23 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mwanga yaanzisha chuo cha ualimu kukabili mahitaji ya walimu
 
2006-10-23 09:02:00
Na VICTOR KWAYU

Wakati serikali inafanya juhudi kubwa ya kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inapiga hatua ikiwa pamoja na kuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji ya elimu kwa sasa, taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Kalua Development Trust Fund(KDTF) ya wilayani Mwanga imeanzisha chuo cha ualimu kiitwacho Green Bird TTC na shule ya sekondari ya wasichana iitwayo Green Birds kwa madhumuni hayohayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya KDFT, BW. HABIB MNDEME anafafanua zaidi kama alivyohojiwa.

SWALI:Umuhimu wa elimu katika zama hizi ni mkubwa sana, ili kuhakikisha kuwa taifa linachukuana vyema na mazingira yaliyopo ikiwa pamoja na utandawazi.

Ukiwa mtanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kalua Trust Fund wilayani Mwanga, hatua zipi mmechukua katika kuhakikisha kuwa suala la elimu linapewa uzito unaostahili katika wilaya hii?

JIBU: Mkoa wa Kilimanjaro unakadiriwa kuwa na shule za sekondari zipatazo 256,Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro ina shule za sekondari 32.Hata hivyo kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa elimu bora Kalua Trust Fund iliamua kuanzisha shule ya sekondari ya wasichana iitwayo Green Birds High School ambayo inalenga kuhakikisha kuwa wasichana toka maeneo mbalimbali ya nchi yetu, sio Mwanga peke yake wanapata elimu bora katika mazingira bora ya usomaji na kuwandaa kuwa wataalamu wa fani mbalimbali.

Kama hiyo haitoshi, pia tulianzisha Chuo cha Ualimu Green Birds wilayani hapa.Hiki ni chuo pekee cha ualimu katika wilaya hii. Kabla ya hapo, wilaya haikuwa na chuo cha ualimu hata kimoja.

Kilianzishwa miaka michache iliyopita na kilifunguliwa rasmi kwa mafunzo Februari 1 mwaka 2006 kikiwa na wanachuo 34 na hadi kufikia sasa jumla ya wanachuo 282 ambapo kati ya wanachuo 215 ni wanawake na wanaume ni 67 wanaochukua mafunzo ya hatua ya kwanza ya ufundishaji (Grade A).

SWALI:Kwa nini mliamua kuanzisha Chuo cha ualimu katika wilaya hii?

JIBU:Mahitaji ya walimu bora, yaani walioivishwa vyema kimafunzo katika taifa letu ni makubwa sana kwa sasa, ambapo serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa tunakuwa na walimu wa kutosha kukabiliana na mahitaji hayo.

Uamuzi wetu wa kuanzisha chuo cha ualimu ni sehemu ya jitihada zetu za kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali kupunguza mahitaji hayo na kuhakikisha kuwa watoto wetu wanafundishwa na walimu bora na si bora walimu.

Lengo letu ni wilaya hii kupata maendeleo ya uhakika kwa kutumia raslimali watu. Kuwa na chuo cha ualimu katika wilaya hii ni kutoa fursa ya kukaribisha watu toka sehemu mbalimbali za nchi yetu ili waweze kuelimika na kujifunza sio mafunzo ya darasani tu ni pamoja na mazingira na kuangalia fursa zilizopo ambazio wanaweza kuzitumia wao wenyewe au kuzitangaza katika maeneo yao na hata kuchangia kuleta kasi ya maendeleo.

Kwa kuwa na chuo hiki, sasa wilaya yetu ya Mwanga ipo katika ramani ya elimu ya miji yenye vyuo vya elimu hapa nchini .

Kimsingi uamuzi wa kuanzishaa chuo cha ualimu katika wilaya hii ulizingayua ukweli kuwa yale ambayo yanaweza kufanyika katika upatikanaji elimu katika mazingira mengine pia yanawezekana kupatikana Mwanga na ndivyo tunavyofanya kuwa na chuo ambacho wanafunzi wanaohitimu hapa wanapoajiriwa wadhihirishe kweli kuwa wameiva na kutoa michango yao ya ufundishaji kikamilifu.

Kwa hiyo, jitihada yetu kubwa ambayo tumekuwa tukiiboresha kila siku na mara kwa mara ni kuwa na walimu waliohitimu vyema ufundishaji wa walimu katika fani zao, ikiwa pamoja na vifaa hasa vinavyokidhi mahitaji ya zama hizi. Ukibahatika kutembelea madarasa yetu, maabara yetu iliyoshehenezwa vifaa mbalimbali vya majaribio ya vitendo na kompyuta utaona ni kwa kiasi gani kweli tumepania Mwanga kuwa kitovu cha elimu.

SWALI:Wakazi wa wilaya hii ya Mwanga wanafaidikaje na kuwepo kwa chuo chenu na shule wilayani hapa?

JIBU:Kwa jumla faida zipo nyingi. Miongoni mwa faida hizo, ni kwamba wanafunzi wanaohitimu shule za msingi wanapata fursa za kuendelea na elimu ya sekondari na wanaohitimu katika shule za sekondari ambao wanapenda na wana sifa bora za kuwa walimu wanapata fursa za kuendelea na mafunzo.

Halikadhalika wakazi wa wilaya hii, wanapata fursa ya kuajiriwa katika shule na chuo hicho na hivyo kushiriki kwa vitendo katika kupiga vita umaskini.

Chuo na shule navyo vinalipa kodi serikalini na katika halmashauri ya wilaya kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jumla.

Pia tumejiwekea utaratibu wa kuichangia halmashauri ya wilaya sh milioni tano kila mwaka kwa ajili ya kusukuma kasi ya maendeleo. Mtazamo wetu ni kuhakikisha kuwa raslimali zinazopatikana katika wilaya hii, zinatumika kuwanufaisha na kuwaendeleza watu wa wilaya hii na mkoa wetu kwa ujumla.

SWALI:Katika kuhakikisha kuwa Chuo kinatumia fursa zilizopo kwa manufaa ya watu wengi zaidi licha ya wanafunzi waliopo, je kuna mkakati wowote wa kuishirikisha jamii kutumia fursa hizo?

JIBU: mipango ya chuo chetu ni kuhakikisha kinafungua milango yake iweze kutumiwa na wananchi katika masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwemo upatikanaji na utoaji elimu za vipindi vifupi vifupi na taasisi mbali mbali nchini katika kuendeleza elimu na ualimu kwa ujumla.

Milango iko wazi kwa taasisi mbalimbali za kielimu kutumia fursa zilizopo kama vile Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinaweza kuyatumia majengo na hali njema ya mazingira ya hapa kuwa kituo chao katika kuhakikisha kuwa kinafanikisha suala la elimu kwa wanafunzi wao.

Matarajio yetu ni kuendelea kukiboresha chuo hiki hatua kwa hatua, hadi kinafikia ngaazi ya kuwa Chuo Kikuu katika kipindi cha miaka ijayo.

Wananchi wa wilaya hii na majirani zake wanapaswa kuitumia bahati ya kuwa na chuo hiki pekee cha elimu katika kutimiza ndoto zao za muda mrefu za kujielimisha na hatimaye kupata shahada baada ya kuhitimu kikamilifu mafunzo yao.

Milango iko wazi wakitumie kwa shughuli mbali mbali zikiwemo shughuli za warsha, mikutano, semina na shughuli nyinginezo

SWALI:Baadhi ya wanafunzi wanaotaka kujiendeleza ni yatima. Je mna utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa wanapata fursa za kuelimika licha ya kukabiliwa na mazingira hayo magumu?

JIBU:Chuo chetu, kina utaratibu wa kutoa nafasi za kujielimisha kwa wanafunzi yatima wawili kila mwaka wenye sifa zinazotakiwa na upendeleo wa kipekee upo kwa wanafunzi wa wilaya yetu hii.Kwa hiyo ni vyema wakajisikia kuwa chuo chetu kinatambua hali waliyonayo na kina nia ya kuwaendeleza ili wamudu mabadiliko ya zama hizi za utandawazi.
SWALI:Je mna mipango gani ya baadaye?

JIBU:Mipango yetu ya baadaye ni kujenga shule ya msingi ambayo pia itatumika kwa mafunzo ya majaribio ya wanachuo wa daraja la A.

Ujenzi huo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa vyuo vyote vya daraja la A nchini.Ujenzi utaanza wakati wowote ardhi kiwanja kikipatikana.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.