|
Magari yakaguliwe uimara na usalama wake
2005-09-26 08:57:06
Na Grace Chilingola
Wakati maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani yanaendelea nchini kote, mikakati mbalimbali inatekelezwa ili kujaribu kudhibiti mfumuko wa ajali za barabarani, ambapo tatizo hilo bado linaendelea kufupisha maisha ya watu ghafla, kusababisha majeruhi na uharibifu wa mali.
Makala hii ya Mwandishi wa PST,Grace Chilingola inafafanua kuhusu umuhimu wa kuendesha kwa usalama na kuzingatia sheria za usalama.
Ajali za barabarani zinalisababishia Taifa hasara kubwa ya mali na raslimali watu hata kuathiri uchumi na maendeleo kwa ujumla.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa, taifa limejikuta likibebeshwa hasara kubwa kinyume na juhudi za kujaribu kuinua uchumi na maisha ya watu, ikiwa pamoja na gharama kubwa za matibabu kwa majeruhi na fidia kwa waathirika.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini SACP Peter Kivuyo, akizungumzia hali halisi ya ajali anasema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu, kumetokea ajali za barabarani zipatazo 7,816 hapa nchini na kusababisha vifo vya watu 1,047 na majeruhi 7,109.
Taifa linatumia kiasi kikubwa cha fedha kugharamia ajali hizi kwa kuwatibia majeruhi na kugharamia uharibifu wa mali, anasema Kamanda Kivuyo.
Uzembe na dharau kwa kiasi fulani zinazofanywa na baadhi ya madereva hapa nchini kwa kutozingatia sheria na alama za barabarani Kamanda anasema zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ajali za barabarani.
Anasema dereva anayebainika kusababisha ajali kwa uzembe huchukuliwa hatua za kisheria za kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na kwamba bila kufanya hivyo mmiliki hawezi kudai bima bila kuwa na vielelezo.
Akifafanua takwimu za ajali za barabarani kamanda Kivuyo anasema kuwa, katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 1995 hadi mwaka 2004 ajali za barabarani zipatazo 145,482 zimetokea na kusababisha vifo vya watu 18,410 na majeruhi wapatao 150,100 nchini.
Ajali hizo, zimekuwa zikiathiri makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara kwa viwango tofauti wakiwemo madereva, abiria, waenda kwa miguu, wapanda pikipiki na waendesha baiskeli.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kundi lililoathirika zaidi ni la abiria, likifuatiwa na watembea kwa miguu, wapanda baiskeli, madereva, wapanda pikipiki na wasukuma mikokoteni.
Utafiti umeonyesha kuwa, ajali zinazohusisha magari yaliyofungwa vidhibiti mwendo, madhara yake ni madogo ikilinganishwa na ajali zinazohusisha magari ya abiria, ambayo hayana vifaa hivyo ama vimelegezwa au kuharibiwa kabisa tena kwa makusudi.
Zipo sababu mbalimbali zinazochangia ajali za barabarani, ikiwa ni pamoja na ubovu wa magari, barabara, makosa ya binadamu na madereva na watumiaji wa barabara kutozingatia kanuni na sheria za usalama barabarani.
Wiki ya nenda kwa usalama kitaifa mwaka huu inaadhimishwa katika mkoa wa Ruvuma ambapo Kamanda amewataka wananchi kupeleka magari yao kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi ili kuhakikisha kuwa yenye ubovu yanarekebishwa na kupunguza uwezekano wa kupata ajali.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam Bw. Alfred Tibaigana akizungumzia wiki hiyo anasema kuwa katika zoezi la ukaguzi wa magari lililofanyika mwezi Agosti, mwaka huu magari yapatayo 6,378 yalikaguliwa na Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam.
Kati ya magari hayo yaliyokaguliwa makubwa yalikuwa 1,285 na magari madogo yalikuwa 5,203 ambapo magari 378 yalibainika kuwa na hitilafu baada ya kukaguliwa kati yao magari madogo yalikuwa 308 na makubwa 70.
Kamanda Tibaigana akichanganua hali halisi alisema kuwa magari 6,110 yaliyobainika kuwa ni mazima yalipatiwa stika ya usalama barabarani, wakati yale mabovu yalitakiwa yafanyiwe marekebisho kisha yarudishwe ili kufanyiwa ukaguzi kwa mara nyingine.
Anasema zoezi la ukaguzi wa magari bado linaendelea kwa mwezi huu, hivyo wale wote ambao magari yao hayajakaguliwa wanapaswa kuyapeleka kwa ajili ya ukaguzi, ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza ajali za barabarani ambazo nyingine husababishwa na ubovu wa magari.
Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, huadhimishwa wiki ya mwisho ya mwezi wa Septemba, kila mwaka ikitanguliwa na zoezi la ukaguzi wa magari yote hapa nchini kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani.
Zoezi la ukaguzi wa magari hufanyika mwezi Agosti ili yale yatakayobainika kuwa ni mabovu ama yana hitilafu yaweze kufanyiwa marekebisho kabla ya kusababisha madhara makubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kusababisha ajali za barabarani ambazo hupoteza maisha ya watu na mali zao.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zinaonyesha kuwa,magari ambayo hayatafanyiwa ukaguzi, wamiliki wake huchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na wakibainika kuwa na hatia huadhibiwa.
Ajali za barabarani zimekuwa ni chanzo cha vifo na majeruhi kwa abiria na watumiaji wa barabara, na kwamba tatizo hilo limekuwa kero kubwa. Watu kupoteza maisha, kujeruhiwa na kupata vilema vya kudumu (maisha).
Pia zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali na mazingira, majeruhi kuibiwa mizigo yao na watu ambao mara nyingi huwahi kufika kwenye matukio na kujifanya wasamaria wema kwa kutaka kuwaokoa majeruhi na kisha kuwaibia na kuwaacha wakiendelea kupigania roho zao hadi pale wasamaria wema wa kweli watakapofika na kuchukua jukumu la kunusuru maisha yao.
Katika mazingira yoyote yale ni muhimu sana madereva kuendesha magari yao kwa mwendo unaozingatia usalama wa magari yao, abiria wanaowabeba na watumiaji wengineo wa barabara.
Halikadhalika ni muhimu kupima afya za wahusika, hasa macho na kuacha kutumia kilevi ambacho kinaweza kusababisha kushindwa kuyahimili magari yao barabarani.
|