21 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ndoa za lazima, zinavyohatarisha maisha ya watoto
 
2006-10-21 08:48:13
Na JOSEPH SHAYO

Mila za baadhi ya makabila kuwalazimisha watoto wa kike kuolewa, zimeanza kuathiri maisha ya watoto hasa wanaokataa kuingizwa katika mfumo huo.

Miezi kadhaa iliyopita, msichana mmoja tena mdogo kwa umri, aliuawa huko Saitosambu wilayani Ngorongoro kufuatia kitendo chake cha ushujaa cha kukataa kuolewa.

Tukio hilo, limewagusa watu wa kada mbali mbali na baadhi yao wamediriki kwenda katika kijiji cha marehemu angalau kujua kiini hasa cha tukio hilo.

Siku kadhaa zilizopita, kundi la zaidi ya walimu na wanafunzi 100 wa Shule za Msingi na za Sekondari za jijini Dar es Salaam , liliwasili katika kijiji cha Soitasambu wilayani Ngorongoro likiwa na shauku ya kubwa ya kutaka kujua kiini cha mauaji ya kikatili ya msichana Sooi Ole Sadira (13).

Kama umri wake unavyojionyesha, huyu alikuwa ni msichana mdogo ambaye watu wameamua kumuua kwa sababu tu ya msimamo wake thabiti ulioambatana na ushujaa wa kupinga kulazimishwa kuolewa.

Ni msichana ambaye hakuamini kama mila ya kumlazimisha kuolewa akiwa bado mdogo, ingemsaidia.

Mauaji dhidi yake yalikuwa ni ya kikatili mno na ndiyo maana yamekuwa yakimgusa kila anayepata kusikia namna alivyouawa.

Kundi la walimu na wanafunzi wa baadhi ya shule za Darc es Salaam ni miongoni mwa hao na kwa bahati wao waliamua kufanya uamuzi wa kwenda katika kijiji cha marehemu.

Safari yao katika kijiji hicho, ilitokana na maamuzi yaliyofanywa na Chama cha Walimu cha Kuwahudumia Wanafunzi wanaoishi katika Mazingira Magumu (EASSO).

Chama hicho kilifikia uamuzi wa kupeleka ujumbe wake katika kijiji cha Saitosambu ili kuelezea kusikitishwa kwake kuhusu mauaji hayo.

Lakini kwa bahati mzuri, tukio hilo lilikuja wakati dunia ikiwa inaadhimisha Siku ya Amani Duniani na kwa hiyo chama hicho, kilililitumia (tukio) kuwa ni sehemu ya maadhimisho.

Pamoja na mambo mengine, ukiwa katika kijiji cha Saitosambu, ujumbe wa wanafunzi na walimu, uliendesha tamasha maalum la kumkumbuka Sooi Ole Sadira na kulaani vikali mauaji dhidi yake.

Katibu Mkuu wa EASSO-TAN Bw, Mosses Mnyanzi, anasema tamasha hilo lililofadhiliwa na Benki ya Microfinance, lililenga katika kuhimiza umuhimu wa jamii kudumisha amani na upendo.

”Na katika mazingira haya ya kijiji cha Saitosambu, tunahimiza hali hiyo miongoni mwa watu wa jamii ya wamasai,” anasema Bw Mnyanzi.

Anasema pamoja na kuhimiza amani na upendo, tamasha hilo pia lilikuwa ni la kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki za watoto.

”Haki za watoto ni lazima zilindwe tena bila kujali jinsia zao,” anasema Bw Mnyanzi.

Katibu huyo wa EASSO anasema wazazi pia wanawajibu wa kuwapa watoto malezi sahihi yanayoambatana na kuepuka adhabu zisizostahili kwa watoto.

”Tumebaini kuwa jamii ya Wamasai ni miongoni mwa zile ambazo zimekuwa zikiwabagua kijinsia watoto...Watoto wa kike hawapewi umuhimu katika kusoma na badala yake wanawaozeshwa tena katika umri mdogo ili tu wazazi wapate mahari ya ng’ombe,” anasema.

Bw Mnyanzi anasema kuna haja ya kuchukua hatua za kujaribu kubadili mtazamo huo potofu katika jamii ya Wamasai ili iweze kwenda sambamba na mazingira halisi yanayotokana na mabadiliko ya dunia.

”Hapa napenda nimuunge mkono tena kwa dhati Mbunge wa Ukerewe Balozi Getrude Mongella aliposema ” Elimu kwanza , ngoma hata ukubwani utacheza…Wamasai wapelekeni watoto wa kike shule kwanza, ng’ombe wa mahari hata ukubwani mtapata tu, tena walionona zaidi” alisema Bw. Mnyanzi.

Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Bw Jowika Kasunga, anasema mauaji dhidi ya Sooi yamemtisha sana.

”Nimekuwa nikijuliza kwamba nitaishi vipi na Wamasai wenye roho mbaya kiasi hicho. Wanamuua mtoto mdogo kwa sababu tu ya kukataa kwake kuozeshwa kwa nguvu,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Bw Kasunga ambaye alikuwa akizungumza kupitia kwa mkalimani, aliwataka watu wa jamii ya Wamasai wabadilike na kuachana kabisa na fikra na mila potofu.

Alisema ng’ombe ni mali na akiba yao lakini mali hizo hazitakuwa na maana kama hawatakuwa watu wa jamii hiyo hawatakuwa tayari kuuza sehemu ya ng’ombe au mbuzi na kugharimia masomo ya watoto wao.

”Somesheni watoto wenu wenye asili ya ng’ombe ili waziendeleze, msipowasomesha ng’ombe wataisha na mtakuja nikumbuka: alisema Bw Kasunga.

Alisema elimu itawasaidia watoto hao kuwa huru kuwasiliana na kushirikiana na watoto wengine katika kulinda ardhi yao kwa ajili ya malisho.

Katika tamasha lao, wanafunzi waliimba nyimbo, kusoma ngonjera mashairi na michezo ya kuigizwa iliyoolezea uovu wanaofanyiwa watoto hasa wa kike.

Tumbuizo hizo zilifanywa kwa ushirikiano wa wanafunzi wa Shule za Dar es Salaam na zile za Ngorongoro.

Wimbo ulioimbwa kwa lugha ya Kimasai ambao uliimbwa na wanafunzi wa Shule ya Emanyatta uliibua simazi kubwa.

Watu wa jamii hiyo na hasa wanawake, walionekana wamelengwa lengwa na machozi machoni.

”Roho iliyopotea haitarudi tena”, hayo yalikuwa ni baadhi ya maneno yaliyosikika katika wimbo huo uliowataka Wamasai kubadili mtindo wa kuwalazimisha watoto kuolewa.

Wasichana watatu wadogo kutoka Shule ya Msingi ya Ruvuma wilayani Temeke waliutia umati simanzi waliposoma shairi lao kumkumbuka marehemu Sooi.

”Tuombeane amani dunia nzima unyanyapaa tuupige vita tutoe haki kwa watoto wote bila kujali jinsia”. ilisikika sehemu ya shairi hilo.

Shule za Msingi za Jiji la Dar es Salaam, zilizoshiriki katika msafara huo na idadai ya wanafunzi zikiwa katika mabano ni Ali Hassan Mwinyi (21), Charambe (1) Mtoni (1), Ruvuma (5), Lumumba (12, Ubungo NHC (3), na Kisutu (18).

Kwa upande wa Shule za sekondari ni Makongo (9), Agape (7) Juhudi (2), Azania (6) na St. Anthony (5).

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.