|
Wanamichezo wajitokeze kuwania uongozi TOC
2006-10-21 08:48:52
Na Mhariri
Kamati ya Olimpiki nchini (TOC) inatazamiwa kufanya uchaguzi wake mkuu unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa michezo mwezi Desemba, mwaka huu.
Uchaguzi huu unatazamiwa kuwa fursa nyingine kwa viongozi wa vyama vya michezo kutoa dhamana ya uongozi wa TOC kwa watu wenye sifa za kuongoza taaasisi hiyo.
Hiyo pia itakuwa nafasi kwa viongozi wa vyama vya michezo kupima mafanikio ya uongozi wa sasa ulio chini ya Gulam Abdalla.
Gulam alichukua nafasi hiyo miaka minne iliyopita kufuatia kungatuka kwa Raphael Kubaga aliyeongoza TOC toka mwaka 1974.
Hata hivyo, mafanikio makubwa zaidi ya TOC yamekuwa mwaka 1980 wakati Tanzania ilipopata medali mbili za fedha katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika nchini Urusi.
Toka wakati huyo Tanzania imekuwa watalii wanaoshiriki katika michezo na baadae kurejea nyumbani mikono mitupu.
Na mara timu inaporejea basi imekuwa ni kawaida kurudi na visingizio kibao na viongozi kulaumiana kutokana na wanamichezo wetu kufanya vibaya.
Tatizo kubwa zaidi kwa TOC, imekuwa ikikaa mbali na kufuatilia maandalizi ya wanamichezo wetu kila mara baada ya Olimpiki kumalizika.
Imekuwa ikidai jukumu la kuandaa timu ni la vyama vya michezo na sio kamati, ambayo ni makosa makubwa.
TOC ambacho zaidi imekuwa ikifanya ni kuandaa safari za timu zetu kushiriki bila kujali kama wanamichezo wetu wameandaliwa ipasavyo.
Sasa ni mategemeo yetu kuwa wanamichezo wengi wenye uwezo watajitokeza kugombea uongozi wa TOC ili kuweza kutengeneza mikakati mizuri ya kuwezesha taifa kufanya vizuri katika michezo mikubwa ya kimataifa.
Sasa changamoto kubwa iliyoko ni kuandaa timu kwa ajili ya michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na ile ya Afrika.
Uongozi wa sasa umeweza kupimwa baada ya michezo ya Olimpiki iliyofanyika Athens, Ugiriki, ambapo Tanzania ilirejea mikono mitupu na ile ya Jumuiya ya Madola, ambako ilipata medali ya dhahabu.
Changamoto kwa TOC ni kufanya kazi kwa karibu na vyama vya michezo ili kuweza kupanga mikakati ya muda mrefu na mfupi ili kuondoa aibu ya Tanzania ya kufanya vibaya kwenye michezo ya kimataifa.
Tunatoa wito sasa kwa wanamichezo mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi wa TOC ili kutoa uwanja mpana zaidi kwa wajumbe waweze kupata viongozi wanaofaa kuongoza kamati hiyo.
|