|
Ushauri huu hakika ufanyiwe kazi
2005-09-27 07:31:39
Na Mhariri
Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani imezinduliwa nchini jana kwa salamu mbalimbali lakini shinikizo likiwa matumizi bora ya barabara.
HOTUBA mbalimbali zilizoambatana na uzinduzi wa juma hilo umeonyesha haja hasa ya watumiaji wa barabara kuwa na uangalifu ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.
PAMOJA na maelezo kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na suala la usalama barabarani, hoja ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ya kutolewa kwa elimu ya matumizi bora ya barabara katika masomo ya shule za msingi, sekondari na vyuo, inastahili kufanyiwa kazi.
HII inatokana na ukweli kuwa katika miji yetu kuna udhaifu mkubwa katika matumizi ya barabara.
UDHAIFU huu unaweza kuelezwa wazi kuwa unatokana na elimu duni kuhusu barabara na usalama wake.
MATHALANI madereva wa daladala wengi wanaonyesha jinsi wasivyokuwa na elimu japo ndogo ya matumizi ya barabara kwa jinsi wanavyosimamisha magari hovyo, wakati mwingine barabara kuu na kuchomekeana ambako kunaleta fujo ya matumizi ya barabara.
PIA wapo wale wasiojali kabisa maana ya chombo walichokuwa nacho haja ya kukitazama kwa uangalifu na kukishughulikia matengenezo yanayostahili na pia kuzingatia mwenendo wa vyombo husika na kanuni za matumizi ya barabara.
KIMSINGI kama watu watapewa elimu kwa mfululizo kiasi cha makosa ni dhahiri kitapungua na barabara zetu zitakuwa mahali pazuri pa kufanyia kazi.
KAMA anavyoamini mkuu huyo wa mkoa, nasi pia tunaamini kuwa iwapo elimu hiyo itatolewa kwa utaratibu huo, itakuwa changamoto katika kupambana na ajali za barabarani ambapo moja ya vyanzo vyake ni matumizi mabaya ya barabara kwa jamii.
INGAWA ni gharama kutengeneza mitaala inayohusu somo hilo lakini hakuna kisichowezekana kwa kuzingatia kwamba miaka ijayo ni miaka ya mwendo kasi na usalama unatakiwa kwa kuangalia vyombo vinavyoingia na ubora wa injini zake.
KUELEWA matumizi ya barabara kuanzia udogo pia kutasaidia hata watakapopata nafasi ya kuwa wapangaji wetu wa mipango wa baadaye, kutambua maana ya barabara, usalama na umuhimu wake katika kuhifadhi uhai na vyombo vinavyotumika ikiwemo na miundo mbinu yenyewe.
KUKOSEKANA kwa elimu hiyo kunafanya hata waajiri, hususan wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwaajiri madereva wababaishaji, kwani wenyewe hawajui nini maana ya kuwa na mtu ambaye anajua kanuni za barabarani.
HATA utoaji wa leseni holela utakoma kwa kuwa hata hao watoaji watakuwa katika miaka yote hiyo wamejifunza maana halisi ya usalama barabarani.
UKIWAULIZA wachambuzi wa ajali za barabarani watakuambia ni ujinga wa kutofahamu kanuni za usalama , kwanza wa vyombo na mpaka matumizi ya barabara.
AIDHA katika kuadhimisha Wiki hii ya Usalama barabarani tungelipenda madereva kutambua kanuni za matumizi ya barabara ili kuokoa maisha na pia kuokoa vyombo husika.
NI vizuri kukawepo na kanuni za kuhakikisha madereva wote wamerejea shuleni kujifunza namna ya kutunza gari na barabara kwa maana ya kuwa dereva mzuri.
PIA nao watu wafundishwe kanuni za barabarani na jinsi ya kukwepa ajali zisizokuwa na msingi kwa kuwa waangalifu zaidi.
KWA kuwa ripoti za mapungufu ya uangalizi wa kanuni za barabarani ni kubwa pamoja na kuwa na kampeni za usalama barabarani kila mwaka ni heri, taifa hili likachukua hatua za makusudi kuelimisha watu wake, kama alivyoshauri Mkuu huyo wa mkoa ili kuepuka matumizi mabaya ya barabara ikiwa na kuondokana na madereva wasiozingatia kanuni za kuendesha gari kiasi cha kuharibu maisha na vyombo wanavyotumia.
|