|
POFIDESO:Yahamasisha Kawe kupiga vita umasikini
2006-10-18 08:58:33
Na BADRU KIMWAGA
Eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo ambayo kama yatachukua hatua za kuunganisha nguvu katika kukabili kero mbalimbali zikiwemo umasikini na mzigo wa yatima zaweza kupiga hatua kubwa ya kujiletea maendeleo.
Umaskini ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayokwamisha kusukuma mbele kasi ya maendeleo ya wananchi wengi hapa nchini.
Katika kujaribu kukabili hali hiyo,juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na watu mbalimbali.
Miongoni mwa hatua hizo ni kubuni mikakati ya namna ya kulikabili tatizo hilo ili kushinda vita vya umaskini na kuboresha maisha yao.
Chama cha Kupambana na Umaskini na Kuleta Maendeleo kwa Jamii (POFIDESO) kilichopo eneo la Kawe jijini Dar es salaam ni mojawapo ya vikundi vilivyo katika mchakato huo.
Kikundi hicho, kimekuwa kikishiriki katika vita vya kukabiliana na umasikini ili kuboresha maisha ya jamii.
Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha kuwa maisha yanaboreshwa kwa kuishirikisha na kuihamasisha jamii katika mikakati ya kupambana na umaskini.
Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Bi. Grace Assey, akizungumzia mkakati wa asasi hiyo anasema chama hicho kilichoanzishwa miaka mitatu iliyopita kimekuwa kikiandaa semina na makongamano kwa lengo la kuwawezesha wananchi kutambua tatizo la umaskini na hatimaye kubuni mikakati ya kupambana nao.
Semina hizo anasema pia zimekuwa zikitumika katika kuwaelimisha vijana na wanawake kuhusu uanzishwaji wa miradi ya uzalishaji mali.
Katika mkakati huo,Bi. Assey anasema POFIDE pia imekuwa ikiwaelimisha wananchi kwa kina kuhusu umuhimu wa kutunza na kulinda mazingira wanayoishi au yanayowazunguka.
Anasema hiyo inatokana na ukweli kwamba uharibifu wa mazingira unachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza tatizo la umaskini katika jamii.
Lengo ni kuamsha mwamko kwa jamii iweze kutambua na kuthamini hifadhi ya mazingira kwa ajili ya kuwa na maendeleo endelevu.
Lakini pia kikundi chetu kinajishughulisha na suala zima la kuielimisha jamii yetu kuhusu tatizo au janga na ugonjwa wa Ukimwi ambalo bado linaikabili jamii yetu na kuua nguvu kazi muhimu.Mtazamo wetu mwingine ni kuwasaidia watoto yatima ambao wanazidi kuongezeka siku hadi siku, anasema Bi Assey.
Kuhusu utafiti wa chama hicho, kwa mujibu wa Bi Assey anasema umebaini kuwa Kata ya Kawe ina watoto yatima zaidi ya 2,500 ambao wazazi wao wamekufa bada ya kuathiriwa na ugonjwa wa Ukimwi.
Hali hiyo imekuwa ikichangia kusababisha kuishi katika mazingira magumu na kwamba wanahitaji mno msaada wa jamii ili waweze kupata mahitaji ya msingi na ya lazima katika maisha yao.
Kwetu sisi, watoto hawa tumekuwa tukiwasaidia kwa kuwapatia elimu, malazi, mavazi na chakula.
Tumekuwa tukifanya hivyo kwa kutumia fedha za mfuko wetu na msaada kutoka kwa wahisani walioonyesha moyo wa kuguswa na tatizo hilo, anasema Bi Assey.
Anasema fedha zinazotunisha mfuko wao zinatoka katika mifuko yao binafsi au ya wahisani.
Miongoni mwa wahisani wanaotuunga mkono kwa hali na mali ni Foundation For Civil Society, Red Cross, GEMA na Carisians Hawa kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakitusaidia sana katika kuhakikisha kuwa tunatimiza malengo yetu ya kuhudumia wananchi ikiwa ni pamoja na yatima kuwawezesha kufanya shughuli zetu, anafafanua.
Anasema licha ya kuwa na mikakati mizuri ya kuchangia kuipunguzia jamii mzigo wa umasikini, hata hivyo ukosefu wa vitendea kazi umekuwa ni kikwazo kikubwa.
Vitendea kazi ambavyo vimekuwa tatizo kubwa kwao ni pamoja na vyombo vya usafiri ili kuwawezesha watendaji wa chama hicho kuwafikia walengwa walio katika maeneo ya vijiji vya kata ya Kawe.
Licha ya tatizo hilo, jingine ni wananchi kuwa na mwitikio wa kiwango cha chini katika matukio ya kujitolea na kushiriki kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi.
Baadhi ya watu ambao wana uwezo mkubwa kiuchumi katika Kata ya Kawe, nao wamekuwa wagumu kusaidia jitihada za kuwakomboa wale ambao wasiokuwa nacho.
Mratibu wa chama hicho, Bw. Shaaban Madega anaelezea kuguswa sana na tatizo la jamii kutohamasika na kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kujikomboa kiuchumi.
Wengi hawapendi kujitokeza na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo...Ukiwafuata wanapuuzia na matokeo yake ni kuendelea kuishi katika lindi la umaskini mkubwa, anasema.
Anasema utafiti wa chama hicho umeonyesha kuwa Kata ya Kawe ndiyo yenye idadi kubwa ya watu maskini katika wilaya ya Kinondoni.
Bw Madega anasema kuwa pamoja na jamii kuwa katika lindi la umaskini lakini watu hao ni kama hawataki kujishughulisha katika mapambano dhidi ya umaskini.
Alitoa wito kwa wananchi wa Kata hiyo kuamka na kushiriki katika vita dhidi ya umaskini ili kuboresha maisha yao na ya jamii kwa ujumla.
Kwa ujumla anashauri kuwa njia mzuri ya kufikia azma hiyo, ni watu kujiunga katika vikundi vitakavyorahisisha uwezekano wa kupata mikopo kwa ajili ya mitaji.
Tunaamini kama wataamua na kujipanga katika vikundi, tatizo la umaskini wanaweza wakaondokana nalo, anasema.
Kwa mujibu wa Bw Madega, umaskini katika kata hiyo, umechangia katika kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Maambukizi ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa vijana wa kata hii yamekuwa makubwa kwa sababu ya umaskini. Vijana hawana kazi na kwa hiyo wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vinavyochochea kasi ya maambukizi, anasema Mratibu huyo.
Kuhusu matarajio ya chama hicho, viongozi hao wanasema ni pamoja na kupanua wigo wa shughuli kutoka katika eneo la Kata ya Kawe hadi katika maeneo mengine ya wilaya ya Kinondoni.
Tumeshaanza kufungua matawi kadhaa katika mitaa ya Kawe na Mzimuni na lengo ni kusambaa katika Mkoa mzima wa Dar es Salaam,Bw. Madega alisema.
|