|
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Kwanini Nyerere alipinga mfumo wa serikali moja
2006-10-19 08:59:41
Na GEORGE JOHN
Ni miaka saba sasa imepita tangu kutokea kwa kifo cha muasisi wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Ni ukweli ulio wazi kuwa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ni jina lenye historia ndefu na ambalo halitafutika katika vitabu vinavyoeleza chimbuko la uhuru wa Tanzania.
Sio lengo la makala hii kueleza kila zuri alilofanya Mwalimu J.K Nyerere wakati wa uhai wake. Yapo mengi lakini moja la muhimu kati ya hayo ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Taifa la Tanzania.
Hata hivyo, wakati mchango wake kwa ajili ya umoja huo unakumbukwa, kumekuwa na hoja inayoibuka na kuzimika na kuibuka tena kwamba ni vipi hadi leo hii Tanzania ina sura ya serikali mbili ya Jamhuri ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar, baada ya muungano uliohitimishwa Aprili 26 mwaka 1964.
Watu mbalimbali kwa vipindi tofauti, wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu muungano, baadhi wakiwa na mtazamo hasi kuhusu muungano huo. Wanataka urekebishwe ili kila upande uwe na mambo yake ambayo sio ya muungano.
Mtazamo wa baadhi ya vyama vya siasa, hasa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, suala la muungano limechukuliwa kama sera ya vyama husika, msisitizo ukiwa ni kudai sura mpya ya muungano huo.
Baadhi ya wenye madai hayo wanasema chini ya muundo wa sasa wa muungano, Tanzania Bara inaathirika kwa kuibeba Tanzania Visiwani katika nyanja nyingi tofauti za kiuchumi.
Pia wapo wanaoamini Tanzania Visiwani ni muathirika mkuu wa mfumo huu wa muungano, wakisema Zanzibar inakosa sauti katika maeneo mbalimbali yanayowagusa watu wake na pengine utamaduni wake.
Mwaka jana, Mohamed Raza, mmoja wa makada maarufu wa CCM aliibuka na maoni ya kutetea kuwepo kwa serikali ya Tanganyika, akisema muungano wa sasa unainufaisha zaidi Tanzania Bara kuliko Zanzibar.
Kwa maoni yake, makubaliano ya waasisi wa chombo hicho yalizingatia usawa wa Tanganyika na Zanzibar katika umoja huo, lakini tofauti na matarajio hayo Zanzibar imenyimwa sauti katika maeneo mengi yanayogusa maslahi ya watu wake.
Mfano wa hali hiyo uliotajwa na Bw. Raza ni Zanzibar kutopata nafasi ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kama nchi.
Mzee Anderson Basil Momburi (76) mkazi wa Chamwino Dodoma anasema suala la muungano kupatiwa sura ya serikali tatu si suluhisho la matatizo yanayojitokeza katika muungano.
Anasema mwalimu Nyerere alikuwa na upeo wa kuona mbali na alipenda kuona watu wake wakiwa katika umoja si tu kwa Tanzania, bali hata Afrika nzima. Hii ndio maana aliamua kushirikiana na marehemu Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar, kuanzisha muungano huo.
Katika hatua inayoonyesha jinsi muungano unavyothaminiwa, Bw. Momburi anasema ni muhimu kwa Watanzania kuepukana na hatua yeyote inayotishia uhai wa muungano kwa sasa.
Katika baadhi ya maoni yake, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hatua yoyote inayotishia muungano ni kama dhambi ambayo kama itaruhusiwa kutendwa itazidi kuleta madhara zaidi kwa pande zote kuliko manufaa yanayotarajiwa.
Kelele za kutaka serikali tatu sio tu kuwa ni kinyume na sera za chama kinachotawala sasa cha CCM bali pia ni kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano, anasisitiza bw. Momburi.
Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, eneo linalohusu utekelezaji wa shughuli za mamlaka ya utendaji vitakuwa ni serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kwa sababu za kiuchumi, isingefaa kwa Watanzania kubeza muungano wao kwani hata nchi za Ulaya, zinaimarisha umoja wao kwa manufaa ya maendeleo ya uchumi kama vile kuunganisha sarafu.
Nini kifanyike kuunganisha mitazamo tofauti juu ya Muungano?
Kama kweli yamejitokeza matatizo ya msingi katika Muungano huu, ni muhimu kutafuta namna ya kuziondoa kero hizo na kuuboresha zaidi bila hata kuwa na serikali tatu, hatua ambayo ni sawa na kurejea nyuma.
Mwalimu Nyerere, enzi za uhai wake aliwahi kusema kuwa utaratibu wa kuwa na mfumo wa serikali mbili, badala ya tatu, ulifikiwa baada ya kutazama hali halisi ya nchi zetu zinazoungana na sababu ya kuungana.
Katika kitabu chake, Uongozi wetu na hatima ya Tanzania, Mwalimu Nyerere anazungumzia mengi lakini sehemu ya hoja yake kuhusu muungano inasema: Nchi mbili zinapoungana na kuwa nchi moja, mifumo ya kawaida ya miundo ya katiba ni miwili.
Muungano wa serikali moja au shirikisho la serikali moja au shirikisho la serikali tatu. Kwa mfumo wa kwanza, kila nchi itafuta serikali yake na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja.
Katika mfumo wa pili, kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.
Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.
Nchi za Afrika Mashariki, zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa ni nchi tatu zilizioungana kuwa nchi moja yenye muundo wa shirikisho.
Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana na kuzaa nchi moja mpya.
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa nchi moja, tungeweza kufuata mojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika.
Zanzibar ilikuwa ina watu laki tatu na Tanganyika watu milioni 12. Kutokana na hali hiyo, muungano wa serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar.
Tulikuwa tunapigania uhuru na umoja wa Afrika, hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!
Kwahiyo mimi nilipinga mfumo wa serikali moja. Shirikisho la serikali tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha serikali yake na kuchangia gharama kuendesha serikali ya shirikisho na Tanganyika ingefanya hivyo hivyo.
Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Watanganyika ndio hasa ungeendesha serikali ya shirikisho.
Kwahiyo Tanganyika ingeendesha serikali yake ya watu milioni 12 na pia ndio ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha serikali ya shirikisho la watu milioni kumi na mbili na laki tatu.
Kwahiyo ilitupasa tujiulize kwanini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo na hasa kwanini tunataka serikali ya Tanganyika?
Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar?
Hofu yetu ni kwamba tukiwa na serikali moja, Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar?
Basi tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha serikali mbili zenye uzito unaolingana na ndipo tukazaa muungano wa aina yetu.
Maneno hayo ya baba wa Taifa yanajitosheleza na ni wakati wa Watanzania wote kumuenzi kwa kuhakikisha Muungano wetu hautiwi doa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi. Tukumbuke wosia wa baba!
|