|
Wanawake kuendesha teksi jijini Dar es Salaam
2005-09-24 09:01:51
Na Mwanaidi Swed
Madereva wanawake walihitimu vyema, hivi karibuni wataanza kuajiriwa kuendesha teksi katika jiji la Dar es Salaam.
Hatua hiyo inatekelezwa na Chama cha Madereva Teksi nchini (TUNAWAJALI) ikilenga kupanua nafasi za ajira kwa akina mama ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia pato la familia. Makala hii ya Mwandishi Mwanaidi Swed inaeleza zaidi kuhusu mpango huo.
Hivi karibuni jiji la Dar es Salaam litashuhudia wanawake wakiendesha teksi za kubebea abiria toka sehemu moja kwenda nyingine, kama wanavyofanya madereva wanaume tayari madereva kumi wanawake wamehitimu mafunzo na sasa wanachosubiri ni kupatiwa leseni za kuendeshea.
Mkakati huo unatekelezwa na Chama cha Madereva wa teksi nchini (TUNAWAJALI) kwa lengo la kuhakikisha kuwa unapanua nafasi za ajira, kuinua vipato vyao na kujikwamua kiuchumi.
Chama kimeandaa mpango mahususi kwa ajili ya kutaka kuwasaidia wanawake kupata ajira zao kupitia kazi ya udereva teksi kama ilivyo kwa wanaume, anaeleza Bw. Chembe.
Mwenyekiti wa TUNAWAJALI, Charles Chembe, anasema kuwa kufuatia kutolewa fursa hiyo, wanawake zaidi ya 20 wamejitokeza ili kuhakikisha kuwa wananufaika kikamilifu.
Chama hicho, kimeanza kutoa mafunzo kwa akina mama kwa kutumia gari la kukodi linalochangiwa kiasi kidogo cha gharama na akina mama hao.
Hata hivyo anasema kwa kipindi hiki ambacho chama bado hakijawa na uwezo wa kununua gari maalum ya mafunzo ya vitendo yanafanyika kwa kutumia gari la kukodi, ambapo akinamama wenyewe wanachangishana kugharamia ukodishaji kwa ajili ya mafunzo na mafuta.
Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa magari yanayokodiwa huonyesha wasiwasi wanapoona kuwa wanaojifundishia magari yao ni wanawake.
Akina mama hao wameonyesha shauku kubwa ya kujifunza ili kuhakikisha kuwa wanahitimu kwa muda mfupi na kuidhihirishia jamii kuwa wanaweza kufanya kazi nyingi hata zile zinazodhaniwa kuwa ni kwa ajili ya wanaume tu.
Bw. Chenge anasema uhaba wa vifaa kwa ajili ya kufanikisha mafunzo ni miongoni mwa vikwazo vinavyosababisha mafunzo hayo kuchukua muda mrefu zaidi, vinginevyo baada ya muda mfupi akina mama wengi wenye nia hiyo watahitimu mafunzo hayo.
Kuhusu michango kwa ajili ya kukodi magari ya mafunzo,Bw Chenge anasema kuwa huchangia kati ya sh 1,500 - sh 2000 kila mmoja kila siku ya mafunzo, ambapo hukusanywa na kisha kukodi gari na kununulia mafuta kwa ajili kukodi.
Kwa sasa wakati utararibu wa kutoa mikopo kwa kununulia magari haujakamilika akina mama hao wakishahitimu mafunzo na kupata leseni ni kwamba wataanza kutafuta ajira kwa wenye magari na kuwekeana mikataba kama ilivyo kwa madereva wengine.
Chama hicho katika mpango wake wa muda mrefu, kinampango wa kuhakikisha wanawake hao wanamiliki magari yao wenyewe kwa kuwapatia mikopo ya magari.
Kampuni mbalimbali zinazouza magari, tayari yamefanya makubaliano na chama hicho, ikiwa pamoja na watu binafsi ambapo magari yapatayo 170 yatakopeshwa kwa utaratibu maalum uliowekwa.
Hatua hiyo ikikamilika na wanawake kupata uzoefu wa kutosha katika barabara za jiji la Dar es Salaam, inatarajiwa kuwa watasaidia sana kuinua biashara za teksi kwa kuwa kivutio maalum kwa wateja.
Bw. Chembe anasema kuwa mkakati huo utaisuta ile dhamira potofu iliyojengekeka kwa baadhi ya watu kuwa kazi ya udereva teksi ni maalum kwa ajili ya wanaume tu na si kwa ajili ya wanawake na kuwanyima fursa za ajira kwa sababau ya maumbile yao.
Katika kuhakikisha kuwa madereva hao wanawake wanakuwa na usalama wa kitosha barabarani dhidi ya vitendo vya uhalifu, Bw. Chembe anasema kuwa chama hicho kitaunda mtandao maalum utakaongoza shughuli nzima za madereva teksi ili kuwaokoa katika majanga ambayo yatatishia magari na maisha yao.
Mtandao huo hautawasaidia wanawake tu bali hata wanaume, ambao mara nyingi wamekuwa wakikumbana na matatizo wakiwa kazini na baadhi yao kupoteza maisha kabisa.
Bw. Chembe anasema kuwa, mpango huo unaweza kuanza muda wowote mara watakapokamilisha taratibu zinazohitajika.
Kwa ujumla, anasema kazi ya udereva teksi, ikifanywa na wanawake inatarajiwa kuwa ya uaminifu kwa wateja na kuondoa dhana kuwa madereva wengi wa teksi si waaminifu kutokana na wengi wao kuvamia kazi hiyo bila kujua maadili ya kazi hiyo.
Anasema kuwa baadhi ya madereva wanaume wamewahi kutumiwa katika kuhatarisha maisha ya wateja wao ili mradi tu kuna chochote wameahidiwa.
Pamoja na kuwa kuna badhi ya wanawake si waaminifu lakini kutokana na mafunzo watakayoyapata anaamini kuwa watu watafanya kazi hiyo kwa ukamilifu na umakini zaidi katika kuweka tofauti za kiutendaji.
Lazima jiji la Dar es Salaam libadilike na kuwa kivutio kama ilivyo kwa baadhi ya miji ya nchi za nje kuwa hata wanawake ndiyo wanaofanya kazi ya udereva teksi kama moja ya kazi inayowaingizia kipato kinachowawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku. alisema.
Miongoni mwa watakaonufaika na elimu au utaalamu huo ni walimu wa shule za msingi jijini Dar es Salaam ambapo watakuwa wakifanya kazi hiyo kama ya ziada na kwa wale mbao hawana ajira watatumia muda wao mwingi zaidi hata kuwa ajira ya kudumu.
Hata hivyo, Bw. Charles anasema kuwa yapo matatizo mbalimbali wanayoyapata katika kufanikisha zoezi hilo yakiwemo kukosa gari la kudumu la kufundishia, ambapo amewaomba watu wenye magari kuwasaidia gari lolote linalofaa kutumika kutolea mafunzo kwa wanawake walioamua kujifunza kazi ya udereva teksi.
Upungufu wa magari unaosababisha kuwa na foleni wakati wa mafunzo hali ambayo inaweza kuboreshwa kama magari mengi zaidi yatapatikana.
Naye, Mwenyekiti wa muda wa mafunzo hayo, Mama Rose Kibasa, amesema kujiunga kwao na udereva teksi sio tu kwa ajili ya kupata ujuzi wa udereva , bali pia kutawasaidia kupata ajira ama kujiajiri wenyewe.
Kwa mujibu wa Bi. Kibasa, mafunzo hayo yameanza kutolewa kwa wanawake zaidi ya 20 katika awamu ya kwanza,ambapo katika mafunzo hayo wapo wanawake wa makundi ya kiwango mbalimbali cha elimu na uelewa.
Anasema kuwa, licha ya wao kupata ujuzi pia wanategemea kuwa walimu kwa kuwafundisha madereva lugha nzuri ya mawasiliano na wateja, ikiwa pamoja na lugha ya Kiingereza ambayo huwa ni kikwazo kwa baadhi ya watu wengi ili waweze kuwa na mawasilinao mazuri pindi wanapokutana na wateja wasiojua Kiswahili.
Kazi ya udereva teksi kwa walimu haitakuwa kama ajira yao ya kudumu bali wataifanya kama kazi ya ziada na wale wengine watakuwa wamepata ajira yao ya kudumu.anasema Mwenyekiti huyo.
Wanawake waliojiunga na mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na chama hicho cha TUNAWAJALI kwa kuwashirikisha wanawake katika mpango huo.
Bi. Kibasa anasema kuwa wanawapongeza sana TUNAWAJALI kwa kuona umuhimu wao katika jamii na hatua hiyo, itakiongezea hadhi chama hicho na pia utakuwa mfano kwa taasisi nyingine zisizokuwa na utaratibu wowote wa kuwapa nafasi akinamama kuchangia maendeleo ya taifa.
Chama hicho kilianzishwa rasmi mwaka 2002 kikiwa na malengo makubwa ya kutaka kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wa teksi na kuondokana na mfumo holela wa kazi hiyo na kuuweka katika mfumo wa ajira.
Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Charles Chembe, anasema kuwa chama kina wanachama 678 na kimefungua matawi kadhaa katika mikoa minane ambayo ni Dodoma, Mbeya. Morogoro, Arusha, Tabora, Kilimanjaro, Pwani na Zanzibar.
Mwenyekiti huyo anasema kuwa, pamoja na shughuli hizo pia kuna vitengo vitatu vinavyoendeshwa chini ya chama hicho. Vitengo hivyo ni cha kinamama, kitengo cha Vijana pamoja na kitengo cha Elimu.
Aidha anasema kuwa katika kitengo cha kinamama zipo shughuli nyingi zinazoendeshwa chini ya kitengo hicho kama kuwapatia kinamama mafunzo mbalimbali yakiwemo ushonaji,udereva teksi na kuwapatia kinamama kazi za kusimamia vituo vya teksi.
Kitengo cha kusimamia vituo kinamama hufanya kazi hiyo na hujipatia pesa kwa kukusanya ushuru katika vituo walivyopangiwa. Hukusanya ushuru wa shilingi 500/- kwa kila dereva na wao kuondoka na Sh. 2000/- kwa siku.
Katika kitengo hicho pia kinashirikisha wanaume ingawa wanawake ndio wanaopewa kipaumbele ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na sio kubaki kuwa tegemezi kama ilivyo kwa wanawake walio wengi.
|