|
Sheria yaja kuzuia kazi ya siasa kufanywa vijiweni
2006-04-22 08:27:32
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa, amesema kwamba ofisi yake inaandaa sheria mpya ili kuhakikisha vyama vyote vya siasa havifanyi kazi za siasa vijiweni.
Bw. Tendwa alisema sheria hiyo ina lengo la kuimarisha utendaji wa vyama vya siasa katika kuimarisha mfumo wa vyama vingi nchini.
Alieleza kwamba vyama vingi vya siasa hivi sasa vinakabiliwa na tatizo la kutomudu gharama za kuendeshea ofisi na kulazimika kufanya shughuli za kisiasa katika vivuli vya miembe na bustani hasa Zanzibar.
Bw. Tendwa alisema sheria hiyo hivi sasa inaandaliwa kabla ya kupelekwa Bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa.
Tunaandaa sheria mpya ambayo itaondoa tatizo la vyama vya siasa kutokuwa na ofisi za kufanyia kazi na tutahakikisha kila chama kinakuwa na ofisi yake, alisema Bw. Tendwa.
Alieleza kwamba ili chama cha siasa kiweze kupata usajili lazima kiwe na sura ya muungano, hivyo chama chochote cha siasa lazima kiwe na ofisi za kudumu Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kwamba ofisi yake imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwa kila chama Zanzibar kuwa na ofisi, lakini vyama vyengine vinashindwa kutekeleza hilo kwa madai ya kukabiliwa na ukosefu wa fedha.
Tunapowatafuta kwa shughuli zetu tunawapata, lakini si vizuri kwa chama cha siasa kukosa ofisi na ndio maana tumeamua kuleta sheria itakayovibana vyama vyote kuwa na ofisi ya shughuli zao, alisem Bw. Tendwa.
Alisema kwamba baadhi ya vyama vimefungua ofisi katika nyumba za familia na kusababisha malalamiko kati yao.
Alieleza kwamba sheria hiyo pia itagusa mambo mbalimbali yatakayosaidia kuimarisha misingi ya demokrasia kwa kuweka mazingira yatayosaidia kuimarisha uhai wa vyama vya siasa.
Msajili huyo alisema hayo kufuatia vyama vingi vya siasa Zanzibar kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa ofisi na kulazimika kufanyakazi za kisiasa katika vijiwe vya kahawa, bustani na katika karakana za vifaa vya umeme.
|