25 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Walimu nao waache kukimbilia mijini
 
2006-10-25 08:59:13
Na Mhariri

Suala kwamba nchi yetu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa shule za msingi na sekondari, halina mjadala wala ubishi.

Shule nyingi, hususan za msingi, zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa watoto kukosa elimu wanayotakiwa kupata.

Lakini shule mbili zenye jumla ya wanafunzi 600 zinapokuwa na walimu watano tu, hii ni hatari kubwa.

Kimahesabu, ni kwamba mwalimu mmoja anapaswa kufundisha watoto 120!

Hivyo ndivyo ilivyo katika shule mbili za msingi za Isene na Isanzu wilayani Iramba, mkoa wa Singida.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Isene, Bw. Hamisi Magema alikaririwa akisema kwamba walimu wachache waliopo wamekuwa wakitumia muda mwingi zaidi kufundisha darasa la saba, huku madarasa ya chini yakikosa walimu, hali ambayo alisema inahatarisha kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule hizo.

Moja ya sababu zilizotolewa za upungufu wa walimu katika shule hizo ni kwamba walimu wanaopangiwa kwenda kufundisha katika shule hizo hugoma kwa madai kwamba ziko mbali na huduma za jamii ni duni.

Hatujui walimu wanaogoma kuripoti kwenye vituo wanavyopangiwa wanafanywa nini...wanapangiwa shule nyingine?

Au wanakula njama na baadhi ya watendaji wa halmashauri ili wapelekwe kwenye shule wanazotaka wao? Ni baadhi tu ya maswali tunayojiuliza.

Ndio maana haishangazi kuona katika shule za mijini walimu wakirundikana katika shule moja huku shule za vijijini zikitaabika kwa kukosa walimu.

Hii ina maana kwamba kila mwalimu anataka kufundisha mjini na ili kuhakikisha wanafanikisha hilo, wapo tayari kutoa hongo ya kiasi chochote ili mradi tu wafundishe mjini. Huu ni ukweli ulio dhahiri.

Ni kweli pia kwamba katika nchi yetu kuna huduma duni za jamii katika vijiji vingi. Walimu na watumishi wengine wa Serikali hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma na mishahara yao wilayani.

Mbali na ukweli huo, walimu wasisahau kwamba watu wanaoishi katika maeneo hayo ni wenzetu na kwamba nao wanahitaji kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

Walimu, kama walivyo watumishi wengine, nao wanao wajibu wa kushiriki katika ujenzi wa taifa letu, mijini na vijijini. Wanapaswa waondokane na kasumba ya kukimbilia mijini.

Kwa hili nalo, serikali inao wajibu wa kuongeza kasi zaidi ya kupeleka huduma vijijini ili watumishi waende huko kufanya kazi za ujenzi wa taifa bila bughudha.

Tunaamini kama kila kijiji kitakuwa na huduma bora za jamii kama vile maji, afya, elimu na usafiri wa uhakika, vijijini kutakuwa ndiko kimbilio la watumishi wengi na kasumba ya kukimbilia mijini itabaki kuwa historia.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.