17 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Dar iige mipangilio ya usafi na usafiri wa Nairobi
 
2006-10-17 09:28:42
Na Gaudensia Mgumi

Dar es Salaam na Nairobi ni miji maarufu katika nchi zinazounda ushirikiano wa Afrika Mashariki ambazo zina mambo yanayofanana na kutofautiana ambayo yaliyo mazuri yakiigwa yatasaidia sana kuboresha maisha ya wananchi wake.

 Makala hii ya Mwandishi Wetu Gaudensia Mgumi aliye Nairobi yanachambua baadhi ya mambo katika miji hii. 

Katika jiji la Dar es salaam wakazi wengi wanategemea usafiri wao kwa mabasi yajulikanayo kwa jina la daladala wakati jijini Nairobi ni ’Matatu’.

Utozaji nauli Dar kwa kiasi fulani ni afadhali kwani kuna mkono wa serikali wa kudhibiti nauli. Nairobi mambo ni magumu. Karibu kila siku kuna nauli mpya na kila mmiliki  hupanga yake.

Utafiti usio rasmi umebainisha kuwa, wanaoishi karibu sana na Nairobi hutozwa  Sh. 20 ambayo ni sawa na kati ya Sh.300 - 400 za Tanzania.

Mambo hubadilika jioni  ambapo hufikia hata Sh. 40 sawa na Sh. 800 za hapa nchini. Shilingi moja ya Kenya hubadilishwa kwa kati ya Sh 18-20 za Tanzania .

Siku ambayo mvua ikinyesha ni balaa. Kama ni jioni nauli ya eneo la kilometa tatu kutoka Nairobi mjini hufikia Sh. 50 sawa na 1,000 na hali hubadilika kutegemeana na umbali kutoka jijini.  Si ’Matatu’ hata teksi nazo hali ni hiyo hiyo nauli huwa juu.

Lakini tofauti na Dar hali ya mpangilio wa mabasi ya matatu Nairobi inaridhisha. Kila abiria huketi katika kiti ( siti levo) pia lazima uvae mkanda wa usalama ile hali ya kuheshimiana sio kubanana kama mifugo.

Hapa Nairobi kuna utaratibu wa watu kupanga foleni ili wapande magari kwa utaratibu bila vurugu. Yawezekana utaratibu huu kwa kiasi fulani ukawa unapunguza uwezekano wa kuambukizana magonjwa ya hewa kama vile mafua na kupakana jasho kama ilivyo kwa daladala za jijini Dar es Salaam. Kuna baadhi ya ’Matatu’   kondakta ana siti yake na hakuna kukanyagana. Dar es salaam ni muhimu kujifunza toka huku.

Baadhi ya wafanyakazi wanaokaa nje ya jiji hulazimika kuanza safari ya kuja mjini kuanzia saa 11.30 alfajiri ili wawahi kazini kabla ya saa mbili asubuhi. Barabara zinazoongoza kwa foleni ni  Thika  na Ngong’. 

Usalama
Lugha inayotumiwa hapa ni ’chunga’ ’watch out’  watu ni wajanja si kama Dar es salaam, kosa dogo umeingizwa mjini. Ukikutana na mtu akikuambia nauza marashi muepuke sana maana ukinusa ili ufahamu harufu yake umevuta mihadarati.

Ukimuuliza mtu, nimepotea mtaa fulani nielekeze baadhi yao wanaweza kutumia mwanya huo kukuibia. Pengine njia bora ni kuuliza walinzi wa maofisi, Wahindi au Wazungu walioko kwenye biashara zao.

Kuna nyakati fulani uhalifu hupamba moto ambapo ’Matatu au daladala’ hutekwa mchana  kweupe au asubuhi na abiria huzungushwa mitaani chini ya mtutu wa bunduki na kupekuliwa hata sehemu za siri.

Wateka nyara au wakora, huwaamuru kuchomoa simu- kadi na  kusalimisha simu, pochi zao na kwa wanawake huamriwa kusalimisha mabegi  na kuyatosa ndani ya fuko kubwa la majambazi hao.

Mirungi.
Kwa Tanzania bangi ni haramu na pia  mirungi ni marufuku pia lakini kwa Kenya mirungi ni kama haina udhibiti mkubwa.

Ukipita kwenye mitaa ya miji na  vibanda pembeni ya barabara, utakuta majani mithili ya mboga yamefungwa kwenye majani ya migomba na kuning’inizwa  ukiuliza Hamad !  ni mirungi. Bei yake ni Sh. 600 kwa kilo sawa na Sh. 12,000 za Tanzania .

Mirungi inatafunwa usiku na mchana hakuna kulala wanaume hata baadhi ya wanawake. Mirungi ni kama inakubalika na kuchukuliwa kuwa ni halali.
 Kubeba miili ya marehemu na misafara ya mazishi.

Kama ukizunguka maeneo mbalimbali ya Dar kwa siku ni jambo la kawaida kabisa kuwa unaweza kukutana na misafara hata 50 hivi ya watu wakibeba marehemu wao kwenye pick-up, vipanya, daladala au hata wengine wakibeba majeneza mikononi kwenda kuzika.

Mambo haya Nairobi hayapo.Utaratibu wa aina hiyo ni kama haupo. Hukutani na misafara ya kubeba maiti wala pick-up zikiwa zimebeba majeneza .

Utaratibu uliopo ni kwamba kuna makampuni ya kushughulikia taratibu za mazishi pamoja na magari ya kubeba miili ya marehemu ambayo yamepakwa rangi nyeusi na si rahisi kuona kilichobebwa ndani.

Vyoo na usafi wa jiji

Nairobi ni jiji ambalo linaweza kuwa mfano wa kuigwa  hasa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki katika  kuimarisha usafi wa vyoo, tatizo ambalo linaikumba miji mingi ya Afrika.

Mwaka huu kuanzia mwezi Aprili huduma za vyoo vinavyohamishwa  au mobile toilets zilianzishwa.

Vyoo hivi vimewekwa katika mitaa mbalimbali na wanaopata huduma hiyo hulazimika kulipia gharama ya Sh. 10 sawa na Sh. 180 au 200  za Tanzania.

Kampuni binafsi  ndiyo inalofanya shughuli zote kuanzia kuhudumia wateja na  usiku kukusanya uchafu na kwenda kuutupa kwenye makaro ya taka za vyooni.

Maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya  Excloosive   inayotoa huduma hiyo Bw. Mosses Nderitu, aliyoyawasilisha Manispaa ya jiji akizungumzia  mradi huo, yasema kuwa sehemu ndogo tu iliyoko katikati ya jiji hili hupokea wageni karibu  700,000 kila siku, wakiwemo watalii, wafanyabiashara na wafanyakazi.

Wote hao hawana huduma za maliwato hatua inayowalazimisha kila mmoja kufikiri kuwa wakibanwa na watafanya nini? Kuna huduma za vyoo vya kulipia lakini si muafaka na havina hadhi ya kisasa, pengine ambayo wananchi wanatarajia na wageni wangependelea.

Anaendelea kufafanua kuwa,  watu zaidi ya milioni tatu wanaoishi Nairobi yasemekana watu milioni moja hawana vyoo na kulazimika kujisaidia haja ndogo na kubwa popote ikiwa ni pamoja na kutumia mifuko ya plastiki.

Anaongeza  kuwa vibanda hivyo vya choo vyenye  huduma zote kama maji na  karatasi za chooni vinawekwa sehemu maalumu zenye mahitaji kama vile kwenye viwanja vya michezo na mikutano , bustani za mapumziko, mikusanyiko ya kibiashara na wasafiri ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Vyoo hivi vina matanki maalumu ya kukusanya  uchafu, tangi hilo liko pamoja na la maji ambalo hufanya kazi ya kuvuta maji na kusafisha choo kuwa rahisi, uchafu hubakia kwenye  tangi la taka za vyooni, ambalo husafishwa baada ya kutumiwa na wastani wa wateja 250.

Vibanda vya vyoo hupendeza, vina maji ya kuvuta uchafu  na ya kunawa mikono tena vimeundwa kwa namna ambayo havisababishi kutoa harufu ya kinyesi na kusababisha uchafuzi wa mazingira.

Yawezekana halmashauri ya jiji la Dar wana mipango yao wanaoiamini kuwa inafaa kuondoa kero, lakini si jambo baya kuomba ’chumvi’ kwa jirani. Kama yanawezekana Nairobi pengine yanawezekana Dar.

Harufu mijini

Ukiwa Dar na ukabahatika kupitia Barabara ya Kivukoni iliko Tume ya Mipango na Ubinafsishaji ama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto unachokutana nacho cha kwanza ni harufu mbaya ya eneo la Feri.

Kinachonuka ni matumbo na mabaki ya samaki yanayokusanywa kutengeneza chakula cha mifugo. Harufu mbaya kama hizi hazipendezi si rahisi kukutana nazo Nairobi tena katikati ya jiji kama ilivyo hapo Kivukoni.

Kuwa na bahari si sababu tosha ya kufanya jiji linuke uchafu wa samaki kiasi hicho? Harufu mbaya yaidhalilisha  Dar . 

Vijiwe na ukosefu wa ajira
Maelfu ya watu Nairobi hawana kazi. Hukaa vijiweni nje ya majengo na  mahoteli ama kwenye bustani mjini tangu asubuhi mpaka jioni.

Kwa namna yoyote ile Dar ina mambo ya kujifunza toka Nairobi, kama ilivyo Nairobi kwa Dar.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.