27 Sep 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kampeni za CCM zaelekezwa kuibomoa ngome ya CUF
 
2005-09-27 07:34:43
Na Ally Mwinyikai

Vuguvugu la kampeni visiwani Zanzibar linazidi kupamba moto,wagombea wakijinadi kwa kutumia sera hizi na zile.

Hata hivyo,kwa kadri siku zinavyozidi kupita CCM kimejipambanua kukubalika vyema na wazanzibar kwa sababu ya kujitenga na siasa za hadaa zenye ahadi zisizotekelezeka zinazotumiwa na vyama vingine.


Tathmini iliyofanywa ndani ya kipindi cha wiki mbili za kampeni za Uchaguzi Mkuu Zanzibar, zinaonesha Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume anakubalika zaidi ikilinganishwa na wagombea wa vyama vingine.

Jumla ya vyama sita vya siasa vimejitokeza kugombea nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar.

Vyama hivyo ni CCM, CUF, Jahazi asilia, DP, Demokrasia Makini na NRA.

Kama hiyo haitoshi,aliyekuwa mbunge wa jimbo la Michewani,Pemba(CUF),Mbwana Haji Mbwana,akiwa na wanachama wenzake 190 wa chama cha CUF wamekihama chama hicho hivi karibuni, na kukabidhi kadi zao kwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuashiria chama hicho kuanza kumomonyoka kwa wanachama wake kukatishwa tamaa na mwenendo wa chama hicho.

Hata hivyo, pamoja na wingi wa vyama kujitokeza kugombea nafasi hiyo, vyama viwili tu - CCM na CUF - ndivyo vinavyoonekana kuwa na ushindani mkali kiasi kwamba wananchi wamekuwa wakifuatilia zaidi kampeni za vyama hivyo kuliko vingine.

Wakati zikiwa zimebakia wiki chache tu, kabla ya Watanzania hawajatumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowapenda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, 2005, ushindani unaendelea kwa vyama hivyo viwili kila kimoja kuwania kukishinda kingine.

Viongozi na wagombea wa vyama hivyo, wamekuwa katika heka heka kubwa za kutangaza ilani zao, kwa ajili ya kuwashawishi wananchi kuwachagua wagombea waliosimamishwa na vyama vyao. Kila chama kikijinadi kuwa na ilani za uhakika.

Kampeni za uchaguzi zimeshika kasi kubwa tokea Tume ya taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar ilipotangaza kuanzwa kwa shughuli hiyo Septemba 5 mwaka huu.

Kampeni hizo zinaonekana kutoa mvuto na hisia maalumu zaidi katika mikutano inayohutubiwa na wagombea wenyewe wa nafasi ya Urais.

Kigezo kikubwa cha tathmini iliyofanyika kinachukuliwa kutokana na mahudhurio ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya hadhara ya kampeni inayoandaliwa na vyama hivyo.

Hadi hivi sasa, CCM ikiongoza kwa kuwa na watu wengi wanaohudhuria kwenye mikutano yake.

Jambo lililojitokeza katika uendeshaji wa kampeni hizo, ni kuanza kwa vyama hivyo viwili kujipima kwa kiasi gani vinakubalika katika ngome za wapinzani wao.

CCM imekuwa ikijipima nguvu zake katika ngome ya CUF iliyoko kisiwani Pemba na CUF ikifanya hivyo katika kisiwa cha Unguja kwenye ngome kuu ya CCM.

Katika kufanya hivyo, CCM iliamua kuzindua kampeni zake hizo kwenye uwanja wa Gombani ya Kale ulioko Chake Chake Pemba. Uzinduzi huo ulifanyika Septemba 5, siku iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya kuanza kampeni hizo.

Kwa upande wa wapinzani wao CUF, uzinduzi wa kampeni zake ulifanyika Nairobi nchini Kenya siku hiyo hiyo, na kufuatiwa na mkutano wake wa kwanza wa hadhara uliofanyika Septemba 8 kwenye kiwanja cha Kibanda Maiti mjini Unguja.

Uzinduzi huo wa CUF ulianza kwa watu kujiuliza kilichopelekea chama hicho kuzindua kampeni zake hizo nje ya nchi ingawa wapiga kura ni Wazanzibari na sio wa Kenya.

Tathmini iliyofanywa imedhihirisha kwamba katika uzinduzi wa kampeni hizo Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimefanikiwa sana kuingia kisiwani Pemba kwa nia ya kuiteka ngome ya CUF ambayo inasadikiwa ilikuwa haiingiliki.

Mafanikio ya chama hicho ni kutokana na idadi kubwa ya watu waliohudhuria kwenye mkutano huo wa uzinduzi.

Wingi wa watu hao unaelezwa kwamba umeweza kuwatia hofu na wasiwasi hata viongozi wa CUF walioshuhudia umati huo wa watu.

Lilikuwa ni tukio la kihistoria ambalo halikupata kuonekana ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi na viongozi wa upinzani walijijengea matumaini mapya kwamba idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mkutano huo walikuwa ni kutoka Unguja na kuendelea kuamini kwamba Pemba hakuna wana-CCM.

Dhana hiyo imekuwa ikikataa kadiri kampeni zinavyozidi kushamiri kwani kinachojitokeza hivi sasa ni kuwepo mwamko mkubwa wa wananchi wa Pemba katika kukikubali Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake wa nafasi ya Urais wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Upande wa CCM umezichukulia dhana hizo za CUF ni za kujipa matumaini na unaamini kuwa hayo yalikuwa ni mafanikio kwa upande wao.

CCM inayaeleza madai yaliyotolewa na viongozi wa CUF kwamba umati huo ulichukuliwa kutoka Unguja yalikuwa ni ya kujipa moyo.

Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema idadi ya watu waliokwenda Pemba kutoka Unguja hawakuzidi 1,000 kwa kutumia meli ya M.V. Mapinduzi watu 750 na Sepideh wafuasi 250.

’Isingewezekana kwa hali yoyote kusafirisha idadi ya watu zaidi ya 30,000 walioshiriki kwenye mkutano wa uzinduzi huo,’ alifahamisha.

Wakati wana harakati za kisiasa wakitathmini hali hiyo, CUF nayo ilijitahidi kutunisha misuli yake katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni uliofanyika Kibanda Maiti, ambapo mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alizungumzia mambo mawili - upunguzaji wa kodi na uongezeko la mishahara iwapo atashinda uchaguzi huo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na watu wengi lakini haukuwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na CCM iliyofanya mkutano wake wa kampeni kwenye kiwanja hicho hicho siku moja tu baada ya mkutano wa CUF.

Matamshi ya Maalim Seif yalitoa matumaini kwa wafuasi wa chama hicho kwa kiasi fulani kutokana na ahadi zilizotolewa.

Kilichoahidiwa na mgombea huyo ni kwamba CUF ikifanikiwa kuingia madarakani kitahakikisha kodi zote za bidhaa zinazoingizwa nchini hazitozidi asilimia 10 ya bei halisi ya bidhaa hizo.

Aidha, watumishi wa Serikali watapandishiwa mishahara yao kwa kima cha chini kulipwa shilingi 100,000 badala ya sasa shilingi 50,000.

Hata hivyo, matamshi hayo yalionekana kupungua nguvu zake kufuatia uchambuzi uliofanywa baadaye na kuonekana kuwa ahadi zilizotolewa na mgombea huo wa CUF haziwezi kutekelezeka.

Ilimchukua siku mbili tu mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume kuwaeleza wafuasi wake kwamba maelezo yaliyotolewa na mpinzani wake ni ahadi za njozi na ni danganya toto.

Msingi mkubwa wa hoja ya Karume ni kwamba ahadi hizo haziendani na misingi ya kiuchumi.

Hoja kubwa ya mgombea wa CCM ni kwamba haiwezekani kupunguza kodi kwa kiwango kikubwa na wakati huohuo ukapandisha matumizi kwa asilimia 100 bila ya kuwepo vyanzo vingine vya kodi. Taratibu za kiuchumi hazikubali hali hiyo.

Hoja hizo zimeanza kutawala mawazo ya wapiga kura wengi wa Zanzibar na kwa kiasi kikubwa zimeanza kuathiri fikra za wananchi ambapo kumekuwa na kutiliwa mashaka makubwa wa baadhi ya kauli zinazotolewa kwenye majukwaa ya kisiasa.

Ndani ya duru za kampeni zinavyoendelea, Mgombea Karume ameonekana kumpiku Mgombea Maalim Seif kwa taaluma ya uchumi, ambapo wafuasi wa mgombea huyo wa CCM wameanza kutangaza kwamba Maalim Seif hamuwezi Karume kwa mambo ya uchumi.

Athari iliyojitokeza kuhusisha na kauli za kutilia mashaka ni kuonekana kudhoofika kwa ngome ya upinzani hasa kisiwani Pemba.

Kudhoofika kwa ngome hiyo, kulijitokeza pale Maalim Seif alipofanya mikutano minne ya kampeni kisiwani Pemba, iliyohudhuriwa na wafuasi wachache kinyume na ilivyozoeleka huko nyuma.

Mikutano hiyo ilifanyika katika kijiji cha Konde, Ole, Mkanyageni na Ditia Wawi.

Katika mikutano hiyo kutokana na mahudhurio yake, mgombea huyo alishindwa hata kuwahutubia wafuasi wake zaidi ya kusimama kwenye jukwaa na kuwapungia mkono baada ya wapambe wake kufanya utambulisho.

Lililodhihirisha kwamba mahudhurio yamewafadhaisha viongozi wa CUF ni pale chama hicho kilipopangua ratiba yake ya kufanya mkutano mkubwa kwenye kiwanja kikubwa ilichokizoea cha Tibirizi na badala yake kuamua kufanya kiwanja kidogo cha Ditia Wawi ambapo hapo Maalim Seif alihutubia kwa dakika 10 tu.

Tathmini ya jumla ya kampeni inavyokwenda inaonekana kung’ara kwa mgombea wa CCM ikilinganishwa na mpinzani mwenzake. Hali hiyo imekuja kwa kufuatilia kwa karibu mikutano ya kampeni inavyokwenda ambapo CCM imebainika kujiongezea nguvu ndani ya ngome ya CUF.

Nguvu hizo zimeongezeka kutokana na baadhi ya wanachama wengi wa CUF kutangaza kujitoa katika chama hicho na kujiunga CCM.

Tukio la karibu ni lile lililofanyika kwenye mkutano wa kampeni wa CCM huko Kangagani katika jimbo la Ole na Pujini jimbo la Chonga ambako wanachama 149 wa CUF walikabidhiwa kadi za CCM na mgombea Karume.

Vitisho na vitendo vya vurugu vinavyosadikiwa kufanywa na wafuasi wa CUF vya kuwapiga mawe CCM wanapokuwa wakirejea kwenye mikutano ya kampeni na kuchanwa kwa picha za wagombea wa CCM, vimeelezwa kuwa ni dalili zinazoashiria CUF kukubali kushindwa.

Aidha, CUF kuanza kulalamika mapema kwenye nchi na jumuiya za kimatifa kwa kila hatua inayotekelezwa katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi, ni ushahidi wa chama hicho kutafuta hisani za kisiasa kutoka kwa taasisi hizo pale itakapofikia chama hicho kushindwa.

Pamoja na kukabidhiwa kadi kwa wanachama hao, fukuto la kutaka kumdhihirishia mgombea Hamad kwamba CUF sio mali yake pekee liko ndani ya wafuasi na wanachama wa Chama hicho na limekuwa likizungumzwa hadharani.

Nini wafuasi hao walichokusudia kukifanya katika uchaguzi mkuu huo, bado hakijafahamika wazi lakini hali inaonekana haiko shwari ndani ya chama hicho cha upinzani na haitoi matumaini yoyote ya ushindi kwa mgombea huyo wa CUF.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.