24 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Uumuhimu wa masoko ya mitaji kwa maendeleo ya taifa
 
2006-10-24 09:03:11
Na Michael Kitulizo

Maendeleo ya taifa lolote duniani yanategemea upatikanaji wa mitaji.

Mitaji hii ndio hutumiwa na makampuni kuanzisha na kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuchangia katika ongezeko la pato la taifa na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mitaji hii yaweza kupatikana kwa njia kuu tatu. Njia hizo ni kutumia faida ya ndani iliyokusanywa kwa muda mrefu, kukopa na kukusanya mtaji kwa kuuza hisa katika soko la mitaji.

Makampuni au mashirika yanaweza kutumia njia yoyote kati ya hizo ila kutokana na ukweli kwamba faida ya ndani huwa haijitoshelezi na ugumu wa upatikanaji wa mikopo ya kutosha kwa ajili ya kutekeleza mipango fulani; makampuni/mashirika mengi hutumia njia ya tatu ambayo ni kuuza hisa kwa wananchi.

Kuuza hisa za kampuni kwa jamii ni suala linalohitaji maandalizi ya kutosha ili kutimiza matakwa na sheria za kushiriki katika masoko ya mitaji.

Lazima kampuni iweke wazi idadi ya hisa zilizopo, idadi ya hisa zitakazouzwa, thamani ya kila hisa na hivyo kiasi kinachotarajiwa kukusanywa kutokana na uuzaji wa hisa kwa jamii.

Pia kampuni itahitajika kueleza ni kwa namna gani itakavyotumia kiasi cha fedha kitakachokusanywa.

Ikumbukwe kuwa, kwa kununua hisa za kampuni, mwananchi anafanya uwekezaji kama zilivyo aina nyingine za uwekezaji na hivyo anategemea kupata faida kutokana na uamuzi wake huo.

Faida za uwekezaji kwenye hisa za makampuni zinatokana na aidha ongezeko la bei ya hisa au gawio linalotolewa na kampuni .

Hivyo basi kampuni inayouza hisa inatakiwa kuweka wazi mipango itakayotekelezwa kwa kutumia fedha itakayopatikana katika mauzo ya mwanzo na pia kuweka wazi matarajio ya baadaye ya ufanisi wa kampuni ili kumpa nafasi mwekezaji kuamua.

Kampuni pia inapaswa kuweka wazi matarajio na utaratibu wake katika kutoa gawio.

Kwa kuweka wazi hayo, mwekezaji atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya uchambuzi wa kutosha na kuamua kununua au kutonunua hisa za kampuni.

Kampuni hukusanya fedha za mauzo ya hisa katika mauzo ya mwanzo na baada ya kufikia malengo husika, kampuni huorodheshwa kwenye soko la mitaji ambapo mauzo na manunuzi ya hisa kati ya wawekezaji huanza.

Ijapokuwa mauzo na manunuzi haya ni ya hisa za kampuni iliyoorodheshwa, kampuni haitopokea au kutoa fedha za mauzo au manunuzi na badala yake mbadilishano huu unakua kati ya wawekezaji wenyewe.

Baada ya kuorodheshwa kwenye masoko ya mitaji, kampuni haitokuwa na uwezo tena wa kuamua bei ya hisa zake kama ilivyokua kwenye mauzo ya mwanzo.

Hapa ndipo ufanisi wa kampuni unapoamua bei ya hisa zake. Kila mwekezaji/mwananchi ana matakwa yake ambayo ni tofauti na ya mwingine na hivyo basi maamuzi yao huwa tofauti.

Matakwa haya yanajengwa kwenye misingi mikuu miwili; yaani kutaka kuwekeza kwa malengo ya baadae au kutaka kupata fedha kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya wakati huu.

Misingi hii ndio husababisha kuwepo kwa umuhimu wa kuuza ama kununua hisa. Mahitaji haya huletwa pamoja katika soko la hisa ambalo hutumika kukusanya matakwa tofauti ya wawekezaji.

Soko hili kama yalivyo masoko ya bidhaa nyingine linatumika kama daraja kuunganisha, kwa mlinganyo sahihi matakwa mbalimbali ya wawekezaji.

Muuzaji daima atamtafuta anayetimiza matakwa yake, yaani atatafuta mnunuzi mwenye bei ya juu na mnunuzi kwa upande wake atatafuta kununua kwa bei rahisi akitegemea kupata faida baada ya ongezeko la baadaye.

Ni katika mvutano (mnada) huo ndipo bei halisi ya hisa hutambulika.

Ikumbukwe kuwa, bei zinazohitajika na aidha mnunuzi au muuzaji zinatokana na mtazamo wao kuhusu ufanisi wa kampuni husika.

Kwa maana hiyo, kampuni iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa daima inajitahidi kuhakikisha kuwa ina ufanisi wa kutosha katika shughuli zake.

Kwa kufanya hivyo, kampuni itakuwa sio tuu inawajengea wawekezaji wake kujiamini kuwa watapata faida kutokana na uwekezaji wao lakini pia inaijengea kampuni heshima nzuri kwa jamii ambayo itasaidia sana katika kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa au huduma za kampuni.

Kutokana na hilo, kampuni daima itajitahidi kuongeza wingi na ubora wa bidhaa au huduma zake na kwa kufanya hivyo mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa unaongezeka.

Uchumi wa taifa unakua kutokanana ongezeko la mchango wa kampuni katika pato la taifa (kodi inayolipwa na kampuni na kuongeza ajira kutokana na ongezeko la uzalishaji.

Hivyo basi, kama masoko ya bidhaa mbalimbali yanavyotumika kutimiza malengo mbadala ya wananchi kujipatia huduma muhimu; soko la hisa linasaidia katika upatikanaji wa bidhaa za kifedha ambazo mara baada ya kupata huduma muhimu katika masoko ya bidhaa, mwananchi anahitajika kupata huduma hii ikiwa kama mojawapo ya njia muafaka ya kuwekeza akiba yake.

Kwa kuwekeza katika masoko ya hisa na mitaji; mwananchi atakuwa kwa namna ya kipekee anachangia katika upatikanaji wa mitaji itakayosaidia katika kujenga na kukua kwa uchumi wa nchi yetu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.