|
Prisca ndiye Miss Utalii Pwani
2006-07-10 08:41:18
By Hussein Omar, Kibaha
Mrembo, Prisca Sulle, juzi aliibuka mshindi katika shindano la kumtafuta mrembo wa Miss Utalii mkoa wa Pwani lililofanyika katika ukumbi wa Kontena na kujipatia zawadi ya kompyuta mpya yenye thamani ya sh. 400,000.
Prisca alifanikiwa kuibuka mshindi baada ya kuwashinda warembo wengine nane aliokuwa akipambana nao katika shindano hilo ambapo, Lilian Urasa alifanikiwa kushika nafasi ya pili na kuondoka na kompyuta huku Aneth Nyamziga akikamata nafasi ya tatu.
Nafasi ya nne katika shindano hilo ilichukuliwa na Jesca Kikumbi ambaye pia alishinda Tuzo ya Mrembo Mwenye Kipaji katika shindano hilo na kuzawadiwa kompyuta mbili zenye thamani ya sh. 200,000 kila moja.
Shindano hilo lilipambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao ni pamoja na H.Baba ambaye alingara kwa kuwainua mashabiki waliofika ukumbini hapo, Sisi Tambala, Smart Girls, Spider na mwanadada Nyota Ndogo kutoka nchini Kenya.
Wakati huo huo mgeni rasmi katika shindano hilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Ishengoma aliwapongeza waandaaji wa shindano kwa kazi walioifanya na kuahidi kutoa ushirikiano na kamati hiyo kwa ajili ya mashindano ya taifa.
|