20 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Lowassa ahuzunishwa na maendeleo ya Tanga
 
2006-10-20 10:06:23
Na Lulu George

Akiwa na timu ya watendaji wake, Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa, alitumia siku saba kukagua shughuli za maendeleo mkoani Tanga. Hata hivyo, alisikitishwa na hali duni ya maendeleo licha ya mkoa huo kuwa na fursa nyingi za kiuchumi. Mwandishi Lulu George wa Shirika la Habari PST Tanga aliyefuatana na kiongozi huyo anaelezea zaidi katika makala haya.


Ingawa serikali ilibuni na kuanza kutekeleza Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) lakini kwa mkoa wa Tanga mpango huo bado ni kitendawili kwa sababu wakazi wake hawajaufahamu vizuri na badala yake wamekuwa wakiusikia kupitia vyombo vya habari.

Katika ziara yake ya siku saba mkoani Tanga, Waziri Mkuu, Bw.Edward Lowassa kuhimiza maendeleo, alionyesha masikitiko kuhusu jinsi alivyojionea mkoa huo ulivyokuwa umerudi nyuma kimaendeleo. 

Akizungumza wakati wa majumuisho ziara hiyo, Bw.Lowassa, anasema kwa ujumla katika wilaya zote alizotembelea amebaini kuwa mkoa unakabiliwa na tatizo la utendaji mbovu wa viongozi.

 Anasema viongozi wanatumia muda mwingi kwa kukaa maofisini badala ya kutoka na kwenda kwa wananchi kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwa mifano bora kwa wanajamii kwa niaba ya serikali yao.

 Bw.Lowassa, anasema viongozi pekee ndio dira ya maendeleo katika maeneo yao iwapo tu watayatumia madaraka yao vizuri, katika utendaji kwa kuwahamasisha wananchi wajue nini wanatakiwa kufanya ili kukabiliana na hali duni ya maisha waliyonayo.

’’Nimetembea katika wilaya zote za mkoa wa Tanga, lakini nilichobaini ni kuwa viongozi wameweka siasa mbele kuliko utendaji, na hii ni ishara mbaya za kuzorotesha maendeleo ya mkoa huu...ndugu zangu nawaomba muache kukaa maofisini mtoke muende kwa wananchi na muwape mikakati ya kimaendeleo’’,anasisistiza Bw.Lowassa.

Akiongelea kuhusu kilimo mkoani humo, Waziri Mkuu anasema sekta hiyo ndiyo inaongoza kwa kuzorotesha maendeleo ya mkoa kwani asilimia 90 ya wakulima wanatumia jembe la mkono ambalo halitaweza kamwe kuwakwamua kutoka katika wimbi la umaskini.

Akasema jitihada za makusudi za vongozi na wataalamu zinahitajika kuwawezesha wakulima kutumia wanyamakazi, matrekta pamoja na pembejeo za kilimo ili kuongeza tija.

Akasema serikali inatambua umuhimu wa kukuza na kuboresha kilimo kwa Mtanzania, kwani ndio tegemeo la pato la taifa na kwamba imeongeza bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka Sh. Bilioni saba mwaka jana hadi kufikia Sh.Bilioni 21 mwaka huu.

 Bw Lowasa anasema wananchi iwapo watahamasishwa vizuri wataweza kujiunga na Vyama vya Ushirika, ili kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao na kuwa wajasiriamali wa kilimo, na kwamba zaidi ya Sh. Bilioni 22 zimetengwa kwa kutoa mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali.

 Bw.Lowassa anasema hayo yote yanaweza kufanikiwa na hivyo kuiwezesha serikali ya awamu ya Nne kutimiza ahadi waliyoitoa kwa wananchi kwenye Ilani ya Uchaguzi mwaka jana ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.

Anasema hali ya kiuchumi mkoa wa Tanga inasikitisha kwani mpaka hivi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya Vyama vya Kuweka na Kukopa ( SACCOS) hivyo ambapo una vyama 69 tu.  

’’Nimezunguka mikoa kama Iringa hali ni nzuri lakini Tanga imenisikitisha .....yaani mkoa mzima mna SACCOS 69 tu...mnanisiskitisha…ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania sidhani kama kwa mkoa huu itatimia kutokana na hali hii...,’’alihoji Waziri Mkuu.

  Kuhusu elimu, Bw Lowassa alikerwa alipobaini kuwa asilimia 60 tu ya watoto wanaoandikishwa shuleni ndio wanaomaliza darsa la saba.

Watoto asilimia 40 huishia njiani kwa sababu mbalimbali zikiwa ni pamoja na watoto wa kike kupata ujauzito au kuozeshwa.

 Pia alielezwa kuwa nusu ya kesi zinazoripotiwa mahakamani kuhusu kuozesha wanafunzi au kuwapa ujauzito wasichana humalizwa nje ya mahakama ambapo ni kinyume na utaratibu.

’’Suala la kumpa mimba mwanafunzi sio la kulimalizia nyumbani....nawaomba sana viongozi mlisimamie hili hasa maafiasa elimu...mzazi akificha kwamba nani kampa mimba mtoto wake basi akamatwe yeye na awekwe ndani.. ’’anasema.

 Afisa mipango sekretarieti ya mkoa Bw.Rashid Luchele anaelekea kukubaliana na kilio cha Waziri Lowassa kwa kuelezea fursa za mendeleo zilizoko katika mkoa huo na hali ya kiuchumi.

Anasema mkoa wa Tanga una wakazi wapatao 1,752,312 kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu wa 2006 na kwamba wastani wa pato la mwananchi ni Sh 165. 576 kwa mwaka yaani chini ya dola moja kwa siku.

 Alisema mkoa wa Tanga una fursa nyingi za maendeleo ikiwamo ardhi ya kutosha yenye rutuba, mtandao wa barabara na reli , uwanja wa ndege, bandari, mwasiliano ya simu, maji na umeme.

Bw Luchele anasema mkoa hutegemea kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda pamoja na shughuli za biashara na utoaji huduma. Pia mkoa una rasilimali za bahari, misitu,wanyama pori, madini ya aina mbalimbali, vivutio vya utalii.

Licha ya kuwapo kwa fursa zote hizo za kuweza kuinua mkoa huo kiuchumi lakini bado wananchi wa Tanga wanakabiliwa na umaskini mkubwa wa kipato .

Bado kuna uzalishaji duni katika shughuli za kilimo,ufugaji na uvuvi na kwamba pato la mkoa kwa mwaka 2000 lilikuwa Sh milioni 281,873 ambapo pato la mkazi lilikuwa wastani wa Sh. 165,576 kwa mwaka.

 Ingawa mkoa una mazao muhimu ya chakula kama mahindi, muhogo, viazi, ndizi, maharage, mpunga,mboga, na matunda lakini kwa kipindi cha mwaka2000 hadi 2005 mkoa haukuweza kujitosheleza kwa chakula na ulilazimika kupata msaada wa chakula kutoka serikalini.

Ziara ya Waziri Mkuu ya siku saba iliyokuwa na lengo la kukagua shughuli za maendeleo ya mkoa wa Tanga ,iliwahusisha viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Waziri wa Mali asili pamoja na Utalii.

Wengine ni Naibu Waziri wa Miundo Mbinu na Mafunzo ya Ufundi Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii pamoja na wabunge wote wa mkoa wa Tanga.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.