mafunzo yaliyotolewa kwa wananchi wa Mafia kuhusu namna nzuri ya kuzalisha Lulu kwa faida.
Bw. Rumisha, anasema mashamba ya kufugia chaza hadi kupata lulu huchukua miezi minane kabla ya kuvunwa.
Shamba la lulu anafafanua kuwa ni tofauti na mashamba yaliyozoeleka na watu wengi kwani shamba hilo hutayarishiwa baharini kwenye maeneo maalum kwa ajili ya kufugia chaza.
Shamba la zao hili linatayarishwa kwenye maji yaliyo kwenye fukwe za bahari, huku yakiwa yamewekewa ishara maalum. Uzalishaji wake hauharibu mazingira ya bahari, Bw. Rumisha anasema.
Akielezea uzalishaji wa zao hilo, meneja huyo anasema baada ya mnyama huyo kukamatwa huleweshwa kwa dawa maalum yenye kilevi cha pombe kabla ya kuwekwa kipande cha plasitiki.
Hatua hiyo, humfanya mnyama huyo kuufungua mwili wake. Hali hii humfanya mfugaji kuingiza kirahisi kipande hicho cha plastiki kwenye mwili wa chaza.
Baada ya chaza kuwekewa kipande hicho, anapelekwa majini kwenye shamba maalum, ambapo mara baada ya kilevi kwisha mnyama huyo hujifunga na kuanza kutengeneza Lulu mwilini mwake.
Lakini kazi hii inapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa kwani ikikosewa ni hatari kwa mfugaji kwani Chaza akikubana anaweza kukuumiza, Bw. Rumisha anasisitiza.
Mlezi Mkuu wa Hifadhi ya Bahari, Kisiwani Mafia, Bw. George Msumi anasema kuwa mafunzo mengi yalitolewa kwa wenyeji wa kisiwa hicho kuhusiana na uzalishaji wa zao hilo.
Mafunzo hayo,Bw. Msumi anasema kuwa yatasaidia sana katika mradi huo, ambao umepokewa kwa mwitikio chanya na wakazi wa kisiwa hicho.
Thamani ya ubora wa zao hilo likishavunwa inafananishwa na dhahabu.
Hii itasaidia sana katika mikakati yetu ya kuhakikisha kwamba hifadhi ya bahari inakuwa endelevu kwa vizazi vijavyo. Lakini wakati huohuo hali ya maisha kwa wenyeji inaboreshwa, Bw. Msumi anafafanua.
Kwa upande wake tena meneja wa kitengo cha hifadhi Bw Rumisha anasema, mradi huo utakuwa endelevu na unaweza kuyahusisha maeneo yote yaliyo kwenye ukanda wa pwani.
Watakaoweza kuzalisha kwa wingi zaidi watanufaika zaidi na zao hili, Bw. Rumisha anasisitiza.
Amesema kuwa soko la bidhaa hiyo ni kubwa katika nchi zilizoendelea. Nchi hizo ni pamoja na Australia na baadhi ya nchi zilizopo kusini mwa Asia.
Katika nchi ya Vietnam kwa mfano, Rumisha anasema kuwa watu wengi wamejitosa kwenye uzalishaji wa zao hilo ambapo baadhi yao sasa ni mabilionea.
Mradi huu ni muhimu kwa uchumi wa eneo husika na nchi kwa ujumla, ambapo unaweza kuingiza fedha za kigeni zinazoweza kusaidia kuinua uchumi na kuondokana na umaskini.
Mpango huu utasaidia sana kupunguza umaskini miongoni mwao wakazi wa Mafia endapo utafanyika kwa umakini mkubwa, Bw. Rumisha anasema.
Maafisa wa kitengo cha hifadhi bahari wanasema kuwa Lulu zinazovunwa kisiwani Mafia zina ubora wa hali ya juu kuliko sehemu nyingine yoyote ya duniani, hali itakayosabaisha soko lake kupanda zaidi katika siku za usoni.
Bei ya Lulu moja ni kati ya dola za kimarekani 12 na 50 ambazo ni sawa na shilingi 12,000 na 50,000.
Kutokana na hali hiyo, mabadiliko makubwa kiuchumi yanaweza kutokea katika maeneo ya mwambao endapo zao hilo litapata msukumo wa kutosha miongoni mwa wahusika.
Inaelezwa kuwa nyama ya Chaza ni tamu sana na inauzwa kwa bei kubwa zaidi katika mahoteli ya kitalii ndani na nje ya nchi.
Hali hiyo itawawezesha wafugaji kupata faida mara mbili na kuinua hali ya maisha katika familia na jamii nzima kwa ujumla.
|