|
Watafunaji fedha za MMEM hadi sasa hawaoni aibu?
2006-10-23 09:02:37
Na Mhariri
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Bi Hanifa Karamagi alifanya ziara ya kushtukiza katika kijiji kimoja wilayani humo na kupewa taarifa za kutafunwa kwa fedha nyingi za MMEM.
Afisa Elimu wa wilaya hiyo, Winfrida Mbuya, alimweleza DC huyo kuwa kiasi cha shilingi milioni 20 zimepotea katika kijiji cha Marui ambazo zilipelekwa huko na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na madawati katika shule ya msingi Marui-Mipera.
Mkuu huyo wa wilaya alipewa taarifa hiyo huku akishuhudia kwa masikitiko makubwa mifuko 30 ya saruji ikikaribia kuganda (kuharibika) huku majengo mawili ya nyumba za walimu yakiwa yametelekezwa katika hatua ya msingi.
Ni dhahiri majengo hayo yameachwa hivyo yalivyo kutokana na kukosekana na fedha ambazo ndizo hizo zilizoliwa na watu hao wasio na huruma wala upendo kwa nchi yao.
Wakati fedha hizo zikitafunwa, vyumba vya madarasa vilivyokuwa vimejengwa kuta zake zimeanza kupasuka kiasi cha kutishia maisha ya wanafunzi wa shule hiyo.
Kitendo hiki kinachodaiwa kufanywa na wajumbe wa kamati ya shule kinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote kwani kimerudisha nyuma mikakati ya serikali ya kuboresha elimu hapa nchini.
Ni kitendo kinachosikitisha hasa ikizingatiwa kwamba Kisarawe ni moja ya wilaya zilizo nyuma sana kielimu hapa nchini. Hilo halina ubishi.
Kwa mantiki hiyo, ingetarajiwa kwamba fungu la MMEM kwa maendeleo ya elimu wilayani humo lingetumiwa ipasavyo kujinasua katika hali hiyo duni. Hivi watafunaji wa fedha hizi hawaoni aibu kuendelea kudidimiza elimu maeneo yao?
Kwa miaka mingi wananchi karibu kila kona walikuwa wakilalamikia ukosefu wa madarasa, nyumba za walimu na madawati. Katika baadhi ya vijiji, wanafunzi walikuwa wanasoma chini ya miti kutokana na wananchi kutokuwa na uwezo wa kujenga madarasa.
Wananchi, wakiwemo wa wilaya ya Kisarawe, walikuwa hawaishi kuilalamikia serikali kutokana na watoto wao kusoma katika mazingira magumu.
Hata hivyo, kilio hiki kilisikika na hakika, kwa nia njema kabisa, ilianzisha mpango huu wa MMEM, lengo likiwa ni kuboresha elimu kuhakikisha wanafunzi kusomea katika mazingira mazuri na walimu nao wanaishi makazi yenye hadhi.
Leo hii wananchi hao hao wanapoamua kula fedha hizo za MMEM, nani wa kulaumiwa?
Wajumbe wa Kamati za Shule wanapaswa kuelewa kwamba fedha za MMEM ni mali ya umma na kwamba fedha hizo zinapaswa kutumiwa kwa maendeleo na sio kujaza matumbo yao.
Wajue kwamba wanapotumia fedha hizo kwa manufaa yao, wanadhulumu haki za wananchi ambao wanataka watoto wao wapate elimu ya kuondokana na hali ya umasikini hatimaye kuendeleza taifa lao.
Tunaunga mkono agizo lililotolewa na DC Karamagi la kuitaka Taasisi ya Kuzuia Rushwa pamoja na Kamanda wa Polisi wa Wilaya Kisarawe kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kashfa hiyo na kisha hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Pia tunatoa wito kwa wananchi vijijini na mijini kuwa na ujasiri wa kuhoji matumizi ya fedha za MMEM maana inavyoonekana, kuna tabia ya kulindana au kuogopana.
Tukiendelea kulindana na kuogopana, ni dhahiri fedha nyingi za umma zitaingia kwenye mifuko ya wachache badala ya kutumika kwenye miradi iliyokusudiwa.
|