|
Matokeo Miss Kinondoni yazua balaa
2006-07-10 08:42:10
By Somoe Ng`itu
Mashabiki mbalimbali wa urembo nchini juzi usiku walizomea matokeo ya washindi wa shindano la kumtafuta mrembo wa Kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo Nadia Mohammed aliibuka mshindi na kujinyakulia gari aina ya Mitsubishi Lancer.
Aidha mshindi watano, Nadia Ahmed, aligoma kutoka mbele na kufanya Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tanzania, Albert Makoye kumuita kwa zaidi ya mara tatu na kuamua kuachana naye.
Nipashe ilimfuata mrembo huyo na kumuhoji ambapo alisema kuwa alistahili ushindi na aliposikia matokeo hakuamini na roho ilimuuma na kushindwa kupanda tena jukwaani.
Nilistahili kushinda leo ila nilivyosikia matokeo yanatangazwa sikuamini, roho imeniuma na ningeweza kudondoka jukwaani, alisema Nadia.
Kutokana na makelele ya mashabiki kuzidi, Mwenyekiti wa kamati ya Miss Kinondoni, Yusuph George, alipanda jukwaani na kusema kuwa hao ndio washindi wa shindano hilo na anawaomba watu waache kuzomea na kukubaliana na uamuzi wa majaji.
Mashabiki nawaomba mtulie, hata kama hupendi ni wewe na hawa ndio washindi wetu, alisema Yusuph na kuanza kutangaza majina ya warembo walioshika nafasi tatu za juu.
Mshindi wa pili katika shindano hilo lililofunga pazia katika mashindano ya kanda nchini alikuwa ni Wema Sepetu ambaye amezawadia kitita cha sh. 800,000 huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Sophia Kapama aliyeondoka na zawadi ya sh. 500,000.
Christabella Peter ambaye ni Miss Sinza alifanikiwa kuwa mshindi wanne na kupata sh. 300,000 huku pia akitunukiwa taji la ubunifu lililotolewa na Redds la kujipatia zawadi zenye thamani ya sh. 150,000.
Katika shindano hilo lililokuwa na mataji mengi madogo madogo warembo wa Sinza waliendelea kufanya vizuri ambapo Sophia tena alishinda taji la malkia wa Executive Solution na kujipatia zawadi sh. 250,000 na ajira ya mwaka mmoja katika kampuni hiyo.
Warembo wengine wanne walioshinda katika shindano hilo ni Wema aliyepewa sh. 200,000, Christabella alipata sh. 150,000, Nadia Ahmed na Vivian Silikwa kila mmoja amepatiwa sh. 100,000.
Taji la kipaji lilishikwa na Ngeu Jackson aliyepewa Dola za Kimarekani 200 huku Nadia Mohammed akiibuka tena kuwa Miss Photopoint Photogenic na kuzawadia sh. 100,000.
Warembo wengine waliofanikiwa kuingia katika hatua ya kumi bora walikuwa ni Yvonne Mashuda, Grace Gabriel, Ania Said, Tina Ambrose na Vivian Silikwa ambao kila mmoja alizawadiwa sh. 100,000 na wanne waliobakia walipewa kifuta jasho cha sh. 50,000 kila mmoja.
|