|
Tusherehekee Idd el-Fitri kwa amani
2006-10-24 09:03:49
Na Mhariri
Waumini wa Kiislamu nchini kote leo wanaungana na wenzao duniani kusherehekea sikukuu ya Idd el-Fitri, kufuatia kumalizika kwa mfungo wa Ramadhan.
Funga ya Ramadhan ni moja kati ya nguzo kuu tano za Uislamu.
Katika mwezi huo wa Ramadhan, waumini huacha kula na kunywa kuanzia alfajiri mpaka jioni.
Kitaifa, sherehe hii inafanyika mjini Arusha ambako Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Huko Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ghuba, sherehe za Idd zilianza jana Jumatatu kufuatia kuandama kwa mwezi katika nchi hizo juzi, lakini Misri na nchi zingine mbalimbali sikukuu ni leo baada ya mwezi kuandama jana.
Kufanyika kwa Idd el-Fitri kunatofautiana kati ya nchi na nchi kutegemea kuonekana kwa mwezi mpya ambao huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kiislamu.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuwatakia sikukuu njema waumini wa Kiislamu pamoja na Watanzania kwa jumla, kwani tunaamini hata wale ambao si Waislamu -- kutokana na utamaduni wa umoja, upendo na mshikamano waliojijengea Watanzania -- wataungana na wenzao katika kusherehekea sikukuu hii muhimu.
Tunapenda kutahadharisha pia kwamba kumalizika kwa Ramadhan sio mwanzo wa vitendo vya kumchukiza Mwenyezi Mungu. Hatutarajii kuona watu waliodumu kwenye mfungo kwa mwezi mzima wakijiingiza tena kwenye vitendo ambavyo haviendani kabisa na mafundisho ya dini.
Uzoefu wa muda mrefu unaonyesha kwamba watu hufurika katika sehemu za burudani kusherehekea sikukuu hii. Wengine hupeleka watoto wao pwani na sehemu zingine mbalimbali za burudani.
Lakini pia tumekuwa tukishuhudia matukio mbalimbali mabaya katika sikukuu hii, hasa ajali ambazo husababishwa na uendeshaji mbaya wa magari unaofanywa na madereva au watu waliokunywa pombe kupita kiasi.
Matukio kama hayo hakika, hatuyatarajii katika siku ya leo ambayo ni ya furaha kwa ndugu, jamaa na marafiki kutembeleana na kupeana mkono wa Idd.
Aidha, wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao, kwani mara nyingi watoto wamekuwa wakipotea katika siku za sikukuu kutokana na wazazi kutokuwa karibu nao.
Ni matarajio yetu pia kwamba vyombo husika na usalama vitakuwa macho kuhakikisha kwamba wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani na utulivu, hasa ikizingatiwa kwamba wahalifu wamekuwa wakitumia siku kama hizi kufanya hujuma mbalimbali katika makazi ya watu na sehemu za starehe.
Tunawatakia Idd njema.
|