|
Wanafunzi wa shule za msingi kushindanishwa kielimu
2006-10-25 08:58:33
Na RAYMOND KAMINYOGE
Ukuzaji wa elimu katika zama hizi za sayansi na teknolojia ni suala muhimu linalopewa kipaumbele na makundi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yenye lengo la kuona maisha ya wananchi yanaboreshwa zaidi.
Bodi ya Elimu ya Dk Didas inaandaa mashindano ya mitihani ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule msingi nchini wa ngazi mbalimbali ili kuwapata washindi watakaotunukiwa zawadi mbalimbali za motisha kwa lengo la kuinua maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa namna yoyote ile, mtoto anaweza kurithishwa urithi wa aina mbalimbali. Lakini urithi pekee ambao una manufaa na wa kudumu katika maisha yake yote ni kumpa elimu na siyo mali.
Mali yaweza kuporwa au kudhulumiwa na wajanja wasiowatakia mema, lakini siyo elimu aliyonayo mtu.
Watoto katika mazingira yoyote yale ya jamii wanatakiwa kujengewa msingi bora wa elimu ambao utawawezesha kufanya vizuri zaidi kimasomo katika ngazi zinazofuata.
Katika kuhakikisha kuwa watoto wanazingatia vyema masomo yao na kukabiliana na changamoto mbalimbali, hupimwa kwa vipimo mbalimbali ambavyo huamua kwa kiasi gani watoto wanazingatia mafundisho wanayofundishwa darasani au nje ya darasa.
Hatua hiyo hulenga kupima kiwango cha uelewa ili kuamua mbinu gani zitumike kuwaimarisha wanafunzi ambao hawajazingatia vyema mafundisho.
Mbinu na mikakati mbalimbali imekuwa ikitumiwa ili kuwahamasisha wanafunzi wapende kujifunza zaidi na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Shule ya sekondari ya Dk.Didas katika kujaribu kuibua vipaji vya wanafunzi na kuwatia shime wajifunze zaidi imeanzisha mashindano ya taaluma kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.Mashindano hayo yatafanyika mwakani.
Mashindano ya taaluma ni utaratibu mpya kwa watu wengi hapa nchini. Mashindano ambayo yamekuwa yakiwashirikisha sana wanafunzi ni yale ya michezo na burudani.
Mabadiliko ya kisayansi na teknolojia katika karne hii yanalazimisha kutumiwa mbinu za kila aina ili kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu bora inayokidhi mahitaji ya zama hizi.
Kuwepo kwa Teknolojia ya Mawasiliano na Habari ni changamoto nyingine ambayo inatakiwa kuhakikisha kuwa vijana wanafunzi wanaandaliwa ili kujenga taifa la watu werevu wanaokwenda sambamba na mabadiliko hayo vinginevyo taifa litakuwa limeachwa nyuma.
Bodi ya shule ya sekondari ya Dk.Didas imebuni mashindano ya kitaaluma ambayo yatawashirikisha wanafunzi wote kulingana na vigezo mbalimbali vitakavyowekwa.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk.Didais Massaburi anasema mpango huo wa aina yake ambao ni wa kwanza kuanzishwa nchini watauratibu kwa utaratibu maalum ambao utakuwa wazi kwa shule zote.
Tunataka kugeuza macho na masikio ya watu wetu yazingatie umuhimu wa elimu ikiwa pamoja na kuzingatia umuhimu wa mashindano ya kitaaluma.
Tumekuwa na mazoea ya kuona mashindano ya urembo wa viwango mbalimbali hadi kitaifa, binafsi nayapongeza sana, lakini sasa tugeukie katika mashindano ya kitaaluma anasema.
Kwa mujibu wa Dk.Massaburi mpango huo utazingatia zaidi kuibua na kuwazawadia watoto wenye uwezo mkubwa na mzuri zaidi kupitia ushindani wa kitaaluma.
Lengo ni kuwaandaa wataalam wa baadaye katika taifa letu kwa kuwapatia zawadi wale wanaofanya vizuri, anasema.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa kwa mujibu wa Dk.Massaburi anasema, ni lazima kwanza uungwe mkono na wadau wote wanaopenda maendeleo ya elimu nchini wakiwemo wazazi.
Mwenyekiti huyo wa bodi anabainisha kwamba utaratibu huo wameufanyia majaribio kwa kuandaa mashindano ya mkoa wa Dar es Salaam. Mashindano hayo yalifanyika Septemba 16 mwaka huu katika shule ya msingi ya Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Shule zipatazo 27 zilishindanishwa ambapo wanafunzi 20 bora waliibuka washindi na kupewa zawadi mbalimbali kama motisha kwao.
Akizungumzia utaratibu huo wa mashindano,anasema katika ngazi ya shule wanateuliwa wanafunzi bora ambao wanakwenda kushindana katika wilaya, mkoa, kanda na taifa.
Kwa mashindano ya mkoa wa Dar es Salaam, miongoni mwa zawadi zitakazotolewa kwa washindi kupitia mpango huo ni kwamba, mwanafunzi atakayeshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu kwenye mashindano hayo watafanya mtihani wa kuingia katika shule ya sekondari ya Dk.Didas na watalipiwa asilimia 50 ya ada katika kipindi chote watakachoelimika shuleni hapo.
Halikadhalika kama sehemu ya motisha kwao,Septemba 30 mwaka huu wanafunzi bora 20 wote walipatiwa fursa ya kwenda Bagamoyo, kama sehemu ya ziara ya kitaalam kwenda kujionea urithi wa kihistoria katika eneo hilo.
Katika mpango huo wa majaribio, mwanafunzi wa kwanza alizawadi seti ya kompyuta na mashine ya kuchapia, baiskeli, seti ya vitabu vya masomo ya sekondari, seti ya vifaa vya hisabati, daftari kubwa tatu na cheti cha utambulisho.
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili, alijipatia seti ya kompyuta, vitabu mbalimbali , seti ya vifaa vya hisabati, daftari tatu na cheti.
Mwanafunzi wa tatu alizawadiwa baiskeli, vitabu mbalimbali seti ya vitendea kazi vya hisabati, daftari tatu na cheti cha utambulisho.
Dk.Massaburi anasema mashindano hayo yametoa mwelekeo mzuri unaotoa picha halisi na uthibitisho kuwa mashindano hayo kwa ngazi ya taifa yanawezekana.
Mpango huo wa majaribio umetoa mwanga kwamba mashindano hayo mwakani yatafanikiwa kwa kuwashirikisha wanafunzi wengi wa shule katika ngazi za wilaya, ambazo nazo zitatoa wanafunzi watakaokwenda kushiriki katika ngazi ya mkoa.
Wanafunzi hao watapata fursa ya kushindana na wenzao katika ngazi ya kanda ambazo hatimaye zitatoa mshindi wa kitaifa.
Kwa utaratibu uliopangwa ni kwamba, Bodi tutakuwa waratibu, tutashirikiana na wadau wengine katika ngazi za chini kuendesha mashindano haya kwa ufanisi zaidi,\ anasema.
Wanafunzi watakaoibuka katika mashindano hayo watapatiwa zawadi mbalimbali ambazo zitakuwa kumbukumbu muhimu katika maisha yao, ikiwa pamoja na kutoa changamoto kwa wanafunzi wengi zaidi kufanya bidii ya kushinda katika miaka ijayo.
Miongoni mwa zawadi zinazotarajiwa kutolewa kwa washindi ni gari dogo la kutembelea na fursa za kulipiwa ada za shule.
Mshindi akikabidhiwa zawadi, uamuzi utakuwa wa kwake, kama aliuze gari hilo ama alitumie kwa shughuli zake binafsi anasema.
Zawadi za washindi wengine zitatangazwa rasmi wakati wa mashindano hayo yatakapoanza, kulingana na wadhamini watakavyojitokeza kudhamini mashindano hayo.
Tunaamini kuwa moyo wa kiushindani miongoni mwa makundi haya utachangia sana kuinua na kuboresha elimu nchini na hivyo kulifanya taifa kupiga hatua za uhakika katika sekta ya elimu, anasema.
|