|
Jumuiya za kiraia na mchakato wa kuelekea jamii isiyo na rushwa
2006-08-28 08:40:24
Na JACKSON KALINDIMYA
Jumuia za Kiraia zaidi ya 100 toka mikoa mbalimbali zilishiriki katika Tamasha na Maonyesho ya Jumuiya za Kiraia na kuzungumzia mchakato wa asasi hizo kuelekea jamii isiyo na rushwa.
Asasi za kiraia zipatazo 100 toka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani hivi karibuni zilishiriki katika tamasha na maonyesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na asasi hizo, kwenye maeneo yao nchini ili kuionyesha jamii wanachokifanya katika kutoa michango yao muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi kwa ujumla.
Tamasha hilo kubwa la aina yake lenye kauli mbiu ya Jukumu la Jumuiya za Kiraia katika mchakato wa Kuelekea Kwenye Jamii isiyo na Rushwa, lilifanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili Agosti 17 – 18 mwaka huu, liliandaliwa na taasisi iitwayo The Foundation for Civil Society ya jijini Dar es salaam.
Washiriki wa tamasha hilo walipata fursa ya kuionyesha jamii kile wanachokifanya, kufahamiana, kujifunza miongoni mwao na kubadilishana ujuzi na uzoefu, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mijadala ya kuelimishana na kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kitaifa.
Majadiliano yaliyofanyika ni kuhusu jukumu la jumla la asasi za kiraia katika kupambana na rushwa na kuleta utawala bora katika ngazi zote za uongozi na ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa programu za uimarishaji wa sekta za afya na elimu, ufuatiliaji wa matumzi ya fedha za umma katika ngazi mbalimbali.
Mengine ni kuhusu ukusanyaji wa maoni ya wananchi juu ya mianya na viwango vya rushwa katika sekta na ngazi mbalimbali na nyinginezo.
Mwenyekiti wa Bodi ya The Foundation For Civil Society,Prof. Chris Maina akizungumza kabla ya mgeni rasmi kufungua tamasha hilo alisema kuwa jumuiya za kiraia zina wajibu mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuchangia juhudi za serikali za kutaka kutokomeza rushwa.
Tunaamini kuwa vita dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mtu mwenye mapenzi mema na ustawi wa Taifa letu alisisitiza.
Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein, akifungua tamasha hilo, alisema kuwa wananchi wanaoichukia na kuikataa rushwa kwa dhati, ndio nguzo kuu ya mafanikio katika mapambano hayo.
Na kwamba rushwa inaposhamiri inapunguza imani kwa wananchi katika mfumo wote wa siasa na demokrasia .
Hii ina maana kuwa juhudi za viongozi wa serikali peke yao na taasisi zake, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) haziwezi kuondoa tatizo hili sugu.Mafanikio yatapatikana, ikiwa watanzania sote tutakuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa.
Tutakaposhirikiana, tutaweza kupata mafanikio na kufikia azma yetu ya kuliondoa tatizo la rushwa katika nchi yetu alisema na kuendelea.
Jambo linalowafanya watu hao kuwa kero zaidi alisema kuwa ni kiburi,jeuri na dharau inayojengwa na watu wanaokumbatia rushwa ambao hawaogopi na hawajali kuwa vitendo vyao ni kinyume cha sheria, haki na dhamana zao, maadili binafsi na ya jamii na imani ya umma juu yao,
Mafanikio katika vita hii yanategemea ushirikiano baina yetu ukiimarishwa na nguvu za sheria, ushawishi wa kijamii, dhamira ya kisiasa na uimara wa maadili binafsi na ya jamii.
Ni matarajio kuwa asasi za kiraia zitalifanyia kazi hususan suala la ushawishi wa kijamii, kwa lengo la kuifanya jamii yetu ichukie na kuikataa rushwa isije ikakubalika na kuonekana kama ni jambo la kawaida katika maisha alisema na kuendelea
Asasi za kiraia hazitaweza kuwa chachu ya uimarishaji wa utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa, kama asasi zenyewe hazizingatii nguzo hii ya utawala bora na uwajibikaji katika uendeshaji wa shughuli zao.
Dhana ya uwazi, khususan kuhusu mapato na matumizi ya fedha ni jambo ambalo halitekelezwi na baadhi ya asasi za kiraia.Ushirikishwaji wananchi ni suala muhimu.
Haitoshi kuwaeleza wananchi juu ya miradi inayotekelezwa peke yake bila ya kuwashirikisha walengwa katika kupanga, kutekeleza miradi na kuwapa taarifa za mapato na matumizi yake alisema.
Aliipongeza Foundation for Civil Society kwa kazi yake nzuri ya kuzisaidia asasi, kuzipatia ruzuku na kuzijengea uwezo wa kuwawezesha wananchi kushiriki katika mipango ya kujiletea maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Bw John Ulanga alizitangaza asasi nne zilizofanya vyema katika maeneo yao na kukabidhiwa zawadi ya ngao na cheti na Dk Shein.
Asasi hizo ni Ruvuma Orphans Associaton, Bendi iitwayo Seven Band Blind ya jijini Dar es salaam, Lusunga Ward Dev Association(LUWADA) ya Mbeya na Umoja wa Wenye Ulemavu Zanzibar(UWZ).
Bi Salma Haji Sadat akizungumza kwa niaba ya UWZ ambao uliibuka kuwa mshindi wa kwanza na wa jumla wa asasi hizo, alisema wanajisikia vizuri kushiriki katika tamsha hilo kwa mara ya kwanza na kupata ushindi huo.
Ushindi wetu umetokana na hatua yetu ya kufundisha lugha ya alama kwa viziwi visiwani Zanzibar.
Kabla ya hapa viziwi hawakuwa wakipata mafunzo kama haya na hivyo kunyimwa fursa za kuwasiliana na watu wengine.
Sasa wamepiga hatua zaidi kwa kuanzisha chama chao na watu wengine pia kujifunza lugha hiyo.Kwa hakika kazi ya Foundation ni nzuri alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Lusungo (LUWADA) ambao walipata ushindi wa pili, Bi Lucia Mkandabile alisema,ni kutokana na utekelezaji wa sera, jinsia, utawala bora na ushauri nasaha katika eneo lao ambapo wanawake wameelimishwa kuhusu sheria, haki zao na namna ya kuzidai .
Maonyesho haya ni mazuri kwa sababu yanatukutanisha watu wa kutoka sehemu mbalimbali, kufahamiana na kupanga mikakati ya utekelezaji bora zaidi. Ukweli tunawapongeza sana The Foundation for Civil Society alisema Bi Lucia.
Mtafiti Msaidizi na |Mweka Hazina wa Mountain Conservation Society of Tanzania, alisema kuwa pamoja na jitihada zao za kutetea hifadhi ya milima na uchomaji moto misitu lakini serikali haijaitikia wito wao wa kuitangaza Desemba 11 ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Milima kama inavyoadhimishwa na mataifa mbalimbali.
Lengo ni jamii itambue umuhimu wa milima katika maisha.
Ni vyanzo vya maji, misitu, hifadhi ya wanyama na mengineyo.Watu wasipeleke madawa huko na kuharibu uoto huu wa asili alisema.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika yaisiyom ya Kiserikali(TANGO),Bi Mary Mwingira anaitazama rushwa kama ni tatizo la kimfumo.
Katika kuthibitisha hali halisi ilivyo anatolea mfano kati ya daktari na mtoza ushuru kuwa na tofauti kubwa ya mapato.
Daktaria na umuhimu mkubwa katika maisha lakini ameachwa nyuma na watu wengine ambao wanatofautiana taaluma.
Watoto wangu wawili ni madaktari, lakini sasa wanataka kuacha kazi ili waende kusomea kazi nyingine itakayowawzesha kufanya kazi kwenye taasisi za fedha alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi Helen Kijo-Bisimba anasema kuwa rushwa bado ni kikwazo katika jamii na inachangia kukosekana kwa haki.
Tatizo jingine aliliainisha kuwa ni Tanzania kukosa sheria ya kuwalinda watu wanaotoa taarifa za wala rushwa.
Watu wanaoishi vijijini wanajitolea kutoa taarifa za wala rushwa kwenye vyombo husika wanaonekana ni wachochezi na hakuna sheria ya kuwalinda ili wasibugudhiwe aliwaambia washiriki hao.
Mwakilishi wa Shirika la Kuzeeka ni Kukua, Bi Frida Chale alisema kuwa vita dhidi ya rushwa siyo ya kuifanyia mzaha.
kwa sababu ni vita inayomaliza nchi.
Msajili wa zamani wa vyama vya siasa nchini, Jaji George Liundi alisema kuwa mafanikio ya mapambano dhidi ya rushwa yatapatikana ikiwa watanzania wataweka shinikizo kama lile lililokuwepo kwenye siasa kuelekea mfumo wa vyama vingi.
Lengo la The Foundation for Civil Society ni kuimarisha uwezo wa jumuiya na asasi za kiraia kushiriki katika zoezi zima la kupunguza umasikini kama ilivyoelezwa katika sera za serikali ya Tanzania.
|