25 Sep 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tuchague mtu na si chama
 
2005-09-25 08:02:49
Na Hamisi Kibari

Wakati akizindua kampeni za chama chake pale kwenye Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam, Agosti 21, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Ben William Mkapa, aliwataka wananchi wawachague wagombea waliosimamishwa na chama chake, akitoa sababu moja kubwa kwamba wana uzoefu.

Mimi nilibahatika kuwa kwenye msafara wake wa kampeni mwaka 2000.

Hoja yake kote tulikuzunguka, hususan katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera, ilikuwa hiyo hiyo, ya kuwataka Watanzania wakichague CCM, eti kwa vile kina viongozi wazoefu.

Na kwa kweli siwezi kutegemea kiongozi wa chama fulani aseme vinginevyo, labda kama atakuwa amekomaa akili kupita kiasi kama alivyo mgombea urais kupitia Chadema, Freeman Mbowe, anayediriki kuwapigia debe wagombea wa vyama vingine, pale anapogundua kwamba ndio wanaokubalika zaidi kuliko wale wa chama chake!

Mimi ninamuomba Mbowe azidi kukomaa akili zaidi na kumpigia debe hata mgombea wa CCM kama atakuta mahala ambapo mgombea huyo anakubalika, amesaidia sana kuwaletea wananchi maendeleo au ana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo, na au hata kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho kikongwe.

Na kwa kweli mimi ninaamini kuwa hiyo ndiyo siasa inayolenga kujenga nchi na si kujenga matumbo ya wanasiasa.

Tusijenge fitna kama za mwenyekiti wa chama fulani cha upinzani ambaye inasemekana kuwa mbunge wake alipowapokea viongozi wa chama tawala waliotembelea katika jimbo lake, akachukia sana na kuanzisha ’bifu’ kali ambalo limeendelea hadi kusababisha mbunge huyo kujiondoa katika chama chake na kurejea CCM.

Sasa turudi kwenye hoja ya Mwenyekiti wa CCM, kwamba tuchague viongozi wa CCM kwa vile wana uzoefu, na tuanze kwa kuujadili huo uzoefu.

Kama kweli uzoefu una la kusema kulinganisha na uwezo wa mtu, bila shaka CCM wenyewe wangelimchagua Dk. Salim Ahmed Salim kuwa mgombea wao wa urais kwa sababu kati ya watu waliowania kupeperusha bendera ya chama hicho katika ngazi ya urais, yeye alikuwa ’anatisha’ kwa uzoefu!

Na kama si Dk. Salim, mtu aliyekuwa anafuata kwa uzoefu basi alikuwa si mwingine, bali mzee John Samweli Malecela.

Lakini bila shaka, wana-CCM walikuwa wakitafuta mtu imara kwa wakati huu kulingana na majukumu waliotaka kumpa kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, na si vinginevyo.

Hata hotuba ya Mkapa kabla ya uteuzi wa Kikwete, iliepuka kabisa kuzungumzia ’uzoefu’ wa akina Dk. Salim isipokuwa ’anayependwa na vijana’.

Pamoja na hayo, uzoefu tunaoambiwa ni wa aina gani sasa? Je, ni uzoefu wa kula rushwa, uzoefu wa kuuza nchi au uzoefu wa kusinzia bungeni? Ni upi sasa?

Na je, tunapoangalia uzoefu hatuoni kama tunapingana na dhana ya vijana kung’atuka na kuwapisha wazee? Na kwa kweli, kama ningekuwa na uwezo, ningeweka vipindi viwili ama vitatu vya kugombea ubunge.

Nilishajiuliza sana kwa nini kuna watu wamekuwa wabunge kwa zaidi ya miaka 20, wao tu? Ninaweza nisijali sana katika nafasi ya ubunge mtu anapopewa kiti hicho kwa miaka 15, lakini inashangaza kwa mtu ambaye amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 20 na bado anataka.

Katika kumuenzi mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wazee hawana budi kung’atuka na wale wanaong’ang’ania sisi wapiga kura tutumie kura zetu ’kuwapiga chini.’

Enzi za ’vingunge’ zimekwisha jameni, lazima sasa tuwe na zama za ’vikwete’, na pengine huu ni mtazamo wa watanzania wengi wanaoamini katika falsafa ya mgombea urais wa CCM ya ’kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya’. Toka lini wazee wakawa na ari, nguvu na kasi mpya?

Na pengine ndio maana wengi walishangilia pale wazee kama Malecela na Salim walipopigwa chini.

Tuchukulie mtu kama Salim, kwa mfano, pamoja na sifa zake nyingi, lakini alishastaafu kazi kule kwenye Umoja wa Afrika.

Alitakiwa kupumzika na kutoa ushauri pale unapotakiwa na si kumtwika mzigo mzito wa kuongoza nchi kubwa na maskini kama hii.

Dhana hii ya kuchagua chama mimi ninaona kama imepitwa na wakati, na hasa pale chama husika kinapokuwa hakijasimamisha mtu anayekubalika zaidi katika eneo husika.
Kinachonifurahisha, Watanzania taratibu wameanza kumka.

Lazima sasa wahusika wa hivi vyama, na hususan chama tawala, wang’amue hilo kama walikuwa bado.

Nina habari kwamba, katika maeneo kadhaa ya nchi ambako wagombea wa ubunge kupitia CCM, ama walikuwa si chaguo la wananchi walio wengi (isipokuwa kwa kigenge kidogo cha viongozi wa CCM) au walichaguliwa kwa mbinu chafu, wananchi wameonyesha waziwazi kuwakataa kwa njia ya kuwazomea wagombea hao mbele ya mgombea urais wa chama hicho, Jakaya Mrisho Kikwete.

Wiki chache, nilieleza kitu nilichokiona katika baadhi ya majimbo kule kanda ya ziwa.

Hata kama wagombea wa chama tawala hawakuzomewa wakati Kikwete alipokuwa akitembelea majimbo hayo kujinadi, nilisikia kwamba walipita kura za maoni kwa njia chafu.

Kwa msingi huo, kama wananchi watachagua mtu na si chama, basi hakuna mashaka kwamba vyama vya upinzani havitakuwa na kazi kubwa kuingia bungeni, isipokuwa kama navyo vimesimamisha wagombea ’bomu’.

Kwa sababu inawezekana kabisa mgombea wa chama tawala, japo hakubaliki kulinganisha na yule waliokuwa wakimtaka wananchi, lakini aweza kuwa afadhali kulinganisha na wale wa vyama vya upinzani.

Lakini kwa nini mimi, bila shaka na watu wengine wanaoitakia heri nchi yetu, wanaamini katika falsafa ya kuchagua mtu na si chama.

Sababu ziko nyingi, lakini kubwa ni kwamba mchanganyiko mzuri wa wabunge bungeni, hulichangamsha na kuibuka na mambo mazuri kwa ajili ya maendeleo ya sisi wananchi na si ya chama ama viongozi wa chama tawala kama ilivyo sasa.

Kuna ushahidi kwamba bunge la mwaka 1995 hadi 2000, lilikuwa limechangamka sana kwa hoja, kuliko lililofuatia kwa idadi ya wabunge kutokana na kambi ya upinzani kuwa na idadi kubwa kidogo.

Inaelezwa kuwa bunge la mwaka 2000 hadi mwaka huu lilikuwa limedorora sana kulinganisha na la nyuma yake kwa vile wapinzani walipungua sana.

Tena wazoefu wanasema ni afadhali hata pale lilipokuwa la chama kimoja kuliko bunge lililopita.

Wanadai kwamba, sasa hivi, kwa mfano, mbunge wa CCM, hulazimika kutetea hata upuuzi wa serikali, alimradi tu serikali ya chama chake isionekane hovyo mbele ya wananchi. Lakini wakati wa chama kimoja, hilo halikuwepo.

Wakati wabunge wa upinzani huwa na kazi ya kueleza mapungufu ya serikali ama miswada inayofikishwa bungeni, nao hawajasalimika na kutetea upinzani, hata kama unafanya mambo ndivyo sivyo.

Hata hivyo, dhana iliyopo ni kwamba wapinzani wanapokuwa wengi bungeni, huifanya serikali inapoleta miswada yake kujiandaa vizuri zaidi na lazima iogope kufanya mambo holela ama kwa maslahi yasiyo ya wananchi kwa sababu wapo watu wa kuisema bila woga.

Sababu ya pili ni kwamba, mpaka sasa haijulikani ni kwa maslahi ya nani wakubwa wamekataa kufanya marekebisho katika katiba ili kuwepo na wagombea huru.

Chukulia mtu kama mimi sina chama na wala sipendi kuwa nacho.

Kwa mantiki hiyo, katiba inayonipa haki cha kuchagua na kuchaguliwa, inaniwekea kiwingu kwenye kuchaguliwa, kwamba lazima nipitie chama cha siasa.

Pengine kwa kutoruhusu wagombea binafsi, labda ndipo watu kama Benjamini Mkapa wanapata uwezo wa kuwataka wananchi wachague chama na si mtu anayefaa.

Pamoja na kwamba vyama vina sera, zikiwemo ambazo hazitekelezeki, lakini mimi naamini uwezo wa mgombea mmoja mmoja, mwenye uwezo wa kufikisha vyema kero za wananchi na kujenga hoja za kuisaidia serikali ama wananchi wenyewe kujisaidia katika kutatua kero zao, ndiye anayepaswa kuchaguliwa.

Na hizi hoja za kuchagua chama, nazo zimechangia sana wahusika kuona hakuna haja ya kuwa na serikali ya mseto.

Mimi ninaamini, tungekuwa na serikali ya mseto, tungekuwa tumepiga maendeleo zaidi ya haya.

Shime wananchi. Tuondokane na hii dhana ya kuchagua chama. Kama wewe ni mpenzi wa Chadema, pima uwezo wa wagombea wengine. Kama yule wa CCM ama CUF unadhani anafaa, chagua huyo.

Na hasa mimi ninadhani kigezo kingine ni cha kumjaribu mgombea mpya, kama anaonekana ana uwezo, na kuachana na ving’ang’anizi, na hasa kama hawana jipya.

Kingine ni kujaribu chama kingine, kama jimbo lenu miaka nenda rudi mnakipa chama hicho hicho tu.

Tubadilishe mapishi mwaka huu tuone kama yatakuwa na ladha nzuri kuliko tuliozoea.

Nadhani ni jambo zuri. Kama tukigundua kwamba mapishi haya mapya heri ya zamani, miaka mitano si mingi. Tunawapiga chini.

Na ile dhana kwamba huu si muda wa kujaribu nayo ni potofu.

Nitaijadili siku moja upotofu wake kama Mwenyezi Mungu ataendelea kunijaalia.
Jumapili njema.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.